25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

CCM, UKAWA VITANI UCHAGUZI WA MADIWANI 43

Na MWANDISHI WETU -DAR ES SALAAM

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 Novemba 26, mwaka huu.

Kwa mujibu wa tangazo hilo la NEC, sasa ni wazi mapambano ya kisiasa yanahamia katika jukwaa, ambapo ushindani mkali unatarajiwa kuwa kati ya CCM na Umoja wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, ilisema uchaguzi huo unafanyika kutokana na sababu mbalimbali.

Alisema sababu mojawapo ni pamoja na baadhi ya madiwani kufariki dunia, kujiuzulu, kutokuhudhuria vikao na wengine ushindi wao kutenguliwa na mahakama.

Miongoni mwa kata hizo ni pamoja na zile za madiwani waliojizulu mkoani Arusha na Kilimanjaro, kwa kile walichokieleza kuwa wanamuunga mkono Rais Dk. John Magufuli.

Jaji Kaijage alisema Tume imetangaza kufanyika kwa uchaguzi huo mdogo baada ya waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kuitaarifu NEC uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata hizo 43 zilizoko katika halmashauri 36 na mikoa 19 ya Tanzania Bara.

Aliainisha kifungu cha 13 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, sura ya 292, kinampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, kuitaarifu Tume kuhusu kuwapo kwa uchaguzi huo mdogo wa madiwani.

“Baada ya kupokea taarifa hiyo na kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa; Sura ya 292, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina wajibu wa kuitisha na kuendesha uchaguzi mdogo katika kata hizo.

“Hivyo, ninapenda kuchukua nafasi hii kutoa taarifa kuwa, Tume imepanga kuendesha uchaguzi mdogo katika kata 43 Novemba 26, mwaka huu,” alisema Jaji Kaijage.

Mwenyekiti huyo wa NEC alisema ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo itaanza Oktoba 26, mwaka huu, ambapo kutafanyika uteuzi wa wagombea udiwani na kampeni za uchaguzi huo mdogo zitaanza Oktoba 27 na kumalizika Novemba 25, mwaka huu.

Alivikaribisha vyama vya siasa, wadau wote wa uchaguzi pamoja na wananchi kwa ajili ya kushiriki kwenye uchaguzi huo utakaozingatia ratiba.

“Vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi wazingatie matakwa ya Katiba, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani) za mwaka 2015, Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015 pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa au yatakayotolewa na Tume wakati wote wa uchaguzi mdogo,” alisema.

Jaji Kaijage pia alizitaja kata hizo 43 zitakazoshiriki uchaguzi huo mdogo kuwa ni pamoja na Musa (Wilaya ya Arusha), Muriet (Halmashauri ya Jiji la Arusha), Moita (Wilaya ya Monduli) na Ambureni, Ngabobo, Maroroni, Leguruki, Makiba, zote kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Meru, mkoani Arusha.

Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam ni pamoja na Kata ya Mbweni (Manispaa ya Kinondoni), Kijichi (Manispaa ya Temeke) na Saranga katika Manispaa ya Ubungo.

Kata nyingine ni ya Chipologo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma.

Geita, Kata zitakazoshiriki uchaguzi huo ni Bukwimba Halmashauri ya Nyang’wale, Senga katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita.

Jaji Kaijage pia alizitaja Kata za Kitwiru (Halmashauri ya Manispaa ya Iringa), Kimala (Kilolo) zote kutoka Mkoa wa Iringa.

Kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro ni Bomambuzi (Manispaa ya Moshi), Mnadani (Halmashauri ya Wilaya ya Hai), Machame Magharibi na Weruweru katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Lindi; Kata ya Chikonji (Halmashauri ya Manispaa ya Lindi), Mnacho (Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa).

Manyara; Kata ya Nangwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’, Mbeya; Kata ya Ibidhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe.

Mkoa wa Morogoro Kata zitakazoshiriki ni Kiloka (Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro) na Sofi katika Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi.

Mtwara; Kata ya Milongodi (Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba), Reli (Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara  Mikindani), Chanikanguo (Halmashauri ya Mji wa Masasi).

Mwanza; Kata ya Kijima (Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi), Mhandu (Halmashauri ya Jiji la Mwanza).

Rukwa; Kata ya Sumbawanga (Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga).

Ruvuma; Lukumbule, Kalulu (Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru), Muongozi  (Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga), huku Mkoa wa Singida Kata itakayoshiriki uchaguzi huo ikiwa ni Siuyu, katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Mwisho

Makonda aimarisha Sekta ya Afya Dar

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekagua ujenzi wa Jengo la Huduma ya Dharura katika Hospitali ya Rufaa Temeke, ambalo ujenzi wake unafadhiliwa na Ubalozi wa Japan hapa nchini.

Ujenzi wa jengo hilo unagharimu Sh milioni 800, ambazo ni jitihada binafsi za RC Makonda, baada ya kumtafuta Balozi wa Japan na kumweleza changamoto ya ukosefu wa kitengo cha huduma za haraka kwenye hospitali za mkoa na baada ya mazungumzo, Balozi alipokea ombi  hilo.

 

Alisema kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na wagonjwa wanaohitaji huduma ya haraka kuikosa huduma hiyo.

“Jengo hili ni mahususi kwa ajili ya wagonjwa wote wanaohitaji huduma ya haraka, hususani majeruhi wa ajali, wanaougua malaria kali, maumivu ya tumbo, wanaobanwa na kifua, wajawazito, homa kali, ajali ya moto na magonjwa yote yanayohitaji huduma ya haraka.

“Wagonjwa wanaohitaji huduma ya haraka wanaofikishwa hospitalini hapa wamekuwa wakipelekwa Hospitali ya Muhimbili, ambako ni mbali kutoka Temeke, hivyo kusababisha wengi wao kupoteza maisha wanapokuwa barabarani,” alisema Makonda.

Alisema baada ya kumalizika kwa jengo hilo, ujenzi wa majengo ya huduma ya haraka utahamia kwenye Hospitali za Amana na Mwananyamala, ili kuipunguzia mzigo Muhimbili.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Dk. Aman Malima, alisema kwa siku wanapokea wagonjwa kati ya 1,800 hadi 2,000, kati ya hao, 200 ni wagonjwa wanaohitaji huduma ya dharura.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles