25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CHIPSI ZASABABISHA SHINIKIZO LA DAMU KWA VIJANA

 

 

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

ULAJI wa nyama choma na chipsi umetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochochea watu wengi hasa vijana kupata shinikizo la juu la damu.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk. Pedro Pallangyo, alipozungumza katika mahojiano maalumu na MTANZANIA Jumapili.

Dk. Pallangyo alisema vyakula hivyo huchochea hali hiyo kutokana na matumizi makubwa ya mafuta yanayotumika kuviandaa na chumvi nyingi inayotumika wakati wa kula.

“Jinsi vyakula hivyo vinavyoandaliwa mafuta mengi hutumika na wakati wa kula watu hupendelea kuweka chumvi nyingi, jambo ambalo ni kosa. Ulaji huu si mzuri kiafya,” alisema.

Dk. Pallangyo ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utafiti na Mafunzo wa JKCI alisema katika miaka ya nyuma idadi kubwa ya watu katika nchi zilizoendelea ndiyo walikuwa wakipata tatizo hilo lakini sasa idadi kubwa inagundulika katika nchi zinazoendelea.

Alisema mbaya zaidi watu wanaokutwa na tatizo katika nchi zinazoendelea ni wale walio katika umri wa uzalishaji.

“Katika nchi zilizoendelea wastani wa umri wa watu wanaokutwa shinikizo la damu ni wale walio juu ya umri wa miaka juu ya 50 na kuendelea.

“Lakini kwa upande wa nchi zinazoendelea, hasa zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo,  picha ni tofauti. Huku wanaokutwa na tatizo ni wenye umri wa miaka 35 hadi 45, yaani kwa wenzetu ugonjwa huu unajulikana kwamba ni wa watu wazima huku kwetu ni ugonjwa wa vijana,” alisema.

Pia alisema tafiti zinaonesha magonjwa ya moyo yanachangia theluthi moja ya vifo vyote vinavyotokea duniani na zaidi ya asilimia 50 ya vifo hivyo vinatokana na shinikizo la juu la damu.

“Utafiti mmoja uliowahi kufanywa katika nchi 23 Barani Afrika, Tanzania ikiwamo ulionesha shinikizo la damu ni sababu ya moyo kushindwa kufanya kazi na kusababisha vifo vya ghafla,” alisema.

Dk. Pallangyo alisema katika nchi hizo ilionekana asilimia 86 ya magonjwa yote ya moyo yanatoka na shinikizo la damu.

“Hapa JKCI kwa miaka mitatu iliyopita tumeweza kufanya utafiti mbalimbali, utafiti huo ulihusisha watu waliopo kwenye jamii na wagonjwa waliolazwa wodini, kwenye jamii asilimia kati ya 42 hadi 56 ya wagonjwa wote tuliowapima walikutwa na shinikizo la juu la damu.

“Asilimia 35 hadi 47 ya wagonjwa waliokuwa wodini wengi mioyo yao ilikuwa imeshindwa kufanya kazi na kusababisha shinikizo la damu,” alisema.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles