24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

CHANGAMOTO kunawa mikono, upotoshaji unaoendelea mitandaoni kuhusu corona

 HASSAN DAUDI 

HALI imeendelea kuwa tete ulimwenguni kote kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona. 

Kwa hali ilivyo hapa nchini, hadi kufikia jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alitangaza ongezeko la wagonjwa wa corona kufikia watatu baada ya watu wengine wawili kuthibitishwa mmoja akitokea visiwani Zanzibar na mwingine Dar es Salaam. 

Kati ya wagonjwa watatu waliobainika nchini, wawili ni raia wa kigeni na mmoja Mtanzania aliyekuwa nje ya nchi kwa muda wa siku kadhaa na kurejea nchini akiwa na maambukizi hayo. 

Siku ya Jumanne, Majaliwa alitangaza kufunga shule zote kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini. 

Serikali imethibitisha hayo baada ya wagonjwa hao kufanyiwa vipimo vya maabara katika Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii. 

Wagonjwa wawili waliobainika jana wametengwa katika sehemu maalumu kwa ajili ya taratibu nyingine za kitabibu, pia kufanya ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu nao. 

Kutokana na hali hiyo, Majaliwa alitangaza kufungwa kwa shule zote kuanzia awali hadi kidato cha sita kwa siku 30 zikiwa ni jitihada za kudhibiti maambukizi. 

Kwa kipindi hiki, wizara itafanya marekebisho ya ratiba kwa wale wanaotarajiwa kufanya mitihani Mei 4, mwaka huu, ambapo itasogezwa mbele kadiri ya matokeo yatakavyojitokeza ili nao wapate kusoma kwa kipindi kilekile kilichokubalika na ratiba hiyo. 

Pamoja na hayo, pia imesitisha michezo yote inayokusanya makundi ya watu kama vile Ligi Kuu ya Tanzania, Ligi daraja la pili, ligi daraja la kwanza lakini pia michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA) , michezo ya shule za sekondari (UMISETA) pamoja na michezo ya mashirika ya umma. 

Pia Serikali imezuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwamo matamasha ya muziki na mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwamo ya kisiasa. 

Hadi kufikia jana, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), tayari maambukizi yamefikia 184,975 duniani kote, huku watu waliopoteza maisha wakifikia 7,529 katika nchi 159 zilizokumbwa na ugonjwa huo. 

CHANGAMOTO KUNAWA MIKONO NCHI ZILIZOENDELEA 

Huku mataifa ya Ulaya na yale yaliyostawi duniani yakifunga mipaka yao katika juhudi za kukabiliana na maambukizi hayo, mamilioni ya watu wanashindwa kuzingatia ushauri wa kuosha mikono na kutokaribiana unaosisitizwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). 

Karibu watu bilioni moja wanaishi katika mitaa ya mabanda na inakadiriwa hadi asilimia 30 ya idadi ya watu wanaoishi maeneo ya mjini. 

Makazi hayo yanakumbwa na msongamano wa watu, huku mfumo wa maji taka na usafi kwa jumla ukiwa changamoto inayochangia kusambaa kwa haraka kwa magonjwa. 

Zipo familia zinazoishi chumba kimoja, ambacho hakina maji wala umeme hivyo mtu anayeishi mazingira ya aina hii, hawezi kutembea katika chumba hicho bila ya kugongana. 

Kwa sababu hii, kuna haja ya Serikali kuwa makini na watu walioambukizwa kwa kuwapeleka hospitalini. 

Kuna siku ambazo hakuna maji hivyo, familia ya aina hii hulazimika kulala bila kuoga na hiyo imeshazoeleka. 

Dk. Pierre Mpele, Mwakilishi wa zamani wa WHO, ambaye amefanya kazi katika nchi nyingi za Afrika Magharibi na Kati, anasema familia nyingi za Kiafrika zinaishi katika mazingira ya msongamano. Wakati mwingine hadi watu 12 wanaishi pamoja katika nyumba ndogo. 

“Suala la kujitenga halitawezekana katika maeneo mengi,” anasema. 

Katika miji ya Johannesburg na Chennai pia mwaka jana zilikabiliwa na uhaba wa maji. 

Wakati kulishuhudiwa uhaba wa maji mwaka uliopita, familia nyingi zililazimika kununua na kutumia maji ambayo hayajatiwa dawa yaliyokuwa yakitumiwa kwa shughuli za kilimo kutoka visima vilivyopo umbali wa kilomita 50. 

Kuna vyoo vichache vya umma na maeneo ya kuchota maji hivyo watu hawazingatii ushauri wa afya kwa umma. 

Ikumbukwe kuwa katika usafiri wa umma kama treni, mabasi yaendayo kasi na daladala watu hukohoa karibu na uso wa mwingine tena bila kufunika mdomo. 

Daktari Poppy Lamberton, Mhadhiri anayetoa huduma za afya katika Chuo Kikuu cha Glasgow nchini Uingereza, anasema serikali zinahitaji kuongeza juhudi za kuzuia maaambukizi. 

“Baadhi ya nchi ni masikini, lakini sio masikini kama baadhi ya raia wake. Endapo mlipuko utatokea zinatakiwa kutenga jamii nzima.” 

WHO inasema inafanya kazi ya kuzisaidia nchi kuweza kukabiliana na janga hili, lakini Dk. Mpele anataka suala hili lije na mwongozo utakaofanya kazi kwa nchi zinazoendelea. 

Pia anashauri kuwapo kwa jitihada za kuhusisha viongozi katika jumuia kabla hali haijawa mbaya zaidi barani Afrika. 

‘’Hali ya maambukizi Afrika haiko kwa kasi. Ripoti nyingi za wagonjwa ni wale watu waliosafiri kutoka China au Ulaya. Hatujui kwanini havisambai kwa haraka,’’ anasema. 

WHO inasema usambaaji ni wa chini kwa watu ambao hawana historia ya kusafiri. 

UONGO KUHUSU MAAMBUKIZI 

Hata hivyo, wakati vita dhidi ya virusi hivyo ikiendelea, zimekuwapo taarifa za uongo juu ya virusi hivyo na hivyo kuzidisha hofu kwa wanajamii. 

Kupitia mitandao ya kijamii, umekuwapo upotoshaji juu namna ya kujikinga na kujitibu virusi hivyo, jambo ambalo kwa namna moja au nyingine linaweza kuchangia kasi ya maambukizi. 

MATUMIZI YA MASK 

Si kweli kwamba anayevaa ‘maski’ ndiye anayejizuia kuambukizwa, bali anayefanya hivyo ni mwathirika. Anayevaa ni yule aliyegundulika kuwa navyo ili asieneze kwa wengine kupitia chafya au kukohoa. 

WATOTO HAWAAMBIKIZWI CORONA 

Licha ya awali kuonekana ni vijana na wazee pekee walio hatarini, ni taarifa za upotoshaji kuwa watoto hawawezi kupata maambukizi ya virusi vya corona. Takwimu zinazoonesha watoto ni wachache katika maambukizi, lakini hii haimaanishi kuwa kuwa hawawezi kuathirika na virusi hivyo. 

DAWA ZA KULEVYA NI KINGA 

Wapo watu wanaopotosha kwamba dawa za kulevya aina ya cocaine huua virusi hivyo, dhana iliyokuwa imeshika kasi nchini Ufaransa, kabla ya Serikali kuingilia kati na kupiga marufuku. 

KUKAA NA MWATHIRIKA DAKIKA 10 

Hakuna ukweli wowote juu ya madai kuwa ili uambukizwe virusi ni lazima ukae na mwathirika kwa dakika 10. Hii si kweli, bali utaambukizwa mara tu atakapokugusa au atakapokohoa na kupiga chafya kisha virusi hivyo vikakufikia. 

MIZIGO KUTOKA CHINA NI HATARI 

Kupokea mizigo au barua kutoka China au nchi zingine zenye kiwango kikubwa cha maambukizi si njia ya maambukizi, hii ni kwa mujibu wa WHO. 

Tafiti za awali zimebaini kuwa virusi hivyo havina uwezo wa kuishi kwa muda mrefu katika vitu kama bahasha au maboksi, ingawa vinaweza kuwa hai kwa siku tisa endapo vitatua juu ya kioo, plastiki au chuma. 

“Kuna hatari ndogo ya maambukizi kupitia bidhaa za kuagiza na kwa Marekani hakuna taarifa yoyote ya maambukizi ya virusi vya corona kupitia njia hiyo,” anasema Dk. Amesh A. Adalja, Mtaalamu kutoka Kituo cha Afya cha Johns Hopkins. 

PAKA NA MBWA HUAMBUKIZA CORONA 

Ni uzushi kwamba paka na mbwa wanaweza kumwambukiza binadamu virusi vya corona. Utafiti uliofanywa kwa mbwa mmoja nchini China, ni kwamba alipata maambukizi kutoka kwa mmiliki wake lakini hakuweza kuhamisha kwenda kwa binadamu mwingine. 

“Uzoefu unaonesha kuwa paka na mbwa hawawezi kuambukiza virusi kwa binadamu,” anasema Mtaalamu wa Afya za Wanyama, Vanessa Barrs. 

MAJI NI KINGA 

Si kweli kwamba kunywa maji mengi huzuia maambukizi. Hakuna ushahidi wa kisayansi juu ya hilo. Bali ni kweli kwamba maji ni sehemu muhimu ya mwili na yamekuwa na faida lukuki, ikiwamo kurahisisha mmeng’enyo wa chakula lakini hakuna uhusiano wa namna yanavyoweza kujikinga na virusi vya corona. 

KUZUIA PUMZI 

Imekuwapo dhana kuwa mtu akizuia pumzi kwa sekunde zaidi ya 10 na kisha asikohoe, basi huyo si mwathirika. Hiyo si kweli. 

WENYE KINGA YA MAFUA HAWAAMBUKIZWI CORONA 

Upotoshaji mwingine ni kwamba ukiwa na kinga ya mafua itakuzuia pia kupata maambukizi ya virusi vya corona. Ni kweli dalili za mafua na mwathirika wa virusi vya corona zinashabihiana kwa kuwa zote mgonjwa atakuwa na homa na kikohozi. “Chanjo ya mafua haitakulinda dhidi ya virusi vya corona. Ni virusi tofauti,” anasema Dk. Simone Wildes. 

VITAMIN C NI KINGA 

Si kweli kwamba Vitamin ‘C’ ni kinga dhidi ya virusi vya corona. Licha ya kueleweka kuwa ni muhimu kwa afya ya binadamu, hakuna ushahidi wa kitaalamu kuwa vinafaa kuaminiwa kuwa ni kiboko ya virusi hivyo. 

Wakati huo huo, hakuna uthibitisho wa kitaalamu juu ya madai kuwa virusi hivyo vilitengenezwa na binadamu, licha ya kwamba ni uzushi ulioenea huko mitandaoni. 

Zinaweza kuwa taarifa za virusi kutengenezwa na Wachina au Wamarekani lakini ukweli ni kwamba hakuna kilichothibitishwa juu ya madai hayo, hivyo hadi sasa inabaki kuwa ni uzushi tu. 

TUNAVYODANYANA KUHUSU TIBA 

Ushauri wa kiafya ambao umeenea kwa kasi mtandaoni usio na uhusiano wowote na taarifa za wanasayansi. 

VITUNGUU SAUMU 

Watu wengi kwenye mitandao ya kijamii wanashauri wenzao kula vitunguu swaumu ili kuzuia kupata maambukizi ya corona. 

WHO linasema vyakula kwa afya mara nyingine huwa vina vimelea ambavyo si salama kwa binadamu, hakuna uthibitisho unaosema kuwa mtu akila kitunguu swaumu basi anaweza kujilinda na virusi vipya vya corona. 

Katika kesi nyingi, aina hii ya tiba huwa haina madhara makubwa kwa afya kama watu wanazingatia utaratibu wa kiafya au kufuata ushauri wa madaktari. 

Lakini wanapaswa kufahamu uwezo wa kile wanachoambiwa. 

Huko Kusini mwa China, taarifa zimeripoti kuwa kuna mwanamke ambaye alipaswa kupata huduma za kiafya hospitalini lakini alitumia vitunguu swaumu vibichi kilo moja na nusu. 

Tunafahamu kwa ujumla kuwa kula matunda na mboga za majani pamoja na kunywa maji kunaweza kukufanya mtu uwe na afya njema. 

Ingawa hakuna ushahidi unaosema kuwa chakula fulani ni tiba na kinaweza kupambana na virusi vya aina fulani. 

MADINI 

Mmiliki wa YouTube, Jordan Sather, ambaye ana maelfu ya wafuasi kutoka duniani kote amekuwa akidai kuwa kuna madini ya miujiza yanayoweza kuponya virusi vya corona. 

Hii inajumuisha watengeneza dawa aina ya ‘chlorine dioxide’ ambayo iliweza kutibu saratani. 

Mwaka jana, Mamlaka ya Chakula na Dawa Marekani, ilitoa angalizo kuhusu hatari za kiafya. 

Mamlaka za afya katika mataifa mengine pia wametoa angalizo kuhusu jambo hilo. 

Mamlaka hiyo imedai kuwa haijapata utafiti wowote unaonyesha kuwa kuna vitu vinavyoweza kutibu ugonjwa wowote. 

Imetoa angalizo kuwa kunywa dawa hizo ambazo hazijathibitiwa kunaweza kusababisha kichefuchefu, kutapika, kuharisha na dalili za kuishiwa maji. 

DAWA YA KUOSHEA MIKONO ILIYOTENGENEZWA MAJUMBANI 

Kumekuwapo ripoti nyingi za kudai kuwa dawa za kuoshea mikono zimeisha, wakati kuosha mikono ndio jambo muhimu watu wameambiwa kuzingatia ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona. 

Ripoti za upungufu wa dawa hizo zilianza kujitokeza nchini Italia, hivyo watu walianza kufundisha namna ya kutengeneza dawa hizo nyumbani kupitia mtandao wa kijamii. 

Lakini mahitaji ya kutengeneza dawa hizo, wanasayansi wamedai kuwa si salama kwa matumizi ya kwenye ngozi. 

Kilevi kutengeneza dawa ya kuoshea mikono nyumbani si jambo sahihi. 

Profesa Sally Bloomfield, kutoka Chuo cha Afya, anasema kuwa haamini kuwa pombe inawezi kutengeneza dawa za kuoshea mikono. 

KINYWAJI CHA MADINI YA FEDHA 

Wazo la matumizi ya kinywaji cha madini ya fedha ambacho kilianzishwa na mchungaji wa Marekani Jim Bakker kilikatazwa. 

Alidai kinywaji cha madini hayo inaweza kuwa suluhisho la maambukizi ya virusi vya corona ndani ya saa 12, ingawa amekubali kuwa hajawahi kutumia kwa mtu mwenye virusi vya corona. 

Wazo hilo lilienea kwenye mtandao wa facebook kuwa kinywaji hicho kinaweza kutibu virusi vya corona. 

KUNYWA MAJI KILA BAADA YA DAKIKA 15 

Picha moja ilisambaa katika mtandao wa Facebook ikimnukuu daktari wa Japan kuwa mtu akinywa maji kila baada ya dakika 15, anakuwa anasafisha mwili hivyo anajikinga na maambukizi ya virusi. 

Na maelezo mengine ya aina hiyo yalishirikishwa kwenye mtandao zaidi ya mara 250,000. 

Professa Trudie Lang kutoka Chuo Kikuu cha Oxford, anasema kuwa hakuna uhusiano wowote wa kibaiolojia unahusisha wazo hilo kuwa kunywa maji mengi kunaweza kuua vijijidudu vya corona. 

Maambukizi ya corona yakiingia kwenye mwili yanaweza kuambukizwa kwa mtu kuhema. Baaadhi ya maambukizi yanaweza kupita kwenye kinywa hivyo hata ukinywa maji huwezi kuzuia. 

JOTO KALI NA KUJIZUIA KULA BARAFU 

Watu wamekuja na ushauri wa kila aina, wengine wakidai kuwa joto linaua virusi hivyo na kuwashauri watu wanywe maji ya moto na kuoga maji ya moto. 

Ushauri ambao ulichukuliwa na watu wengi katika mitandao ya kijamii katika nchi mbalimbali na kudaiwa kuwa Unicef wamethibitisha wakati ni uongo, walidai kuwa kunywa maji ya moto na kukaa kwenye jua na kujizuia kula barafu. 

Unicef ilitoa angalizo kwa watu kuwa makini na taarifa ambazo si sahihi, hakuna ukweli kuwa ‘ice cream’ (barafu) na vyakula vya baridi vinaweza kuzuia mtu kupata magonjwa. 

Tunafahamu kuwa virusi vya mafua huwa havikai kwenye mwili wakati wa jua lakini hatufahamu kama virusi vipya vinaweza kudhurika na jua. 

Kwa mujibu wa Profesa Bloomfield, kujaribu kukaa kwenye jua wakati virusi viko tayari kwenye mwili wako, hakuna namna ambayo jua linaweza kukabiliana na virusi hivyo. 

Kuoga maji ya moto au kunywa maji ya moto hakutaweza kuua vijijidudu wakati ukiwa mgonjwa tayari. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles