28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

CCM inaweza kubadilika katika azma ya kutafuta mabadiliko?

HILAL K SUED

KWA binadamu yeyote kubadilika ni ufunguo sahihi wa kujinasua, wahenga walipata kunena, kwani kuwabadilisha wengine ni kibarua kigumu.

Mtu unaweza kushawishi, kuwatia moyo, kuwalaghai au njia nyingine yoyote lakini mwisho wa siku, kubadilika wewe mwenyewe ndiyo njia ya haraka zaidi kupata matokeo yanayokusudiwa. Isitoshe, njia hiyo inakufanya udhibiti ari na matendo yako.

Na huu ndiyo ukweli kwa wanasiasa wengi. Siku zote wana ari ya kuwabadilisha wengine, lakini wakishindwa huanza kujibadilisha wenyewe.

Lazima pia tukubali kwamba unafiki na tamaa, katika mazingira fulani, husaidia wanasiasa kuihama misimamo yao ya awali, huku wengine mabadiliko wanayofanya huwa ni ya dhati kabisa kwa manufaa ya watu wengi.

Hapa kwetu sauti kubwa zimekuwa zikisikika kwamba baada ya zaidi ya nusu karne ya uhuru, nchi inahitaji mabadiliko kwani ubwetekaji (complacency) miongoni mwa chama tawala umekuwa ukiathiri sana ari ya wananchi katika kupiga hatua kubwa ya maendeleo ya kweli – maendeleo ya watu.

Na kama wananchi hawawezi kupata mabadiliko wanayotaka kupitia chama tawala, basi wanayo haki ya kuyatafuta mabadiliko hayo kutoka chama kingine.  Aliyoyasema haya si mwingine, bali Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Ndiyo maana mwaka 2015 alivyoonekana kutokea pale mwanasiasa mashuhuri nchini na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu azma yake ya kujibadilisha katika lengo la kutafuta mabadiliko.

Lakini kama ilivyo ada kutokana na ile hali ya siku zote ya ‘ubwetekaji” – alishambuliwa kutoka kila kona na mara akawa mtu mbaya kuliko wote waliowahi kutokea katika nchi hii na waliowahi kulelewa na chama hicho tawala – CCM.

Kwani mtikisiko aliouleta katika chama haukuwahi kutokea katika historia ya nchi hii – na hasa tangu demekrasia ya vyama ilipoanza.

Miongoni mwa sifa bora za uongozi ni kwa kiongozi kuficha hofu au ile hali ya kuchanganyikiwa mbele ya wengine iwapo chochote kitaenda sivyo ndivyo kutokana na maamuzi yako au yale ya walio chini yako. Kamwe usijaribu kuonyesha kwamba mpinzani wako amekuzidi akili.

Hii ni kwa sababu katika siasa kuna wakati ambapo “ukimya” huwa ni ishara ya sauti kubwa. Na pia kuna wakati kuwa kiongozi bora ina maana kuwa na uwezo wa kufanya ‘timimg’ katika maamuzi yako… kuna wakati wa kuyanyamazia mambo ili kuwaacha watu wajipeleke wenyewe katika hatima yao… na pia kuna wakati wa kujitayarisha na kuokota mabaki baada ya matokeo – yoyote yake – hasi au chanya.

Watu wengi, hata ndani ya chama tawala, wanakubali kwamba chama hicho kimefikia wakati mgumu katika historia yake na hii yote imesababishwa na chama chenyewe. Na jinsi chama kinavyotafakari mikakati yake ya kuendelea kukaa madarakani, wengi hawaamini kwamba kuna siku chama kinaweza kujikuta ni chama cha upinzani, iwapo kitaweza kuishi kama chama baada ya hapo.

Hali hii inaajiri pamoja na mikakati ya miaka yote tangu chama hicho kilipokuwa chama pekee cha siasa nchini kupitisha mabadiliko katika katiba na sheria zingine zilizoanzisha mfumo wa demokrasia ya vyama vingi.

Iliziba mianya yote ya vyama hivyo kushika dola, kama vile kuruhusu vyama kuungana na kugombea chaguzi kwa jina la muungano huo (kama ilivyo kwa jirani zetu wa Kenya). Siku zote sheria ya vyama imekuwa ukihakikisha kuna utitiri wa vyama dhidi ya CCM hakuna umoja dhidi yake.

Hata kumeguka kwa CCM kuliangaliwa na kuhakikishiwa kwamba hilo haliwezi kutokea. Sote twakumbuka mwaka 2010, miezi michache kabla ya Uchaguzi Mkuu, pale Chama Cha Jamii (CCJ) kilipoanzishwa. Wengi hawakulielewa hili wakati ule lakini suala zima likaja kuwekwa hadharani baadaye, baada ya uchaguzi.

Kwanza kabisa wengi tulishangaa kwa nini Msajili wa Vyama, wakati ule John Tendwa alikuwa anacheza danadana kubwa katika kukipa usajili chama hicho kwani kama ilivyokuwa ikiaminika siku zote uwingi wa vyama katika upinzani ndiyo nafuu ya CCM katika uchaguzi.

Lakini kwa CCJ, utawala wa CCM haukutaka kabisa kukisajili chama hicho. Tendwa alikuwa akitoa sababu zisizokuwa za msingi sana kama vile hakuwa na hela za uhakiki wa wadhamini (wadhamini 200 katika mikoa 10).

Lakini kumbe danadana hizo zilikuwa za kimakusudi tu bila shaka kutoka kwa utawala kwa sababu CCJ kilikuwa kimeanzishwa na vigogo kadha ndani ya CCM ambao walikuwa tayari kuhamia chama hicho mara tu baada ya chama kusajiliwa na hivyo kuwepo kwa uwezekano wa kuipasua CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo.

Hivyo basi CCJ kilikosa usajili kwa sababu tu kilionekana tishio kubwa kwa chama tawala. Ingekuwa ni Chadema ambako vigogo wake ndiyo walitaka kukihama chama basi chama hicho kipya kingesajiliwa kwa kasi ya zimamoto.

Jaribio la pili la kuiondoa CCM kupitia sanduku la kura likaja miaka mitano baadaye (2015) na naweza kusema liliwastukiza sana watawala, hawakutarajia kabisa na yaliyojiri sasa ni historia. Lakini bila shaka hilo halitakuwa la mwisho.

Lakini kuna kitu kimoja utawala wa CCM hawakuliangalia vizuri wakati wanaruhusu mfumo wa vyama vingi – kutoa ruzuku kwa vyama vya upinzani. Kuna dalili kwamba ruzuku kwa vyama vya siasa inaweza ikasitishwa muda si mrefu kutokea sasa. Hili nitaeleza hapo mbele. Lakini bora nielezee kwa kifupi sana umuhimu wa fedha katika kuendesha vyama vya siasa.

Kuna nukuu moja maarufu ya Groucho Marx, Mmarekani mcheza sinema mchekeshaji (comedian) aliyeishi karne iliyopita. Siku moja alikuta watu njiani ambao walitumia muda mwingi kuisifia nyumba moja ya kifahari iliyokuwa karibu na ufukwe wa bahari.

Baada ya muda aliwasogelea na kuwaambia: “Nawahakikishia hiyo nyumba si chochote si lolote. Hebu ondoa tu bahari na uone iwapo uzuri wake utaendelea kuwepo.”

Hakuna anayeweza kubisha ukweli kwamba fedha ni msingi mkubwa wa kuendesha karibu kila kitu – serikali, makampuni, taasisi, familia na na vyama vya siasa pia. Pasipo na vyanzo vya uhakika vya mapato basi mambo yanakuwa si shwari.

Na kwa vyama vya siasa bila fedha haviwezi kujiendesha kwa sababu ada kutoka kwa wanachama ni kitu kilichokuwapo enzi zilizopita – tena kwa vyama vyote.

Angalia vile vyama vidogovidogo visivyokuwa na ruzuku kutoka serikalini. Vipo vipo tu na baadhi yao vipo kwa sababu ya kutumika katika kazi fulani fulani tu, vinginevyo havina uhalali wowote wa kuwepo.

Serikali ya CCM iliweka uwepo wa ruzuku bila shaka baada ya kukifikiria chama chake kwanza (CCM) wapi kitakuwa kinapata fedha za kujiendesha. Kwani huko nyuma enzi za mfumo wa chama kimoja CCM ilikuwa inapewa fedha kutoka Hazina.

Na baada ya ujio wa Rais John Magufuli niliwahi kuandika kwamba kutokana na azma yake ya kubana matumizi ya serikali angefuatilia mbali ruzuku kwa vyama. Hata hivyo nilitoa tu angalizo kwamba pengine ilikuwa mapema mno kuyasema hayo.

Lakini sasa hivi dalili za kufutwa ruzuku kwa vyama vya siasa huenda zinaanza kuonekana. Kama tunavyofahamu CCM ina mali na vianzo vingi vya mapato – vingi vya tangu kikiwa chama kimoja kama vile viwanja vya mpira, majengo na miradi mingine.

Lakini kwa miaka mingi kumekuwa na uangalizi mbovu wa mapato kutokana na mali hizi na mapato mengi yalikuwa yanaingia mifukoni mwa baadhi ya viongozi wanayosimamia.

Mwaka juzi mwenyekiti wa chama hicho aliunda kamati ya kulifuatilia suala hilo na mwaka jana kamati hiyo ilimkabidhi mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli ripoti yake.

Inasadikiwa ripoti inaonyesha uwepo wa utafunjaji mkubwa wa mapato yanayotokana na mali na miradi yake mbalimbali nchini.

Sasa iwapo itabainika kwamba kumbe CCM inaweza kujiendesha na fedha kutoka vyanzo vyake vya mapato, basi huenda serikali ikafuta ruzuku kwa vyama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles