31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

CUF isipeperushe bendera ya Hizbu – CCM

30Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetakiwa kukichukulia hatua za kisheria Chama cha Wananchi (CUF) kwa madai ya kupeperusha bendera ya zamani ya chama cha Afro Shiraz Party (ASP) kinyume na sheria namba 5 ya mwaka 1992.
Tahadhari hiyo kwa msajili na vyombo vya dola imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka alipokaribishwa kuhutubia katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana katika Uwanja wa Magereza, Mkoa wa Mjini Magharibi kisiwani hapa.
Shaka alisema kwa mudu mrefu kumekuwa na ukiukaji huo wa sheria ukifanywa na viongozi wa CUF na wafuasi wake, wakipeperusha bendera yenye rangi ya ASP kwenye mikutano yao ya hadhara na kusema inatokana na CCM.
“Tunazitaka mamlaka za kidola na ofisi ya msajili hapa Zanzibar kukizuia chama cha CUF kiache kupeperusha bendera ya ASP, CUF hawana nasaba na ASP, asili yao ni ZNP, tumevumilia sasa hatutakubali tena dhihaka hiyo,” alisema Shaka.
Alisema kitendo cha kutumia kaulimbiu, bendera au alama za chama kilichofutwa kisheria ni kosa, hivyo inashagaza kuiona CUF ikuvunja sheria na kutazamwa bila kuchukuliwa hatua za kisheria na msajili wa vyama vya siasa.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi mstaafu Ali Abeid Karume, alisema ubora wa CCM haujatetereka kwa sababu ni chama kinachoheshimu misingi yake tofauti na vyama vingine vilivyokosa dira, sera na dhamira ya kuwatumikia wananchi.
Balozi Karume ambaye ni mtoto wa pili wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Mzee Abeid Karume alisema chini ya misingi hiyo wananchi kwa hiari yao wameemdelea kukiamini na kila wakati kitaendelea kushinda na kuongoza taifa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa CCM, Kinana, alisema licha ya CUF kupewa wizara kadhaa katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini imeshindwa kuonesha ubunifu na uwezo wa kiutendaji na kujikuta siku zote viongozi wake wakipiga maneno bila vitendo.
Alisema kazi ya chama tawala ni kufikiria jinsi ya kuiletea nchi maendeleo kiuchumi na si kupiga soga au kutoa ahadi zisizotekelezeka kama wafanyavyo CUF na viongozi wake.
“Mmepewa Wizara ya Viwanda na Biashara, hata kiwanda kimoja kimewashinda kujenga, mnaongoza Wizara ya Afya, hata chumba kimoja cha zahanati hamjajenga, wananchi wamewapima na sasa wako tayari kuwakataa na kutowategemea kwa lolote,” alisema Kinana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles