33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

CCM Mwanza wavurugana

Anthony Diallo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo

NA WAANDISHI WETU, MWANZA

HALI ya hewa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), mkoani Mwanza siyo shwari baada ya kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa kuvunjika huku Mwenyekiti wa Mkoa, Anthony Diallo na Katibu, Joyce Masunga, wakirushiana maneno makali.

Taarifa za uhakika kutoka katika kikao hicho zinaeleza kuwa baadhi ya maneno makali waliorushiana viongozi hao ni pamoja na ‘andazi’…, ‘kiazi’…, ‘mpuuzi umehongwa’.

Kwa mujibu wa habari hizo, hali hiyo ilimfanya Mwenyekiti Diallo amtimue katibu wake katika kikao hicho kilichafanyika katika ofisi ya Mwenyekiti huyo.

Inaelezwa kuwa kikao hicho cha Juni 27 mwaka huu, kilivunjika muda mfupi baada ya kuanza ajenda ya yatokanayo na kikao kilichopita.

Katika yatokanyo, ilidaiwa kuwa vikao vya CCM vya Wilaya ya Misungwi vimekuwa vikiongozwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Wilaya hiyo, Dalali Shibiliti, badala ya mwenyekiti wa wilaya.

Wakati wa kulijadili suala hilo, Katibu wa Mkoa, Joyce Masunga, alitoa ufafanuzi akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha katiba ya CCM.

Masunga alieleza kuwa anayepaswa kuendesha vikao hivyo ni Mwenyekiti na siyo mjumbe wa NEC wa wilaya hali iliyosababisha mjumbe, Bernard Polycarp, kunyoosha mkono na kumshambulia katibu huyo.

Polycarp alidai kuwa Masunga anampigia debe Mbunge wa Jimbo la Misungwi ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati), Charles Kitwanga, ili apite bila kupingwa katika uchaguzi mkuu ujao.

“Masunga alimjibu kwamba alipokuwa katika ziara ya kazi wilayani humo, viongozi mbalimbali wa Chama walieleza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani na kumtaja mbunge huyo kwa kuyafanikisha.

“Kwa sababu hiyo Masunga aliwahoji iwapo viongozi karibu wote wamemfagilia atakuwa anachukiwa kwa lipi na kwamba ingekwa ni Kilimanjaro viongozi wangesema apite bila kupingwa,” kilieleza chanzo chetu kikimnukuu Masunga.

Ilielezwa kuwa baada ya maelezo hayoya Masunga, Diallo aliingilia kati na kumtaka atulie na kumkumbusha kwamba hatakiwi na anapaswa kuondoka Mwanza.

Taarifa zinasema matamshi hayo ya Diallo yalizua vurugu ambako yeye (Diallo) walirushiana maneno makali hadi Mwenyekiti akamwamuru Masunga kutoka nje ya kikao.

“Mwenyekiti alicharuka na kumtolea maneno makali Katibu… naye alimjibu kuwa yeye siyo andazi la kutoka tu vinginevyo yeye ni kiazi… lakini ukweli ndiyo huo MNEC hawezi kuongoza vikao vya wilaya,” kilieleza chanzo chetu.

Ilielezwa kuwa hali hiyo iliwaacha baadhi ya wajumbe wakiduwaa huku wengine wakisisitiza katibu atoke naye ikabidi atoke nje ya kikao akifuatiwa na makatibu wake wasaidizi; Sukwa na Zubeda Mbaruku na kikao kuvunjika.

Chanzo cha mgogoro

Kuibuka kwa mgogoro huu kunadaiwa kunatokana na makovu ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambako Diallo akiwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) Mkoa wa Mwanza alidaiwa aliendesha kampeni za kumkwamisha Charles Kitwanga kushinda ubunge Misungwi ili mshindi awe Jacoub Shibiliti (sasa MNEC wa Misungwi) ambaye Diallo alikuwa akimuunga mkono.

Sababu nyingine inayotajwa kuwa chanzo cha mgogoro huo ni hatua ya Mbunge Kitwanga kufuatilia na kusimamia kwa ukamilifu mapato ya Halmashauri ya Misungwi yaliyokuwa yakifujwa na baadhi ya viongozi na watendaji.

Hatua hiyo ilisababisha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Polycarp ambaye inaelezwa ni rafiki wa Diallo, kusimamishwa uenyekiti na CCM. Wakati huo Marehemu Clement Mabina ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Mwanza na Katibu akiwa Masunga.

Polycarp alisimamishwa uenyekiti kutokana na ripoti ya Mkaguzi na Mdibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo iliibua ubadhirifu wa zaidi ya Sh bilioni 2 zilizodaiwa kutafunwa na baadhi ya watendaji. Ripoti hiyo pia ilieleza kuwa Polycarp alikuwa akifanya biashara na halmashauri yake.

Kauli ya Joyce Masunga

Akizungumza na MTANZANIA kwa simu kuhusu kuvurugika kwa kikao hicho, Masunga alikuja juu akisema aliyevujisha taarifa hizo hafai kwa kuwa kikao hicho kilikuwa ni kikao cha ndani.

“Aliyekueleza taarifa hizo hafai, mwambie afuate ya kwake… kikao hicho kilikuwa cha ndani na cha siri hakuna mhudumu au mtu yeyote asiyehusika aliyehudhuria… anakuambia wewe mwandishi wa habari ili iweje,” alihoji Masunga na kueleleza kuwa masuala yote ya kikao hicho anapaswa kuulizwa Mwenyekiti wake.

Mwenyekiti Diallo

Diallo naye alipotafutwa alisema hawezi kuzungumzia mambo yaliyotokea katika kikao hicho kwa kuwa vikao vya kamati ya siasa ni vikao vya siri.

Kuhusu makundi yaliyopo ndani ya Chama hicho, alisema yeye anasimamia kitu kiitwacho CCM na kamwe katika uongozi wake hawezi kuongoza chama hicho kwa kufuata makundi.

“Ninawatumikia wana CCM wote walionichagua kuwaongoza katika kipindi cha miaka mitano. Kama kuna watu wana makundi mie siwezi kuyumbishwa, ninasimamia Katiba ya CCM na si vinginevyo,” alisema Diallo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles