31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

CCM WALIA RAFU KWENYE KAMPENI


NA AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM

Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa wabunge katika majimbo ya Ukonga, Monduli na katika kata 23, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekishutumu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kukiuka maadili ya uchaguzi kwa kutumia maneno makali majukwaani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi  wa CCM, Humphrey Polepole, alisema chama hicho kimefanya kampeni zake kwa ugumu kwakuwa Chadema wamekuwa wakitumia matusi na maneno yanayoondoa utu wa binadamu.

“Uchaguzi huu una mitihani kwetu, tumefanya jitihada zote, lakini wenzetu wamekuwa wakitumia maneno makali, hasa katika Jimbo la Ukonga, tukasema tusiwajibu jukwaani tukapeleka malalamiko yetu katika kamati ya maadili ya uchaguzi, wakaitwa na miongoni mwa adhabu walizopaswa kupewa ni kufungiwa kufanya kampeni, kulipa fedha na kuomba msamaha hadharani kwakutumia maneno yale yale lakini hawakwenda.

“Wametakiwa kuomba msamaha, lakini hawakufanya hivyo, badala yake wakaenda kukata rufaa ambayo  ilikataliwa kwakuwa muda ulikuwa umepita, wenzetu hawa wameshindwa hata kuomba radhi, kwakifupi kile chama ni jeuri na kinafanya kinavyotaka, hakifuati sheria wala maadili ya uchaguzi,” alisema Polepole.

Alisema pia kuna taarifa za chama kuandaa wanachama wake ili wafanye vurugu siku ya uchaguzi kwa kutumia vijana ambao wamewaandikisha kama mawakala.

“Tumeshatoa taarifa katika vyombo husika, zipo taarifa za uwepo wa makundi ya vijana ambao ni wanachama wa Chadema walioandikishwa kama mawakala wa vyama kutoka NLD na NCCR kwa lengo la kuja kufanya vurugu katika vituo kwakuwa wanajua wameshashindwa,” alisema Polepole.

Alisema baadhi ya vijana hao pia watatumika kuwatisha wakina mama wanaojipanga kwenda kupiga kura na kuichagua CCM ili washindwe kutimiza haki hiyo ya msingi.

Mbali na malalamiko ya Jimbo la Ukonga, Polepole pia alidai uwepo wa matukio ya ugawaji rushwa wa vitu  mbalimbali, ikiwepo sukari katika Jimbo  la Monduli.

“Monduli sasa wanagawa fedha na sukari kwenye maboma na zoezi hili linaongozwa na  mgombea wao wa 2015, Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) Monduli  mnapaswa kuchukua hatua, tunafuatilia kwa ukaribu na hatutachoka kulalamika,” alisema Polepole.

Katika hatua nyingine, Polepole amesema Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, anategemea kuongoza wanachama wa chama hicho katika mkutano wa kufunga kampeni za kugombea ubunge Jimbo la Ukonga wakati katika Jimbo la Monduli zitafungwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Rodrick Mpogolo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles