23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

CUF wagoma rasmi

Pg 1*Watangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio

*Wadai CCM inafanya njama kujitangazia ushindi

 

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetangaza rasmi kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Machi 20, kwa kile walichodai kuwa ni batili kisheria na kikatiba.

Kinadai kuwa uchaguzi huo uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salum Jecha si halali kwa kuwa ule wa halali ulikwishafanyika Oktoba 25, mwaka jana na kumalizika kwa amani.

Tamko la Baraza Kuu la CUF lilisomwa na Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, lilisema uamuzi huo umetokana na makubalino yaliyofikiwa katika mkutano wa Baraza hilo lililoketi jijini humo juzi na jana.

“Baraza Kuu ndicho chombo cha juu cha uamuzi baada ya Mkutano Mkuu wa Taifa katika chama, hivyo baada ya kikao hicho tulichokifanya jana ofisi za Buguruni tuliamua kwamba hatutashiriki katika uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, 2016 kwa sababu uchaguzi huo si halali kwa kuwa ule wa halali ulishafanyika,” alisema Taslima.

Alisema katika mkutano huo walijadili pia mwenendo wa hali ya kisiasa Zanzibar tangu ZEC ilipotoa tamko la kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo, ambalo Jecha alilitoa Oktoba 28, mwaka jana.

Hata hivyo, alisema Baraza pia limesikitishwa na kushangazwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kuandika barua na kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari kutaka vyama vya siasa vishiriki uchaguzi wa marudio Machi 20, Zanzibar bila ya kujali kwamba uchaguzi huo ni haramu na unakiuka matakwa ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Nam. 11 ya 1984.

“Baraza Kuu halikutarajia mtu mwenye hadhi ya ujaji kufanya kazi ya kutumikia masilahi ya watawala ambao wameamua kuvunja katiba na sheria za nchi yetu na kukanyanga misingi ya haki na demokrasia, huku akishindwa kukemea uhuni mkubwa uliofanywa wa kubaka demokrasia na haki za bindamu,” alisema Taslima.

 

UKIMYA WA DK. MAGUFULI

Aidha CUF imehoji ukimya wa Rais Dk. John Magufuli kukwepa dhamana na wajibu wake kama mkuu wa nchi na amiri jeshi mkuu kwa kuiacha njiani kazi aliyoianza ya kutafuta ufumbuzi wa mkwamo wa kisiasa uliosababishwa na uchaguzi mkuu uliofutwa kwa ubabe na matakwa ya watu wachache.

“Baraza Kuu linamtaka Rais Magufuli kujitathmini na kujiuliza anatoa taswira gani mbele ya macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa kutokana na kutosimamia ahadi yake aliyoitoa mbele ya Watanzania wakati akilizindua Bunge jipya kwamba atafanya kazi na vyama vya CUF na CCM ili kuupatia ufumbuzi mkwamo huu,” alisema Taslima.

 

MAAZIMIO YA CUF

Mkutano huo wa CUF ulitoka na maazimio  12 likiwamo la kutoingia kwenye uchaguzi wa marudio kwa sababu Zanzibar imeshafanya Uchaguzi Mkuu halali Oktoba 25 na kukamilishwa kwa kupatikana kwa wajumbe halali wa Baraza la Wawakilishi na madiwani ambao walipewa shahada za kuwathibitisha na kuwatambua kisheria na kikatiba.

Katika maazimio hayo, chama hicho kiliainisha kuwa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar matokeo yalikwishabandikwa nje ya vituo vya majumuisho vya majimbo yote 54, na kilichokuwa kinaendelea baada ya hapo ni kuhakiki matokeo hayo kutoka majimboni, na kazi hiyo ilikwishakamilika kwa majimbo 40 na katika hayo, matokeo ya Uchaguzi wa Rais kwa majimbo 31 yalikwishatangazwa kabla ya Mwenyekiti wa ZEC kutangaza isivyo halali kwamba ameufuta uchaguzi huo.

“Hakuna kifungu chochote cha Katiba ya Zanzibar au Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar kinachotoa uwezo kwa mwenyekiti wa ZEC na hata kwa tume yenyewe kufuta uchaguzi au kuitisha uchaguzi wa marudio,” alisema Taslima.

Azimio jingine lililotolewa na baraza hilo ni kulaani matumizi ya nguvu kubwa yaliyotumiwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano na vikosi vya SMZ dhidi ya wananchi wasio na hatia.

 

WITO KWA JUMUIYA ZA KIMATAIFA

Pamoja na mambo mengine, baraza hilo la CUF limetoa wito kwa jumuiya akiwamo Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kufanya uchunguzi wa kauli na matendo ya uhalifu, uvunjwaji wa haki za binadamu na ubaguzi ambao umekuwa ukifanywa dhidi ya wananchi wa Zanzibar.

Aidha baraza hilo pia limezipongeza taasisi na jumuiya zote za kitaifa, kimataifa za kikanda zikiwamo Jumuiya ya Madola, Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na nchi za Marekani na Uingereza kwa kuwaunga mkono Wazanzibari na kutetea haki yao ya kidemokrasia na uamuzi halali walioufanya kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015 kwa kutaka mchakato wa uchaguzi ukamilishwe na matokeo yake kutangazwa.

Taasisi nyingine ni pamoja na jumuiya za dini, haki za binadamu, vyombo huru vya habari, vyama vya vya siasa, Wazanzibari na Watanzania wote wanaopenda amani na demokrasia kwa msimamo wao wa kutetea uamuzi wa Wazanzibari walioufanya katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, 2015.

 

MAALIM SEIF

Akijibu maswali ya wanahabari katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alisema hawako tayari kuhalalisha haramu kwa kuingia kwenye uchaguzi huo.

“Mwanzo tulikataa uamuzi wa Jecha kufuta uchaguzi kwa sababu hatua hiyo ilikuwa haikubaliki kisheria na kikatiba, hivyo kama tutakubali kuingia kwenye uchaguzi wa marudio itatoa tafsiri kwamba tulikubaliana na matamko ya Jecha,” alisema.

Maalim Seif alisema marudio ya uchaguzi huo yamepangwa na CCM kujihakikishia ushindi na kuna taarifa kwamba wamejipanga kumtangaza Dk. Mohammed  Shein usiku baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo.

Mgombea huyo alisema suala la wao kugomea uchaguzi wakati kuna vyama vingine vidogo vitashiriki na hivyo kuupa uhalali uchaguzi huo alisema hatishiki nalo kwa sababu anajua havina uungwaji mkono.

“Tumepata taarifa kwamba katika marudio CCM wamejipanga kujipatia ushindi hata kama tukishiriki au tukigoma kushiriki, wameshajipanga hata kama tutaingia na kushinda hatutapewa ushindi wa urais, hivyo tumeona bora kuacha kushiriki kwenye haramu,” alisema Maalim Seif.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles