BONDIA wa uzito wa kati, Saul ‘Canelo’ Alvarez, jana amefanikiwa kumdunda mpinzani wake, Liam Smith, katika mzunguko wa tisa wa pambano la uzito wa kati la kugombea mkanda wa WBO lililofanyika jijini Texas, Marekani.
Kipigo hicho kilichokuwa kikishuhudiwa na zaidi ya watu 51,240, kilikuwa cha mara ya kwanza kwa Smith ambaye aliwahi kushinda mapambano nane kwa ‘knock out’.
Baada ya ushindi huo, sasa Canelo anatarajia kupambana na bondia machachari, Gennady Golovkin, ambaye amekuwa akisubiri kwa muda mrefu kuzichapa na nyota huyo.
Alvarez ambaye kwa sasa anaonekana kuwa katika kiwango bora cha ngumi, kabla ya pambano hilo alitarajiwa kupambana na Oscar De La Hoya na Golden Boy.
“Kama nitaendelea kusubiri kwa muda mrefu na kupata uzoefu wa kutosha, nitaweza kupambana kwa kiwango bora kama nilichokionesha katika mchezo huu, hata hivyo nilichukizwa sana na matokeo haya ingawa Canelo alikuwa bora zaidi yangu na alinishinda kimbinu,” alithibitisha Smith baada ya kudundwa na Canelo.
“Ilinichukua muda mrefu kujibu mapigo, lakini niligundua sikuwa na mbinu za kutosha na kumfanya adui yangu afikiri mara mbili kwani mwenzangu aliweza kumudu kila kitu,” alisema Smith.
Kwa upande wake, Canelo alisema ndoto yake ya kushinda pambano hilo ilifanikiwa kwa kujituma kwa bidii akiwa ulingoni.
“Niliahidi kwamba ningeshinda pambano hili na kuwa bingwa kama ilivyotokea leo, nilipambana ingawa nilikuwa katika mazingira magumu ulingoni.
“Niliumia mkono wangu wa kulia, hivyo ilinilazimu kutumia wa kushoto mara kwa mara,” alisema Canelo na kuongeza kuwa mpinzani wake alikuwa makini ulingoni, alikuwa akifikiri kabla ya kurusha ngumi dhidi yake.
Canelo alisema kuna wakati alilazimika kutumia mkono wa kushoto ili kutunza nguvu mkono wa kulia.
“Niliumia mkono wa kulia katika mzunguko wa pili wakati niliporusha ngumi iliyotua juu ya kichwa cha mpinzani wangu,” alisema Canelo.