25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

CHUO CHA MISITU OLMOTONYI CHAPEWA MAELEKEZO

Na HAMZA TEMBA – WMU

CHUO cha Misitu Olmotonyi kilichopo mkoani Arusha, kimetakiwa kuboresha taaluma na mitaala ya kufundishia iweze kukidhi mahitaji ya jamii ya sasa na ijayo, ikiwemo kujibu kero na changamoto zinazoikabili jamii hiyo.

Agizo hilo limetolewa  jana mjini hapa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alipotembelea chuo hicho kwa ajili kukagua maendeleo yake na kuzungumza na walimu pamoja na wafanyakazi ambapo pia alikagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayojengwa chuoni hapo, ikiwemo ya bweni na ukumbi wa mihadhara.

Alisema Tanzania ya leo inahitaji wataalamu watakaojibu kero na kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya uhifadhi nchini ikiwemo ya uharibifu wa misitu kwa njia ya uchomaji wa mkaa, uvunaji haramu wa magogo na vitendo vya uingizaji wa mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini.

“Ni lazima muwafundishe wanafunzi wenu uaminifu na uzalendo wa kutumia rasilimali za misitu kwa njia endelevu, muwafundishe uhifadhi zaidi na si uvunaji pamoja na kutumia sheria ipasavyo katika kulinda na kusimamia rasilimali hizi, huku wakitambua kuwa rasilimali hizo zikitoweka hakuna maisha kutokana na umuhimu wake katika maisha ya binadamu,” alisema Prof. Maghembe.

Kutokana na hali hiyo, alikitaka chuo hicho kujiimarisha zaidi katika mafunzo kwa vitendo kufikia viwango bora vinavyotakiwa, ikiwa ni pamoja na kuendeleza walimu kitaaluma kwa kutumia fursa mbalimbali, ikiwemo za mafunzo ya nje ya nchi kwa mfumo wa ‘Scholarships’.

Alikitaka pia chuo hicho kujikita zaidi katika utoaji wa huduma kwa jamii katika sekta ya misitu pamoja na kuanzisha na kuimarisha programu mbalimbali za utafiti ambazo pamoja na faida nyingine pia zitakitangaza chuo hicho ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Prof. Maghembe amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya United Builders Ltd, Harshad Patel, kukamilisha haraka ujenzi unaoendelea wa jengo la bweni na ukumbi wa mihadhara chuoni hapo. Ujenzi huo upo chini ya mradi wa ECOPRC na jengo la bweni litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 na ukumbi wa mihadhara wanafunzi 200.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Christognus Haule, alisema chuo hicho kinatoa mafunzo ya misitu na hifadhi ya mazingira kwa ngazi ya astashahada na stashahada pamoja na mafunzo ya muda mfupi.

Pia kinatoa huduma za ushauri na utafiti wa misitu na hifadhi ya mazingira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles