23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

CAG akiuka agizo la Rais Magufuli

cag-mussa*Adaiwa kutumia Sh milioni 15 kwa siku tatu

Na Masyaga Matinyi

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad, amekiuka agizo la Rais Dk. John Magufuli, baada kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.

Vyanzo vya habari kutoka ofisini kwake, vimedai kuwa CAG aliondoka nchini Jumamosi (Desemba 12, 2015) kwenda jijini Nairobi, Kenya na kurejea nchini Jumanne wiki hii.

Taarifa hizo, zimesema CAG alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi, kazi ambayo haina uhusiano na ofisi yake, lakini alilipiwa gharama zote na ofisi yake.

“Bosi wetu aliondoka kwenda Nairobi Jumamosi iliyopita na kurejea Jumanne, alikwenda kutoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Nairobi bila kibali cha Ikulu, alipaswa kupata kibali kwa sababu ofisi yake ndio ililipa gharama zote.

“Jumla ya gharama zinafika Sh milioni 15, ambazo ni pamoja na posho, tiketi ya ndege, hoteli na gharama nyinginezo,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu safari hiyo, Profesa Assad hakuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo, zaidi ya  kutishia kwenda mahakamani.

“Wewe si umesema umepata taarifa kutoka vyanzo vyako na umenipigia ‘for validation’, sasa mimi nakwambia hizo taarifa si za kweli na mkiandika tutachukua hatua,” alijibu CAG.

Baada ya muda, Profesa Assad alipiga simu kwa mmoja wa wahariri wa gazeti hili akimtaka afike ofisini kwake akachukue nyaraka za kuthibitisha kuruhusiwa na kusafiri nje ya nchi na ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue.

Kutokana na mhariri huyo kuwa nje ya Dar es Salaam, ofisi ilimtuma mwandishi mwingine kwenda katika ofisi ya CAG ili kuchukua nyaraka hizo.

Mwandishi alipofika, CAG alikataa kumpa wala kumwonesha nyaraka hizo, akidai yeye alitaka amwonyeshe mhariri aliyempigia simu na si mwandishi huyo.

Baada ya mwandishi kuondoka ofisini, CAG alimtumia ujumbe mfupi mhariri aliyewasiliana naye awali, akisema kwa kuwa alizungumza naye hawezi kuendelea kuzungumza chochote.

“Sitatoa nyaraka yoyote, kama unaamini chanzo chako cha habari endelea tutakutana kwa wasimamizi wenu,” alisema CAG katika ujumbe huo.

Juhudi za kumpata Balozi Sefue kuzungumzia suala hilo hazikuzaa matunda. Baada ya kupigiwa muda mrefu aliandika ujumbe mfupi wa simu ukisema. “Nimebanwa na majukumu siwezi kupokea simu yako,” ulisomeka ujumbe huo.

Baada ya ujumbe huo, mwandishi alimwandikia ujumbe mfupi wa kueleza nia ya kumtafuta, hata hivyo hakujibu.

Tukio hilo la CAG limekuja siku mbili baada ya Rais Dk. John Magufuli kuagiza kusimamishwa kazi kwa watumishi wanne wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kosa la kusafiri nje ya nchi bila kibali cha Ikulu.

Watumishi wa taasisi hiyo waliosimamishwa kazi ni Ekwabi Mujungu (Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu), Doreen Kapwani, Rukia Nikitas na Mary Mosha.

Profesa Assad aliteuliwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba 5, 2014.

Kabla ya uteuzi wake, alikuwa Profesa Mshiriki, Idara ya Uhasibu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na alichukua nafasi ya Ludovick Utouh ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Profesa Assad ni msomi, mwenye weledi, ujuzi na uzoefu mkubwa wa uhasibu na udhibiti wa fedha ambaye ana Shahada ya Uzamivu wa Uhasibu (PHD in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Southampton, Uingereza mwaka 2001 na Shahada ya Uzamivu katika Udhibiti wa Fedha (MA in Financial Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City, Jamhuri ya Ireland mwaka 1991.

Profesa Assad pia ana Stashahada ya Kitaaluma ya Uhasibu (Professional Diploma in Accounting) kutoka Chuo Kikuu cha Dublin City mwaka 1990 na Shahada ya Biashara (Bachelor of Commerce) ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam mwaka 1988.

Pamoja na uzoefu wa kitaaluma, Profesa Assad anao uzoefu mkubwa katika eneo la uhasibu na ukaguzi. Alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) kwa miaka saba (2007 – 2014).

Ni Rais na Mjumbe wa Chama cha Wahasibu Afrika (Pan African Federation of Accountants) tangu mwaka 2012 na pia ni mjumbe wa bodi kadhaa za wakurugenzi nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles