33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema kuwatimua waliosaliti Ukawa

Dk. Wilbrod Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa

NA SHABANI MATUTU

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amesema kuwa kazi ya kuwaadhibu wajumbe wa Bunge la Katiba waliokaidi makubaliano ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa kuingia katika Bunge Maalumu la Katiba wataadhibiwa na vikao maalumu vya chama.

Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na wanahabari.

Alisema yeyote aliyekiuka maazimio ya Ukawa na kuingia kwenye vikao vya Bunge Maalumu kwa njaa zake atahukumiwa kwa vikao.

Mbowe alisema iwapo kuna aliyeingia bungeni kwa nia ya kufuata posho na kuweka pembeni maslahi ya Katiba mpya, atakuwa hafai kuwa kiongozi ndani ya Chadema.

“Kama kuna kiongozi anayeshindwa kufahamu umuhimu wa Katiba ambayo ni maoni ya wananchi, inayotetewa na Ukawa, hatufai na anastahili kushughulikiwa na vikao husika vya chama,” alisema Mbowe.

Akizungumzia kile linachodaiwa ni usaliti uliofanywa na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (Chadema), alisema alishangazwa na kiongozi huyo kutumia maneno ya uongo kujitetea kwa kusema kuwa alikwenda Dodoma kufuata fedha za kutibia mguu wake.

“Viongozi hao ni waongo, wamekwenda Dodoma kwa njaa zao, kwani Bunge limeacha siku nyingi utaratibu wa kutoa fedha kwa wabunge kwa ajili ya kupatiwa matibabu, na badala yake wanatumia kadi ya matibabu ya Jubilee Insurance,” alisema Mbowe.

Alisema kwamba hadi sasa mbunge wa chama hicho aliyejiweka wazi kushiriki kwenye mchakato huo alikuwa wa Mpanda mjini, Said Arfi, lakini hao wengine kama Mbunge wa Viti Maalumu, Leticia Nyerere na Shibuda wataunganishwa kuhojiwa katika vikao vya chama.

Taarifa za uhakika ilizozipata MTANZANIA kutoka ndani ya Chadema, zinasema kuwa wabunge hao ambao wanaonekana kuwa wasaliti kwa kuingia katika Bunge la Katiba watafukuzwa ndani ya chama hicho kwa kuvuliwa uanachama katika mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Septemba.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, alipinga taarifa za kuwapo mpasuko ndani ya Ukawa.

Alisema kwamba wajumbe ambao hawajaingia ndani ya Bunge hilo ni asilimia 95, hivyo haoni kama hoja ya mpasuko ina mashiko.

Profesa Lipumba aliwashangaa wabunge hao aliowaita wasaliti kuhudhuria katika Bunge hilo ambalo amesema linaongozwa na mwenyekiti ambaye ni mbadhirifu, Samuel Sitta, ambaye wakati akiwa Spika alijijengea ofisi maalumu ambayo tangu ijengwe, Spika Anna Makinda hajaitumia.

Akizungumzia kuhusu kikao cha siri walichofanya na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kunusuru mchakato wa Katiba mpya, Mbowe alikiri kuwepo kwa kikao hicho ambacho alisema kiliandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

Akizungumzia sababu za kukifanya siri, Mbowe alisema: “Suala hilo tulikubaliana na mwakilishi wa CCM, Abdulrahman Kinana ili iwe rahisi kupatikana muafaka katika jambo hilo nyeti, lakini tulishangaa CCM wakatugeuka na kutoa siri hiyo.”

Miongoni mwa mambo waliyoafikiana ni kusitisha Bunge Maalumu la Katiba, kubadili sheria ili ipatikane Tume Huru ya Uchaguzi, kuruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi na kura za urais kuhojiwa mahakamani.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles