27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BYE BYE RAIS MUGABE 1980-2017

Na WAANDISHI WETU NA MASHIRIKA


RAIS wa Zimbabwe, Robert Mugabe, amejiuzulu wadhifa wake baada ya kuwa katika shinikizo la kuachia madaraka kwa takribani wiki moja tangu jeshi lilipomuweka kizuizini, likisema linataka kupambana na wahalifu waliomzunguka.

Mugabe (93), ambaye ametawala taifa hilo kwa miaka 37, tangu alipoingia madarakani mwaka 1980, alitarajiwa kujiuzulu mwisho wa juma lililopita, lakini wengi walibaki mdomo wazi baada ya kulihutubia taifa na kusema ataendelea kubaki madarakani kama rais halali wa Zimbabwe.

Jana muda mfupi baada ya Bunge kuanza kujadili namna ya kumwondoa madarakani Mugabe na kumshtaki, Spika wa Bunge, Jacob Mudenda, alitangaza kuwa rais huyo amejiuzulu na hivyo mpango huo wa kujadili namna ya kumtoa madarakani na kumshtaki ukaahirishwa.

Taarifa hiyo ya kujiuzulu iliyotokana na barua ya Mugabe aliyoiwasilisha kwa Spika huyo, ilipokewa kwa shangwe kutoka kwa wabunge wa kambi zote mbili; chama tawala na upinzani.

Katika barua yake ya kujiuzulu, Mugabe aliandika: “Mimi Robert Gabriel Mugabe, kufuatana na ibara 96 ya Katiba ya Zimbabwe, nawasilisha rasmi uamuzi wangu wa kujiuzulu kuanzia sasa.

“Uamuzi wangu wa kujiuzuu ni hiari. Nimejiuzulu ili kuruhusu makabidhiano  tulivu ya madaraka. Tafadhali toa taarifa hii ya uamuzi wangu haraka iwezekanavyo.”

Uamuzi huo wa Mugabe unakuja baada ya kubainika kwamba amejikuta akiwa ametengwa na kudhalilika baada ya ombi lake la kuwataka mawaziri wake wahudhurie kikao chake cha kila wiki kupuuzwa.

Haikuweza kufahamika mara moja hatima ya familia yake hasa mkewe, Grace (52) anayefahamika kwa matanuzi.

Anguko la ghafla la Mugabe linatokana na uhasama wa makundi mawili yanayowania kumrithi, moja likiongozwa na mkewe na jingine Mamba.

Jeshi lilitwaa madaraka baada ya Mugabe kumfukuza aliyekuwa makamu wake, Emmerson Mnangagwa ambaye ni kipenzi cha jeshi, ili kumsafishia njia mkewe Grace.

Mnangagwa, bosi wa zamani wa usalama wa taifa, anatarajia kumrithi Mugabe urais.

Ndani ya wiki moja, mambo kadhaa yalifanyika kwenye taifa hilo, ikiwa ni pamoja na chama tawala cha ZANU-PF kumvua Mugabe madaraka ya kuwa kiongozi wake.

Chama hicho, baada ya kumwondoa Mugabe, nafasi ya kiongozi wa  ZANU-PF ilipewa Mnangagwa aliyefukuzwa mwezi huu na Mugabe, na sasa anatarajiwa kuwa kiongozi ajaye wa taifa hilo. 

MNANGAGWA AMGOMEA MUGABE

Uamuzi wa Mugabe kuachia madaraka, umekuja ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka taarifa kuwa amemtaka Makamu wa Rais aliyemfukuza, Mnangagwa, arejee Zimbabwe, lakini akakataa akisema atafanya hivyo pale atakapohakikishiwa usalama wake.

Mnangagwa alisema Mugabe alimpigia simu, lakini alikataa wito wa kurudi Zimbabwe kwa kuhofia usalama wake.

Alisema hatarudi kwa sababu anahofia maisha yake kwa vile haaminiki tena kwa Mugabe.

“Aliniomba niende Ikulu na nilimjibu niko nje ya nchi na kuwa alishaondoa hadhi yangu ya umakamu wa rais na kwa sababu hiyo haina haja ya kumwona,” alisema.

Mnangagwa, aliongeza kusema kuwa kutokana na matukio yaliyotokea baada ya kufukuzwa kwake, hawezi kumwamini tena Mugabe.

“Hata hivyo, naweza kurudi tu kwa mwaliko wa wenzangu katika chama na jeshi, wakati watakapohisi uwapo wa usalama wangu,” alisema Mnangagwa.

Alisema walinzi wake waaminifu katika makazi yake, waliondolewa mara moja baada ya kufukuzwa umakamu wa rais mapema mwezi huu.

“Walinzi waaminifu kwangu, walinionya  kuwa kuna mpango wa kuniua mara nitakapokamatwa na kupelekwa polisi. Ni kwa usalama wangu ikabidi nikimbie nchi mara moja,” alisema.

Mnangagwa aliongeza kuwa alimwambia Mugabe hali ya sasa ya kisiasa na kikatiba si suala la baina yao tena, bali baina ya watu wa Zimbabwe na Rais Mugabe.

Alisema anaungana na viongozi wa jeshi na wanasiasa, wanaomtaka Rais Mugabe aheshimu maoni ya umma na kuondoka madarakani, ili nchi hiyo iweze kusonga mbele na kulinda hadhi yake.

Juzi usiku jeshi la Zimbabwe lilisema Mnangagwa atarejea nchini humo hivi karibuni na amekuwa akiwasiliana na Mugabe.

Baraza la Mawaziri

Awali jana, Mugabe aliitisha kikao cha Baraza la Mawaziri na ikaripotiwa kuwa waliojitokeza ni wanne na wengine 17 wakaudhuria kikao cha kuandaa mpango wa kumng’oa madarakani.

Kikao hicho kilichoitishwa na Mugabe, kilitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri (OPC), Dk. Misheck Sibanda, ambaye alikuwapo pia.

Mawaziri walioitikia wito huo wa Sibanda, ni Waziri wa Utalii, Mazingira na Sekta ya Ukarimu, Edgar Mbwembwe, Waziri wa Viwanda na Biashara,  Mike Bimha, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Umwagiliaji, Joseph Made na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Prince Machaya.  Imeripotiwa kuwa kutokana na akidi kutotimia, kikao hicho cha Mugabe kilishindikana.

Mawaziri wengine 17 waliripoti makao makuu ya ZANU-PF, ambako walishiriki kikao cha wabunge wa chama hicho kilichopitisha uamuzi wa kumwondoa Mugabe kikatiba.

Awali ZANU-PF iliwaonya mawaziri dhidi ya kushiriki kikao hicho cha Mugabe, ambacho kingekuwa cha kwanza tangu jeshi litwae madaraka wiki iliyopita, ikiwa ni saa chache baada ya kikao cha mwisho kufanyika.

Wakati wabunge wa chama tawala na upinzani wakikutana kwa kazi hiyo, waandamanaji walikusanyika nje ya majengo ya Bunge wakipaza sauti ‘Mugabe lazima aondoke’, huku wakipeperusha bendera ya Zimbabwe.

“Tuko hapa kwa sababu tunataka kuwa sehemu ya tukio hili muhimu la kihistoria kwa nchi hii,” alisema mmoja wa wakazi wa Harare, Samuel Wadzai. 

WABUNGE ZANU-PF WAPITISHA AZIMIO

Saa kadhaa kabla ya wabunge kukutana jana, wabunge wa ZANU-PF walikutana makao makuu ya chama hicho na kupitisha azimio kwa kauli moja kumwondoa Mugabe.

Hilo lilikuja baada ya Mugabe kukaidi shinikizo linalomtaka ajiuzulu, ambalo lilitolewa na kikao maalumu cha Kamati Kuu ya Chama cha ZANU-PF Jumapili iliyopita.

“Kufuatia uamuzi wa Kamati Kuu ya ZANU-PF iliyokutana Novemba 17, 2017 kumtaka Rais Robert Gabriel Mugabe ajiuzulu urais na ukatibu mkuu wa kwanza wa ZANU-PF, chama kimemjulisha rasmi uamuzi huu asubuhi hii,” alisema msemaji wa chama hicho, Simon Khaya Moyo.

“Kwa sababu hiyo, chama kimemwagiza kiongozi wa wabunge wake kuanzisha mchakato wa kibunge wa kumwondoa Mugabe madarakani baada ya kiongozi huyo kushindwa kumwarifu Spika wa Bunge kujiuzulu kwake kama alivyooombwa,” alisema Moyo.

Mkutano huo wa wabunge wa ZANU-PF uliohudhuriwa na wabunge 230 kati 260, uliridhia azimio hilo kwa kauli moja.

“Mchakato huu unatarajia kuwasilishwa bungeni wakati litakapokutana leo (jana),” alisema msemaji huyo.

Mugabe ambaye ameiongoza Zimbabwe kwa miaka 37, hakuonyesha dalili zozote za kukubali shinikizo la kujiuzulu, lakini jeshi likasema katika tangazo lake la juzi usiku kwamba amekubali kuzungumza na aliyekuwa makamu wake, Mnangagwa, ambaye inaaminika atachukua nafasi yake. 

MASHTAKA YANAYOMKABILI MUGABE

Katika rasimu ya hoja za kumwondoa Mugabe, chama kimemtuhumu kiongozi huyo kuwa chanzo cha ukosefu wa utulivu, kuparaganyika kwa utawala wa sheria na kusababisha kuporomoka kwa uchumi kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Sheria wa ZANU-PF, Paul Mangwana, alisema Mugabe anakabiliwa na mashtaka kadhaa, ikiwamo kumruhusu mkewe Grace kujitwalia madaraka makubwa ya kikatiba wakati hakuwa kiongozi wa kuchaguliwa.

“Shtaka kuu ni kwamba alimruhusu mkewe kujitwalia madaraka ya kikatiba wakati hana haki ya kuongoza Serikali. Mkewe anatukana watumishi wa umma, Makamu wa Rais katika mikutano ya hadhara na kulishushia heshima jeshi.

“Moja ya mashtaka mengine makuu ni kukataa kutekeleza Katiba ya Zimbabwe. Tuna maofisa wa kuchaguliwa wa majimbo, lakini hadi sasa hawajasimikwa madarakani.

“Tatu, ana umri mkubwa na hana uwezo wa kimwili wa kuweza kuongoza nchi,” alisema Mangwana.

 NINI KITATOKEA

Nafasi ya Mugabe inatarajiwa kuchukuliwa na makamu wa rais.

Jeshi ambalo linamuunga mkono Mnangagwa, lingependa kuona akichukua wadhifa huo.

Lakini kwa vile alifukuzwa, Phelekezela Mphoko – anayefahamika kuwa mfuasi wa Grace Mugabe – anaweza kuwa makamu wa rais.

Haikufahamika iwapo Mnangagwa atarudishwa katika nafasi yake ya zamani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles