23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CHINA YACHANGIA UJENZI WA CHUO CHA UONGOZI KIBAHA

NA PATRICIA KIMELEMETA

SERIKALI ya China imechangia zaidi ya Sh. bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Uongozi cha Kimataifa, kilichopewa jina la Mwalimu Julius Nyerere.

Jiwe la msingi la chuo hicho kinachotarajiwa kujengwa Kibaha, mkoani Pwani, limewekwa leo na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli kwa kushirikiana na vyama sita vya ukombozi barani Afrika pamoja na chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Akizungumza katika hafla Dk. Magufuli alisema Serikali ya China kupitia CPC wametoa zaidi ya Sh. bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi huo.

“Serikali ya China kupitia chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo wameweza kutoa zaidi ya Sh bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki kwa nchi sita zilizopigania Uhuru,” alisema Magufuli.

Chuo hicho kinahusisha vyama sita vya ukombozi barani Afrika ambavyo ni CCM (Tanzania) FRELIMO (Msumbiji), ANC (Afrika Kusini), SWAPO (Namibia),  ZANU-PF na MPLA  (Zimbabwe).

Ujenzi wa chuo hicho kinachotarajiwa kutoa mafunzo ya Itikadi na Uongozi unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili.

Chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kutoa mafunzo ya muda mfupi yatakayochukua muda wa miezi mitatu, mafunzo ya kati ya mwaka mmoja na mafunzo ya muda mrefu ya miaka mitatu.

“Tunaamini mafunzo yatakayotolewa katika chuo hiki yataweza kuwapika vijana wa Afrika kiuongozi na kiitikadi ili wawe viongozi bora katika Bara hili kupitia nchi zao,” alisema.

Alisema imefika wakati wa nchi kutoa mafunzo ya uongozi kwa vijana wao ili waweze kuwa chachu ya maendeleo na kutetea maslahi ya nchi zao.

Dk. Magufuli aliwashukuru, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na aliyekua Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdurlahaman Kinana kwa kushirikiana na viongozi wa nchi hizo kujadili ujenzi wa chuo hicho.

Katika kutia hamasa Dk. Magufuli aliwataka makatibu wakuu wa vyama hivyo kukutana na kujadili masuala yaliyobaki ili ujenzi utakapomalizika kianze kutoa mafunzo mara moja.

Alisema wananchi wa Mkoa wa Pwani wanapaswa kuchangamkia fursa zilizopo wakati wa ujenzi huo ikiwamo ajira na kujiepusha vitendo vya wizi wa nondo na mafuta.

Mwenyekiri huyo wa CCM ambaye pia ni Rais wa Tanzania, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kuhakikisha barabara zinazokwenda chuoni hapo zinawekwa lami bila ya kuathiri nyumba na mali za wananchi na ikiwezekana waweke lami kwenye  barabara ya zamani.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa CPC ,Song Tao alisema ujenzi wa chuo hicho utaleta maendeleo katika nchi za Afrika na kuondoa ubeberu.

Alisema chama hicho kimepanga kuvijengea uwezo vyama vya Afrika ili viweze kujiongoza na kupata maendeleo.

Aliongeza, China imelenga kuleta mabadiliko katika nchi za Afrika  na hivi karibuni, Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping atakutana na viongozi wa Afrika jijini  Beijing  ili kujadili maendeleo ya bara hili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles