23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CHELSEA WAMALIZA KAZI LIGI KUU ENGLAND

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

HATIMAYE klabu ya Chelsea imefanikiwa kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, baada ya mwishoni wa wiki iliyopita kufanikiwa kushinda bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao, West Brom.

Ubingwa huo wameweza kuutangaza huku ikiwa imebaki michezo miwili Ligi hiyo kumalizika, wingi wa pointi walizozipata msimu huu, 87 zilitosha kutangaza ubingwa dhidi ya wapinzani wao, Tottenham ambao waliachwa kwa pointi 10.

Hata kama michezo iliyobaki Tottenham wanaweza kushinda yote, na Chelsea wakapoteza yote, bado Chelsea wanaendelea kuwa mabingwa kwa kuwa hakuna klabu ambayo inaweza kuzifikia pointi hizo cha Chelsea.

Kocha wa Chelsea, Antonio Conte, amewatangazia mashabiki wa klabu hiyo na viongozi kuwa kazi waliyomtuma na wachezaji wake kuifanya msimu huu tayari ameikamilisha kama walivyotaka, kilichobaki ni kusherehekea mitaa ya jiji la London.

Ubingwa huo ni wa sita kwa Chelsea katika michuano ya Ligi Kuu nchini humo, huku mara yao ya kwanza kuchukua ilikuwa msimu wa 1954/55, mara ya pili ikiwa 2004/05, 2005/06, 2009/10, 2014/15 na msimu huu.

Conte amesema ni furaha kubwa kwake kuweza kuingia kwenye michuano ya England msimu huu kwa mara ya kwanza na kutwaa ubingwa, japokuwa alikutana na ushindani wa hali ya juu dhidi ya makocha wenzake kama vile, kocha wa Tottenham, Mauricio Pochettino, Jurgen Klopp wa Liverpool, Pep Guardiola wa Manchester City na wengine wengi.

“Huu ni msimu bora sana kwangu, kwa kuwa nimeingia kwa mara ya kwanza kwenye michuano ya Ligi Kuu nchini England na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, haikuwa kazi rahisi kufanya makubwa hayo, lakini kupambana pamoja na ushirikiano vimetufanya tuwe mabingwa msimu huu.

“Nilikuwa na wakati mgumu dhidi ya uwezo wa kocha Pochettino, kwa kuwa kikosi chake kilikuwa na ushindani wa hali ya juu katika michuano hiyo, lakini tuliweza kupambana kwa kiasi kikubwa na kuweza kumshinda.

“Nimejifunza mengi katika ushindani wa Ligi hiyo na ninaamini nimepata uzoefu wa hali ya juu, niwapongeze wale wote walioleta ushindani, ninaamini wao wametufanya tuwe hapa kwa sasa, nawashukuru mashabiki wote kwa sapoti yao, viongozi na wadau mbalimbali wa timu hii.

“Nawapongeza wachezaji kwa ushirikiano waliouonesha kipindi chote na kufanya yale ambayo viongozi, mashabiki na wadau mbalimbali waliyataka kuyaona kutoka kwetu,” alisema Conte.

Kocha huyo alianza kuwapa mashabiki matumaini ya ubingwa msimu huu mara baada ya kushinda michezo 13 mfululizo, hivyo mashabiki hao walikuwa na imani na ubingwa msimu huu.

Hata hivyo, kocha huyo ameonesha kuwa kazi bado haijakamilika, hivyo amewataka wachezaji wake kuendelea kupambana kuhakikisha wanatwaa na taji la michuano ya Kombe la FA dhidi ya wapinzani wao, Arsenal katika fainali itakayopigwa wiki ijayo, Mei 27.

“Bado tunahitaji kuendelea kuweka historia nyingine msimu huu, japokuwa ligi imemalizika, lakini tuna kazi ngumu katika mchezo wa fainali wa Kombe la FA dhidi ya Arsenal, ninaamini wapinzani hao wanajipanga kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

“Ili tuweke historia kubwa ni kuendelea kujikusanyia vikombe, ikiwa pamoja na kikombe hicho cha Kombe la FA, nimewataka wachezaji wangu kwa sasa kufurahia ubingwa wa Ligi Kuu, lakini huku wakijua kwamba, bado tuna safari ya kuelekea katika fainali hizo.

“Lengo ni kutwaa ubingwa huo na tunaamini inawezekana, kwa kuwa ni mchezo pekee ambao tunajiandaa nao, japokuwa kuna michezo mingine ambayo imebaki ya Ligi Kuu,” aliongeza Conte.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles