Imechapishwa: Thu, Oct 5th, 2017

CCM YAWAONYA WATAKAOSHINDA KWA RUSHWA

Na GUSTAPHU HAULE-SINGIDA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, kimetangaza kuwafutia matokeo viongozi wa   ngazi ya wilaya na mkoa, wakiwamo wenyeviti ambao watabainika kushinda nafasi zao kwa kigezo cha  kutumia rushwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Singida, Jimson Mhagama, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na MTANZANIA kuhusu mwenendo wa uchaguzi unaotarajia kufanyika leo.

Alisema chama hicho kimejipanga kupata viongozi waadilifu wenye uwezo wa kukitumikia ili kisonge mbele lakini hata hivyo, vipo vigezo vinavyoangaliwa kwa wagombea hao likiwemo suala la vitendo vya rushwa.

Alisema katika uchaguzi huo, hakutakuwa na huruma kwa mgombea yeyote ambaye anabainika kujihusisha na vitendo vya rushwa na  kwamba akikamatwa anaondolewa katika orodha ya wagombea pamoja na kufukuzwa uanachama.

Alisema hata kama mgombea akishinda nafasi yoyote na akabainika ushindi wake ulitokana na kutoa rushwa kwa wajumbe matokeo hayo yatafutwa na uchaguzi utarudiwa upya huku jina lake likiondolewa.

“Tumepewa maagizo mazito na chama kupitia Mwenyekiti wetu, Dk. John Magufuli, kuhakikisha tunadhibiti masuala ya rushwa kwa wagombea kwa kuchukua hatua kali, hivyo lazima tutekeleze maagizo hayo kwa vitendo,” alisema Mhagama.

Alisema chama hakihitaji viongozi wanaotafuta uongozi kwa kutoa rushwa na kwamba kiongozi wa namna hiyo hafai katika chama kwa kuwa hajiamini na hana uwezo wa kukisaidia chama badala yake anataka kukitumia chama kwa masilahi yake.

Mhagama amewaasa wagombea walioteuliwa kuachana na vitendo hivyo kwa kuwa vinaweza kuwapotezea sifa ya kuwa viongozi wazuri ndani ya chama na  kwamba kiongozi mzuri lazima awe mwadilifu na mwenye kujiamini.

Displaying 1 Amechangia
Toa Maoni Yako
  1. mtanzania says:

    Kudhibiti rushwa CCM si rahisi. Labda kutoa rushwa kwa namna nyingine. Kwa miaka nenda rudi Rushwa ndio iliyojenga chama hiki. Kila kiongozi alitoa au kupokea rushwa. Na hakuna adhabu kali iliyotolewa. Kuwafavour watu kwa kuwapa cheo kwa ajili ya kutimiza matakwa ya mtu binafsi pia ni rushwa. Sababu anayeteuliwa na kuchaguliwa hayupo huru. Mpaka watu wawe huru kifikra na kiutendaji, na mpaka watu na viongozi wateuliwe na kuchaguliwa sababu ya uwezo na elimu zao ndipo rushwa itakomeshwa. Bado hatujafikia hapo. Bado tunapeana vyeo sisisi kwa sisi bila kujali elimu wala uwezo wa mtu ingawa sheria zipo wazi. zinapinduliwa . Mpaka tuwe na demokrasia, sheria itawale na kila mtu atendewe haki. Bado hatupo huko. Mtu mmoja asijiweke juu ya mwingine bado hatupo huko. Maskini athaminike sawa na na Tajiri bado hatupo huko. Tulikuwepo, tumepoteza. Ni maneno na si vitendo. Ingekuwa wote tunatenda tunayomumg’unya, Tungeijenga nchi yetu kwa misingi nchi hii ilivyozaliwa chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere. Tunalitumia jina lake vibaya.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

CCM YAWAONYA WATAKAOSHINDA KWA RUSHWA