23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema waja na hoja nyingine, NEC wajibu

Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Tume ya Uchaguzi (NEC) kueleza kuwa haitavitumia vifungu vya sheria vilivyokuwa vikiruhusu wakurugenzi wa halmashauri na wilaya, miji na majiji kusimamia uchaguzi, Chadema kimeitaka tume hiyo kuvifuta kwenye kanuni ya uchaguzi.

Kutokana na hilo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage jana aliliambia MTANZANIA kuwa vifungu vinavyohusu uboreshaji wa daftari la wapigakura havikubatilishwa, hivyo wataendelea kuvitumia.

Alisema watafuata sheria kama zilivyo, lakini vile vifungu vya 7(1) na 7(3) ambavyo vilitenguliwa na mahakama hawatavitumia.

“Tunafuata sheria kama zilivyo, lakini vile vifungu vilivyotenguliwa na mahakama hatutavitumia, lakini vinavyohusu uboreshaji wa daftari la wapigakura havijabatilishwa.

“Hivyo tutaendelea kuvitumia kwa sababu suala la kutunga sheria ni la Bunge,” alisema Jaji Kaijage.

CHADEMA

Akitoa msimamo wa Chadema jana mbele ya waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje, John Mrema, alisema pamoja na kwamba NEC imeeleza kuwa haitawatumia wakurugenzi, lakini haijaweka wazi itatumia utaratibu gani.

“Jaji Kaijage hajatuambia wanakwenda kutumia utaratibu gani, lakini kwenye kanuni imewataja hawa Ma-DED kama waandikishaji na wanaosimamia uchaguzi na hata vifaa vya BVR huwa vinapitia kwao,” alisema Mrema.

Mei 10 mwaka huu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa uamuzi wa kuvifuta vifungu vya sheria ya uchaguzi namba 7(1) na 7(3).

Uamuzi huo uliotolewa na Jaji Dk. Atuganile Ngwala, ulitokana na kesi iliyofunguliwa na mwanachama wa Chadema, Bob Wangwe, aliyekuwa akitetewa na Wakili Fatma Karume.

Pia mahakama hiyo ilibatilisha kifungu cha 7(3) kinachoipa NEC mamlaka ya kuteua mtu yeyote miongoni mwa watumishi wa umma kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Mahakama ilisema vifungu hivyo ni kinyume cha Katiba ya nchi ikibainisha kuwa wakurugenzi hao ambao si waajiriwa wa NEC, huteuliwa na rais aliyeko madarakani, ambaye hutokana na chama tawala na kwamba wengine ni wanachama wa chama cha mamlaka inayowateua jambo ambalo huathiri utendaji wao katika kutenda haki.

Ilisema kifungu cha 7(1) kinasema kila Mkurugenzi wa Jiji, Manispaa na Halmashauri anaweza kusimamia uchaguzi wakati viongozi hao ni wateule wa Rais na si waajiriwa wa NEC wakati Katiba inasema NEC inapaswa kuwa huru na haki.

Jaji Ngwala alisema kutokana na hali hiyo, kifungu hicho kinakinzana na sheria mama ambayo inasimamia nchi. Pia kifungu cha 7(3) kinasema kuwa NEC inaweza kuteua mtu yeyote kuwa msimamizi wa uchaguzi bila ya kuainisha ni mtu wa aina gani.

Alisema lakini Katiba inasema kuwa mtu yeyote anayekuwa msimamizi wa uchaguzi hapaswi kuwa mwanachama wa chama chochote cha siasa.

VIFUNGU NA KATIBA

Akizungumza jana, Mrema aliitaka NEC iondoe vifungu vyote vya kanuni ambavyo ni kinyume na Katiba ya nchi vinginevyo watakwenda mahakamani.

“Pia tume iache mpango wake wa kuajiri makada wa vyama vya siasa kuwa maofisa waandikishaji bali iwaajiri watu ‘neutral’,” alisema.

Akizungumzia kuhusu kauli ya Jaji Kaijage, kwamba vyama vya siasa vimeshirikishwa katika kila hatua ya uandikishaji wa daftari la wapigakura, Mrema alisema hawakuwahi kushirikishwa katika hatua yoyote.

“Hata hiyo kanuni tumekuja kuiona tangu Desemba mwaka jana katika gazeti la Serikali na sisi tumekabidhiwa mwezi huu, lakini hatujashiriki katika kuandaa kanuni na tumekaa kikao kimoja tu na tume,” alisema.

Katika mkutano wake wa juzi na wahariri, Jaji Kaijage alisema vyama vya siasa kama wadau wao muhimu wameshirikishwa katika hatua zote.

Aidha akizungumza na gazeti hili jana, Jaji Kaijage alisisitiza kuwa katika suala nzima la ushirikishwaji, waliwashirikisha vyama vyote na Chadema kilituma mwakilishi na kutoa maoni yao.

“Hao (Chadema) si wamesema, na sisi pia tumesema. Sheria inaipa wajibu tume kuandaa kanuni na haijaweka masharti yoyote. Sasa kama wanasema hatukuwashirikisha, sisi tuna kumbukumbu ya waliohudhuria na Chadema kilituma mwakilishi wake na wakaleta maoni yao,” alisema Jaji Kaijage.

Hata hivyo, Mrema alisema wanaitaka NEC iondoe vituo vyote ambavyo viko katika kambi ya Jeshi la Polisi, kwa kuwa wananchi wamekuwa hawafiki kwa sababu ya hofu.

Vilevile alisema NEC iweke hadharani majina ya asasi za kiraia 24 zilizoruhusiwa kutoa elimu kwa wapigakura.

“Vyama vya siasa tumenyimwa haki ya kutoa elimu kwa wapigakura, yaani haturuhisiwi kuelimisha na kuhamasisha. NEC haitaki elimu itolewe, leo unapowazuia vyama vya siasa wasitoe elimu watawapataje wapigakura wao?

“Sasa hata hizo asasi 24 zilizoruhusiwa ni zile ndogo ndogo ambazo zimesajiliwa siku za karibuni, lakini zile kubwa hazijapewa kibali cha kutoa elimu ya wapigakura,” alisema Mrema.

LHRC WATAKA POLISI WASIMAMIE

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa pendekezo la walimu ama askari  kusimamia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Akizungumza  jana Dodoma, katika mkutano wa kujadili mkakati wa Katiba Mpya ulipotoka, ulipo na uendako, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Anna Henga, alisema wana furaha kubwa kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuwaondoa wakurugenzi kusimamia uchaguzi.

“Wasimamizi wengi wana ‘interest’ na chama na kwenye mikutano unakuta wamevaa kabisa nguo za chama kimoja,  hii inabidi ifanyike kwa watu ambao hawana upande wowote.

“Tunashukuru uamuzi wa mahakama kutotumia wakurugenzi, iteue watu ambao hawana chama chochote, wanaweza wakawatumia walimu au askari, lakini wasiwe na upande wowote.

“Sheria inaruhusu atumiwe mtu yeyote, tunafurahi na hili tunaliunga mkono kwa nguvu zote, tunataka haki ionekane ikitendeka,” alisema Henga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles