26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema wamjia juu Dk. Bashiru

Leonard Mang’oha -Dar es Salaam

BARAZA la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bazecha) limemjibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, kuhusu kauli yale kuwa wanaotaka tume huru ya uchaguzi wanahitaji huruma na msaada wa tume kwa sababu hawana wanachama wa kuwapigia kura.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Bazecha, Hashim Juma Issa, alisema kuwa hivi karibuni Dk. Bashiru alifanya kejeli kuhusu Tume Huru ya Uchaguzi huku akisema kuwa CCM haihitaji tume huru kwa sababu ina wapigakura wengi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotekelezwa na Serikali.

“Anasema wao CCM wana wanachama kwa sababu wameinua kiwango cha elimu, wameweka elimu bure, wameinua kiwango cha afya, wamejenga barabara, wameagiza ndege na mifano mingine mingi. Kwa hiyo wana wanachama wengi wa kuwachagua, akauliza ninyi mnaodai tume huru mna wanachama kutoka wapi.

“Ningependa nimjibu Dk. Bashiru kwa sababu ameonyesha dharau kubwa kwa wale wote wanaodai tume huru katika nchi hii, ni bora tumjibu tusimwache aende hivihivi.

“Sisi kama chama huu mwaka wa pili tunafanya kitu kinaitwa Chadema Msingi, hiyo ni operesheni tumeifanya karibu miaka miwili ikiongozwa na mwenyekiti wetu wa chama (Freeman Mbowe), tumeimarisha chama chetu Tanzania nzima, mikoa yote tumefika mpaka vijijini. Tuna muundo wa chama uliokamilika kwa asilimia karibu 90, kwa hivyo chama chetu kiko imara, tuna wanachama wengi nchi hii.

“Lakini kwa kumjibu tena Dk. Bashiru, akiuliza wanachama wetu tunawatoa wapi sisi tutamwambia wakulima wote wa Tanzania ni wanachama wetu kwa sababu madhila waliyoyapata wakulima wa korosho hawana imani tena na CCM, wote wale wanaitegemea Chadema kuwa ndiyo mwokozi wao, wakulima wa pamba wote kwa bei waliyopangiwa wote hawana imani na CCM,” alisema Issa.

Alisema kuwa mfano mzuri kuwa CCM haina wapigakura ni Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka jana ambapo alidai kuwa wapigakura waliojitokeza hawakufika 10,000 licha ya kutarajiwa kuwa zaidi ya watu milioni 30 wangeshiriki uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, Issa alimwomba Rais Dk. John Magufuli kuitisha maridhiano ya kitaifa na vyama vya siasa vya upinzani kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kwamba kuomba kufanyika kwa maridhiano hayo si kwamba wanamnyenyekea au kumwogopa ila kwa sababu ni suala muhimu.

Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuweka hali nzuri ya kisiasa nchini kama ilivyowahi kufanyika Zanzibar wakati wa utawala wa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume alipoamua kmwita mezani aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, baada ya kuona mambo hayaendi sawa.

Naye Katibu wa Bazecha, Rodrick Lutembeka, alisema kuwa chama hicho hakitasusia Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa sababu chama chochote cha siasa kipo kwa lengo la kushika dola.

“Kila chama kipo kwa ajili ya kushika dola, kwa hiyo suala la kususia uchaguzi hilo halipo tutashiriki uchaguzi kama kawaida,” alisema Lutembeka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles