30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM WAPIGA KAMBI KWA NYALANDU

Na WAANDISHI WETU-SINGIDA/DAR

CHAMA Cha Mapinduzi  (CCM), Mkoa wa Singida, kimepiga kambi katika Jimbo la Singida Kaskazini, ambalo lilikuwa linaongozwa na Lazaro Nyalandu.

Nyalandu alitangaza kujiuzulu uanachama wa CCM, hivyo kupoteza ubunge wake Oktoba 30, mwaka huu, kwa kile alichodai chama hicho kimepoteza mwelekeo.

Jana viongozi wa CCM Mkoa wa Singida wakiongozwa na Mwenyekiti Martha Mlata, walilazimika kuitisha Mkutano Mkuu Maalumu wa jimbo ili kueleza kilichojiri baada ya kujiuzulu kwa Nyalandu.

Viongozi wengine walioambatana na Mlata, ni Mkuu wa Wilaya ya Singida, Elias Tarimo, Katibu wa CCM wa Mkoa, Jamsom Mhagama na Mbunge wa Viti Maalumu, Aysha-Rose Matembe.

Akizungumza katika mkutano huo, Mlata alianza kwa kumshambulia Nyalandu kutokana na uamuzi wake wa kujiuzulu na kusema kiongozi huyo si mwaminifu kwa chama na wapigakura wa jimbo hilo.

Katika mkutano huo uliofanyika Kijiji cha Ilongero, uliotanguliwa na Mkutano wa Halmashauri Kuu ya jimbo, wana CCM wengi waliokusanyika walionekana wamepigwa butwaa kutokana na mbunge wao kujiuzulu na kukihama chama chao.

Mlata alisema Nyalandu alianza kuwa shida tangu alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, aliposhindwa kufanya kazi za ubunge jimboni kwake.

“Kwahiyo akawa mzigo jimboni kutokana na kutofika na akifika, anasimama jukwaani dakika mbili halafu anashuka huku kukiwa hakuna cha maana alichokiongea. Na hata alipokuwa jimboni, hakuweza kuwatetea wananchi wake na hatimaye akawa bubu kabisa,” alisema.

Mlata alidai kuwa katika kipindi chote cha ubunge, Nyalandu hakuwahi kushinda kwa kupigiwa kura na wananchi zaidi ya kuhonga wapigakura na shughuli zote za ubunge zilikuwa zikifanywa na wasaidizi wake watatu na yeye anafika jimboni ikiwa zimebakia siku saba za uchaguzi.

Mwenyekiti huyo wa CCM alidai kuwa Nyalandu aligeuza jimbo hilo kuwa kitega uchumi chake na kwamba katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita aliwaaibisha wafadhili wake raia wa kizungu.

“Wafadhili zaidi ya 20 walifika katika jimbo hili kuangalia wanafunzi ambao alikuwa akidai anawasomesha na kufika hapo hawakuona mwanafunzi hata mmoja,” alidai.

Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu, Matembe, alisema katika uchaguzi mdogo unaokuja ni lazima wana CCM na wananchi kwa ujumla wawe makini kwa kuchagua mtu makini na mwenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Singida ambaye pia alikuwa ni mshauri wake wa karibu tangu anaanza kugombea mwaka 2000, Elia Diga, alisema kuwa hakuwa akifanya kazi ya kumwombea kura mbunge huyo pamoja na kusimamia majukumu yake.

Katika mkutano huo, CCM ilimsimamisha pia aliyekuwa Meneja Kampeni wa Nyalandu, Khadija Kisuda, aliyesema kwamba mbunge huyo alikuwa na kazi ya kuwalaghai wananchi na si kufanya kazi waliyomtuma.

“Nyalandu siku tatu kabla kutangaza kuachana na CCM, alikuwa jimboni kwenye ziara na alikuja na kundi la vijana ambao aliwaacha hotelini, mara baada ya kumaliza hakurudi tena kwa wale vijana, ghafla kesho yake ndio akatangaza kujiondoa CCM.

“Hata hivyo, alipofika jimboni alifanya ziara ya kutembelea jimbo, shule na miradi mbalimbali ya jimboni humo, lakini hakuwa mtu wa furaha kwa kuwa alionekana kuwa na wasiwasi muda wote tofauti na ambavyo tumemzoea akiwa anafanya ziara zake.

“Na akiwa katika mkutano wake wa hadhara, alitangaza kufanya mkutano mwingine mkubwa hapo baadaye kwa ajili ya kufanya tathmini, lakini ndio hakutokeza tena na wale vijana aliokuwa amekuja nao aliwaacha palepale hotelini,’’ alisema.

 

HALI YA WANACHAMA

Wanachama wengi walionekana kupatwa na mshtuko kutokana na kueleza kuwa tukio hilo ni la kushtukiza kwa kuwa walizunguka naye katika kampeni ya kukagua jimbo.

Mmoja wa wanachama hao alisema kuwa baada ya kukagua jimbo, Nyalandu alihudhuria mkutano wa dini uliokuwa ukiongozwa na Mchungaji Engon.

“Hatuwezi kuamini kilichotokea kwa kuwa alifanya ziara yake kama kawaida na baada ya hapo akahudhuria mkutano wa Mchungaji Engon, lakini pia si yule Nyalandu ambaye tunamfamu siku zote, alikuwa ni kama mtu ambaye alipatwa na kitu kutokana na kuwa na hali ya wasiwasi mkubwa,’’ alisema.

 

NYALANDU ATOA BARUA

Siku moja baada ya Ofisi ya Bunge kutoa taarifa kwa umma, kwamba Spika wa Bunge, Job Ndugai hajapokea barua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, mwanasiasa huyo ameweka hadharani barua yake aliyomwandikia kiongozi huyo wa Bunge.

Nyalandu ambaye alijivua uanachama wa CCM mapema wiki hii, aliweka hadharani barua hiyo jana, ambayo alimwandikia Spika siku aliyotangaza kujiuzulu Oktoba 30, mwaka huu.

Katika barua yake hiyo kwa Spika, Nyalandu alisema: “Itakumbukwa kwamba nilichaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia bungeni nikiwa Mbunge wa Singida Kaskazini kwa tiketi ya CCM tangu mwaka 2000 na kuchaguliwa mfululizo kuwakilisha wananchi wa jimbo hilo, kazi ambayo nimeifanya kwa mapenzi makubwa, dhamira thabiti na moyo wa ukunjufu.

“Kwa barua hii, napenda kukujulisha kuwa kama nilivyotangaza muda mfupi uliopita kupitia mkutano wangu na wanahabari, nimeamua kujiuzulu nafasi yangu ya ubunge wa Singida Kaskazini kupitia tiketi ya CCM kuanzia leo Oktoba 30, 2017.

“Nachukua nafasi hii kukushukuru wewe pamoja na wabunge wenzangu wote wa CCM kwa muda wote ambao tumefanya kazi kwa pamoja kupitia kamati ya wabunge wote wa CCM.

“Aidha nawashukuru maspika waliotangulia ambao nilipata fursa ya kuwa chini ya uongozi wao bungeni, kuanzia na Pius Msekwa, Samuel Sitta (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) na Anne Makinda,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles