33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

‘CHID BENZ AMENITOA CHOZI’

chidi-benziii

NA MWANDISHI MAALUM

ETI miye ni mgumu sana wa kutoa machozi? Hapana sina ushujaa huo hata kidogo. Kuna mengi huwa yananiliza, bahati nzuri siku zote huwa ninakuwa na staili yangu ya kulia.

Yapo yale yanayonifanya nilie kimoyomoyo huku nikiweka nadhiri ya kulipa kisasi kwa yule anayenifanya nitokwe na machozi hayo.

Sasa ukiniona natoa machozi hadharani, ujue kwamba yamenifika hadi pomoni. Ni kama vile walivyosema Msondo Ngoma…. ‘Ukimuona mtu mzima analia (…mbele za watu) ujue kuna jambo.’

Yaap! Leo nimelia, ndiyo nimeumizwa baada ya kuziona picha za mdogo wangu… nyie huwa mnamuita Chid Benz au Chid Benzino. Lakini miye namfahamu zaidi kwa jina la Rashid Makwilo.

Ndiyo. Namfahamu Rashid tangu akiwa mdogo, akiwa anachezea makamasi pale Ilala Flat’s jijini Dar es Salaam.
Kuna watu wanaweza kuthibitisha hili; Afarat Bakari, Bora Mafaa ambao tulikuwa wakubwa kwa Rashid pale Ilala, tukicheza soka na kaka yake Man Makwilo.

Nini kinachoniumiza? Kuna wakati unajiuliza nini kimemkuta Rashid? Mtoto wa mtaani na kwa nini anapotea?

Nikiri wazi kwamba, tangu mapema sikuwa nikipendezwa na tabia zake za ubabe, ingawaje kuna kipindi niliwahi kuwaza kwamba ni utoto tu unaomsumbua na kwamba  pindi akikua ataachana na tabia hizo.

Lakini pia nilihisi ni ile tabia (kama sio ugonjwa wa utoto wa mjini) ilichangia kumtesa. Nikuambie kitu?
Siye watoto wa mjini huwa tuna ugonjwa mbaya sana.

Tunajiona tunajua na tuna uhuru wa kufanya kila kitu. Tunahisi hakuna wa kuweza kutuambia kitu.
Sababu kubwa ni kuzaliwa mjini! Hii kitu inatufanya tuwe viburi sana na kuweza kufanya maamuzi bila ya kutafakari kwa kina.

Katika kuthibitisha hilo, ndiyo maana utawakuta watoto wa mjini wachache sana wanaoweza kukubali kuajiriwa na kutumikishwa kwa kazi za kuingia saa 2:00 asubuhi na muda wa kutoka haujulikani.

Wengi wetu tulizoea kufanya starehe bila ya kufanya kazi, ndiyo mtoto wa mjini hana shida na sehemu ya kulala, hajiulizi pesa ya kula… hana haja ya kuhonga… ukimuajiri utampa sh’ngapi?

Binafsi nimeshapitia hatua hizi. Nilikuwa kiburi, mjeuri na mgomvi kama Rashid. Ndiyo maana niliamini kwamba dogo akikua ataacha tu kama miye nilivyoacha.

Lakini bahati mbaya dogo akaingia kwenye vitu vingine vibaya zaidi. Siyo ukorofi tu, akakubali akili yake itawaliwe na vilevi haramu.

Taratibu akavuka mipaka na kuingia katika matumizi ya ‘Albadili ya Kiarabu’ (unga). Acha wengine tumshukuru Mungu.

Rashid aligusa kitu ambacho watoto wa mjini siku zote tulikuwa tunaambiana kuwa tusikiguse kwa kuwa tuliamini kwamba unga haukuwa umeletwa kwa ajili yetu bali ni kwa wale washamba.

Tuliamini kwamba mtoto wa mjini anaweza kushiriki kuuza unga lakini si kujaribu kuuonja. Kauli mbiu yetu ilikuwa ‘Unga hautestiwi’.

Ona sasa Rashid ametuangusha, ameutesti. Gari limewaka hakuna mtu wa kulizima tena. Leo unga unamwangamiza mdogo wetu, hautaki kumwacha na hakuna wa kuweza kumnusuru tena!

Akili yake ya utoto wa mjini imepitiliza na kumharibu, dogo, hawezi tena kumsikiliza mtu yeyote. Hawezi kuacha ‘handasi’ ya unga kwani imemteka akili yake na anajiona mjanja kuliko mtu mwingine yeyote duniani.

Anaamini kwamba anachokifanya ni kitu sahihi zaidi kwa kuwa mtoto wa mjini huwa hakosei! Ni lazima itakuumiza kama kweli unafikiria maisha ya mdogo wako aliyekuwa na haiba kama ya Rashid kisha anatumbukia kwenye utumiaji wa madawa ya kulevya.

Najaribu kumkumbuka kaka yake, Man Makwilo ambaye yuko Marekani, anawezaje kumsaidia mdogo wake?
Kwani Rashid hawezi kutusukiliza sisi watoto wa mjini wenzake. Nikiangalia picha hizi za Rashidi inaniumiza sana, inanisikitisha na ni zaidi ya unavyoweza kufikiria. Leo machozi yamenitoka.

 

Andiko hili limeandikwa  na Mohammed Kuyunga na kuweka katika ukurasa wake wa Facebook, Desemba 30, 2016, saa 2:32 usiku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles