23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Chave: Siyo rahisi kwa Tanzania kurejesha mabilioni ya Uswisi

1ELIAS MSUYA

Kwa zaidi ya miaka miwili, kumekuwa na taarifa za kufichwa kwa mabilioni ya fedha katika benki za Uswisi na nchi nyinginezo duniani.

Taarifa ya awali ilitoka ilitokana na ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi ikionyesha kuwa kuna zaidi ya Sh300 bilioni za Tanzania zilizofichwa kwenye benki mbali mbali nchini humo.

Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na Mtandao wa Kimataifa wa Habari za Uchunguzi (ICIJ) zimeonyesha kuwepo kwa Watanzania 99 walioficha kiasi cha Sh210 bilioni katika benki ya HSBC ya Geneva

Akizungumza na mwandishi wetu pamoja na mambo mengine, Balozi wa Uswisi nchini Olivier Chave anafafanua.
Swali: Kwa zaidi ya miaka miwili, vyombo vya habari vya Tanzania vimekuwa vikijadili mabilioni ya Uswisi. Habari nyingine mpya imeibuka hivi karibuni kuhusu benki ya HSBC ya Geneva. Nini maoni yako katika hili?
Jibu: Kwanza ile habari ya Mabilioni ya Uswisi iliyovuma miaka miwili iliyopita ilitokana na taarifa ya Benki ya Taifa ya Uswisi (Swiss National Bank (the Swiss central bank). Ripoti hiyo ilieleza kuhusu benki 97 kubwa binafsi za Uswisi bila kuweka wazi kiasi cha fedha za wateja wake kutoka nchi husika.
Mjadala uliokuwa ukiendelea Tanzania ulilenga kuwekwa wazi kwa kiasi cha fedha hizo na na kama fedha hizo zilikuwa zinamilikiwa na kuwekwa huko kihalali.
Habari ya Swissleaks ni tofauti kabisa. Ilitokana na ripoti ya kiasi kikubwa cha fedha zinazowahusu wateja wapatao 106’458 wa benki ya HSBC (Private Bank (Switzerland) kati ya mwaka 2006 na 2007.
Taarifa hizo ziliibwa na HervéFalciani aliyekuwa mhandisi wa komputa wa benki hiyo. Baadaye alijaribu kuziuza kwa serikali za Ulaya akidhani atakuwa anapambana na wakwepa kodi.
Ufaransa walizichukua taarifa hizo na kuzipeleka kwenye gazeti lao maarufu la ‘Le Monde’ na baadaye wakazigawa kwa Mtandao wa Kimataifa wa waandishi wa Habari za Uchunguzi (ICIJ) uliohusisha vyombo vya habari 55 katika nchi 65 duniani vilivyofanya uchunguzi wa kina wa taarifa hizo.
Ripoti ya ICIJ kuhusu “Swissleaks” ilionyesha kuwepo kwa Watanzania 99 wateja wa HSBC na walikuwa wamehifadhi kiasi cha Dola za Marekani 114 milioni. Miongoni mwao 17 walionekana kuwa raia wa Tanzania huku wengine wakihusishwa tu na Tanzania.
Kwa hiyo habari hizi mbili ziko tofauti; ya kwanza ni ile ripoti ya Benki ya Taifa ya Uswisi inayotoka kila mwaka nay a pili ni ripoti ya ICIJ ikihusu taarifa za wateja zilizoibwa katika benki ya HSBC miaka saba iliyopita.
Halafu haikuwa rahisi kwa Hervé Falciani kuziuza taarifa zake alizoibwa kwa Serikali za Ulaya, kwa sababu taarifa zilizoibwa huwa hazikubaliki kwenye vyombo vya sheria na ndiyo Serikali hizo zilihofu kuzinunua kwa kuwa zisingeweza kuwashitaki wakwepa kodi wao.
Hata hivyo, mwaka 2008 ulikuwa ni wa anguko la uchumi duniani hivyo nchi za Ulaya zikaona kuwa ukwepaji wa kodi ndiyo chanzo kikubwa cha mdororo huo. Hatimaye nchi hizo zikamtafuta Falciani na kuzinunua.
Ndipo nchi hizo kila moja kwa wakati wake zikaanza kuwatafuta wakwepaji wakodi wao bila kutumia vyombo vya sheria. Waliowaomba tu kueleza mali walizonazo na kuwatoza kodi na adhabu.
Kw aufupi tu taarifa za Swissleaks zinaonyesha jinsi benki ambayo ni tawi tu la benki ya HSBC ya Uingereza ilivyokuwa ikifanya kazi kwa miaka yote hiyo. Benki hiyo ilikiuka misingi yake ya kazi na ilipokea fedha kutoka kwa wateja wote bila kujali ni kina nani, wakiwemo hata wanasiasa na mafisadi.
Swali: Wakati HSBC inafanya hivyo, Serikali ya Uswisi ilichukua hatua gani?
Jibu: Wakati haya yakitokea, Serikali ya Uswisi ilishaanza kusafisha kituo chacke cha fedha na kuweka sheria na kanuni ngumu. Hata hivyo kanuni hizo zilikuwa zikitumiwa na benki zenyewe kama wajibu wao. HSBC imeonyesha mfano kwamba baadhi ya benki zilikuwa hazifuati kanuni hizo.
Swali: Kwa hiyo sasa Tanzania itazipataje fedha zake hasa kwa hawa Watanzania 99 waliotajwa?
Jibu: Binafsi sidhani kama Serikali ya Tanzania inaweza kutumia taarifa hizi kuzipata hizo fedha. Nirudie tena kusema, taarifa hizi ni za muda mrefu za wateja wa mwaka 2006 hadi 2007, kwanza hata akaunti hizo zinaweza kuwa zimeshafungwa kwa hiyo zimeshapitwa na wakati. Isitoshe, hata HSBC yenyewe imeshajitenga na maelfu ya wateja wake.
Hata hivyo Tanzania inaweza kufanya uchunguzi kama nchi za Ulaya zilivyofanya mwaka 2008 kuwapata wateja hao wa mwaka 2007 kwa kujaribu kuwashawishi kueleza hali zao za kifedha bila kutumia vyombo vya sheria. Lakini udhaifu wake ni kwamba taarifa hizo zimepitwa na wakati.
Njia yoyote watakayotumia katika kutafuta ufumbuzi, nawahakikishia kuwa Serikali ya Uswisi iko tayari kusaidia, ilimradi tu ombi la msaada lifanwe kisheria na kwa kufuata viwango vya kimataifa.

Swali: Uswisi imekuwa na ushirikiano na Tanzania tangu mwaka 1960. Je, ushirikiano huu unagusa maeneo gani hasa?

Jibu: Ni kweli Switzerland imekuwa na ushirikiano na Tanzania tangu mwaka 1960. Mwaka 1981 Uswisi ilifungua ofisi yake rasmi Dar es Salaam. Mpango wa maendeleo ya Uswisi umeisadia Tanzania katika mikakati ya kupunguza umasikini ikishirikiana na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa.

Mkakati wa Ushirikiano wa Uswisi wa mwaka 2011 hadi 2014 unalenga kupeleka misaada katika maeneo mbalimbali hasa kanda ya kati (mikoa inayozunguka Dodoma).

Katika sekta ya afya, Uswisi imesaidia upatikanaji wa afya bora na na matunzo kwa jamii zilizo katika maeneo yasiyofikika kirahisi. Lengo kuu ni kupambana na ugonjwa wa malaria na kufadhili huduma za afya. Maeneo mengine ni kuboresha mfumo wa afya na maendeleo ya miradi ya utafiti ili kuwawezesha wafanya uamuzi kuwa na taarifa sahihi.
Katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa malaria, Shirika la maendeleo la Uswisi (SDC) limesaidia katika mpango wa Taifa kwa kutoa vyandarua vilivyowekwa dawa kwa zaidi ya Watanzania 28 milioni. Kutoka na hali hiyo idadi ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano imepungua kwa asilimia 48 tangu mwaka 2000 hadi 2010 huku ajira 6,000 zikipatikana.

Mwaka 2012 Tanzania ilikuwa nchi ya 152 miongoni mwa mataifa 187 kimaendeleo ya binadamu, hivyo ilikuwa nchi masikini sana duniani. Licha ya kukua kwa uchumi, umasikini bado unaonekana ambapo watu 12 milioni sawa na asilimia 28 walikuwa wakiishi chini ya mstari wa umasikini mwaka huo.

Hata hivyo Tanzania ni kati ya nchi amani na utulivu katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara.

Kwa upande wa utawala bora, Uswisi imekuwa ikisaidia kujenga utamaduni wa kuwajibika na uwezeshaji. Tumekuwa tukisaidia asasi za kiraia na kutetea uhuru wa vyombo vya habari ambao ni muhimu katika kuwaunganisha wananchi na Serikali yao. Mwananchi mwenye taarifa za kutosha atakuwa na nguvu ya kudai haki na kuiwajibisha serikali katika utoaji wa huduma za umma.

Katika eneo hili, Uswisi imekuwa ikisaidia Baraza la Habari Tanzania (MCT) kuboresha vyombo vya habari, katika maadili na kiwango hicho cha wananchi kinaridhishwa.

Katiak kilimo, tumesaidia katika upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya kilimo. Kuboresha ushirikiano wa wakulima wadogo katika masoko ya ndani, siyo tu kwamba huongeza mapato yao bali pia hukuza kilimo kwa ujumla.

SDC imesaidia katika ushirikiano wa kiuchumi wa wakulima wadogo kutoka maeneo ya vijijini na kutwatoa katika umasikini. Wakulima hawa waliokuza kipato chao kwa asilimia 15 wako katika kilimo cha mpunga, alizeti, pamba na ufugaji wa kuku.

Tumesaidia pia kukuza usawa kati ya mwanamke na mwanaume katika miradi yote, ikiwa pamoja na kupinga ubaguzi na kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi.

Tunafadhili pia mradi wa kuchoma mkaa uliopo wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Shirika la Kuhifadhi misitu ya asili Tanzania, Mjumita na Tatedo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles