24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Bwawa la Nyumba ya Mungu hatarini kupasuka

Na Safina Sarwatt-Moshi

BONDE la Maji la Mto Pangani limewatahadharisha wananchi wanaoishi jirani na Bwawa la Nyumba ya Mungu lililopo Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, kuondoka haraka kutokana na kujaa maji na kufikia mita 688.91 kutoka usawa wa bahari. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Moshi, Mkurugenzi wa Bonde la Maji la Mto Pangani, Segule Segule, alisema kuwa bwawa hilo kwa sasa tayari limeshafikia kiwango cha ujazo unaotakiwa ambapo kwa kawaida likifikia lazima litoroshe maji.

Segule alisema kuwa maji hayo yasipotoroshwa mapema athari yake ni kubwa kuliko, kwani yanaweza kuvunja bwawa na kusambaa kwenye makazi ya watu. 

“Lengo likishafika tunaruhusu maji yatoroke kwani tusipoyaruhusu yaweza kuvunja bwawa na kusambaa kwenye vijiji vinavyolizunguka na kuleta maafa kwani maji hayazuiliki,” alisema Segule. 

Alisema kuwa mvua zilizoanza kunyesha mwishoni mwa mwaka jana na kuunganisha hadi mwaka 2020, zilijaza bwawa na kuna dalili ya kunyesha mvua nyingi zaidi.

Segule alisema kuwa wametoa taarifa kwa wenzao wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuongeza uzalishaji wa umeme ili maji yaendelee kupungua katika bwawa hilo. 

Alisema kuwa mvua bado zinaendelea kunyesha huenda zikawa nyingi zaidi kuliko mvua za masika. 

“Kwa hali ya kawaida mvua zilizonyesha mwaka jana zimetosheleza kabisa, na kwamba zaidi ya miaka 10 mfululizo bwawa hilo halijawahi kujaa,” alisema Segule. 

Alisema kuwa Bwawa la Nyumba ya Mungu kuanzia Januari 1, mwaka huu tayari limeshafikia kiwango kinachotakiwa.

“Tulipoona mwelekeo wa bwawa hilo kujaa tulitoa taarifa kwa wakuu wa wilaya ambazo zinazunguka bwawa hilo ili kutoa tahadhari kwa wananchi kuondoka mapema kabla ya madhara hayajatokea,” alisema Segule. 

Alisema kuwa mwelekeo wa bwawa mwaka huu hautabiriki kutokana na kwamba bado mvua za vuli hazijaanza.

Alisema kuwa timu ya wataalamu wa bonde hilo wako katika maeneo ya bwawa kufanya utafiti kama mvua zitaendelea wanaweza kudhibiti vipi bwawa hilo lisiathiriwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles