27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Chadema Arusha wacharuka Nassari kung’olewa ubunge

ELIYA MBONEA-ARUSHA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Arusha, kimemtaka Mbunge Joshua Nassari, aliyevuliwa ubunge na Spika wa Bunge, Job Ndugai, kukusanya vielelezo vyote ili shauri hilo lipelekwe kwenye mikono ya sheria.

Agizo hilo lilitolewa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha ambaye pia ndiye Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa.

Akizungumza kwa njia ya simu juu ya sakata hilo la kuvuliwa ubunge Nassari, Golugwa, alisema watapeleka vielelezo hivyo ili mikono ya sheria itafsiri uamuzi uliofanywa na Spika Ndugai.

 “Chama na Nassari tupo naye imara kuhakikisha tunachukua hatua za haki. Ndio maana tumemwambia akusanye vielelezo vyote vya taarifa alizoandika kwetu na kwa Spika,” alisema Golugwa na kuongeza:

“Sisi hatuoni utoro hapo wa kutohudhuria vikao vya Bunge kama taarifa inavyojieleza, kwani alikuwa anatoa taarifa za kuhudhuria masomo nje ya nchi pamoja na matibabu ya mke wake.

“Kwenye mikono ya sheria tunaamini hakuna wanasheria wala majaji watakaovumilia jambo hili.

“Lakini alikuwa akihudhuria vikao vya Kamati za Bunge, uthibitisho upo posho alizokuwa analipwa kwenye vikao vya Kamati ushahidi upo, pengine kesho Nassari atazungumza na wanahabari,” alisema.

Golugwa aliendelea kufafanua kwamba, kati ya wabunge vijana waliofanya vizuri kwenye majimbo yao ni pamoja na Nassari kwani amekuwa na kumbukumbu nzito kwa masuala ya kuhudumia jamii.

“Nassari si mtafuta sifa, ni kijana amekuwa karibu na wananchi, anajituma kutafuta wadau wa maendeleo watakaoleta miradi ya macho, maji, madarasa kwenye eneo lake.

 “Hapa hatutetei ubunge tu, tunaangalia kwa upana mzima kwamba unawaondolea wananchi mwakilishi wao kwa utaratibu gani, ili tu uchaguzi uitishwe tena kwa mamilioni ya fedha,” alisema Golugwa.

Nassari alivuliwa ubunge juzi kutokana na kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge mfululizo, huku mwenyewe akisema amepokea taarifa hiyo akiwa kwenye kazi za kibunge mkoani Kilimanjaro na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Kuvuliwa ubunge wa Nassari kunafanya Chadema kupoteza wabunge nane tangu Uchaguzi Mkuu wa 2015, ambapo kati yao saba walijiuzulu uanachama wa chama hicho na baadaye kuteuliwa tena kuwania nafasi zao kupitia CCM.

Juzi Spika wa Bunge, Ndugai, alimwandikia barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage, kumtaarifu kuwa Jimbo la Arumeru Mashariki lipo wazi.

Taarifa hiyo ilieleza sababu za Nassari kuvuliwa ubunge kuwa ni kutohudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo.

Taarifa hiyo ilitaja mikutano hiyo kuwa ni mkutano wa 12 wa Septemba 4 hadi 14, 2018), mkutano wa 13 wa Novemba 6 hadi 16, 2018 na ule wa 14 wa Januari 29 hadi Februari 9, mwaka huu.

Taarifa hiyo ilisema: “Uamuzi huo wa Spika umezingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 71(1) (c). Ibara hiyo inaeleza kuwa ‘Mbunge atakoma kuwa mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge ikiwa atakosa kuhudhuria vikao vya mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ya ruhusa ya Spika.

“Ibara hiyo pia imefafanuliwa katika kanuni ya 146 (1) na (2) ya kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari 2016, kuwa ‘kuhudhuria vikao vya Bunge na kamati zake ni wajibu wa kwanza wa mbunge, mbunge yeyote atakayeshindwa kuhudhuria mikutano ya Bunge mitatu mfululizo bila ruhusa ya Spika iliyotolewa kwa maandishi, atapoteza ubunge wake na Spika ataitaarifu Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”

Taarifa hiyo ilisema: “Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaweza kuendelea na mchakato wa kumpata Mbunge wa kujaza nafasi hiyo iliyo wazi ya Jimbo la Arumeru Mashariki.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles