30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

BURHAN HEMED: MKONGWE ANAYEKUBALI MFUMO WA MABADILIKO SIMBA, YANGA

Na HENRY PAUL-DAR ES SALAAM


burhan-hemedJINA la winga Burhan Hemed sio geni masikioni mwa wapenda soka nchini hususan wa klabu ya Yanga, kwasababu ameichezea timu hiyo yenye maskani yake makuu mtaa wa Jangwani na Twiga katika kipindi cha kuanzia mwaka 1976 hadi 1982.

Hemed pamoja na kuichezea klabu ya Yanga kwa miaka saba mfululizo, pia kabla ya kuichezea timu hiyo ameichezea klabu ya Co-op. United ya Mwanza.

Nyota huyo wakati anacheza soka ya ushindani miaka ya nyuma alisifika mno kutokana na kasi, mashuti makali na uwezo mkubwa aliokuwa nao wa kupachika mabao hali iliyowafanya mabeki wa timu pinzani kupata wakati mgumu kumkabili.

Hivi sasa Hemed haonekani viwanjani kama zamani kwa maana ya kucheza soka ya ushindani, kwasababu amestaafu kucheza mpira mwaka 1982 akiwa na klabu ya Yanga na hivi sasa amegeukia shughuli ya ukocha.

Katika kazi yake hiyo ya ukocha mkongwe huyo amekuwa akifundisha timu mbalimbali za vijana wenye umri mdogo hapa jijini baada ya klabu ya Yanga kuamua kuwasomesha wachezaji wa zamani wa timu hiyo kozi ya awali ya ukocha ambayo ilianza Septemba 4, 2010 hadi Septemba 18, 2010.

Hivi karibuni SPOTI KIKI lilikutana na mstaafu huyo wa soka na kufanya naye mahojiano kuhusiana na masuala ya soka yanayojiri hapa nchini kwa hivi sasa.

Katika mahojiano hayo kwanza, Hemed akiwa kama mdau mkubwa wa mchezo huu wa soka anakubali mabadiliko yanayotaka kufanywa na klabu kongwe hapa nchini Yanga na Simba katika suala la umiliki wa hisa na ukodishwaji.

Pia katika mazungumzo hayo Hemed anawapa somo wanachama wa klabu hizi mbili kongwe nchini Yanga na Simba kuwa zinatakiwa ziendeshwe kisasa na suala la hisa na ukondishwaji ndio njia pekee itakayozilitea maendeleo timu hizi badala ya kutegemea mapato ya mlangoni na kutembeza bakuli.

Akizungumzia umiliki wa hisa na ukodishwaji wa klabu nchini hususan Yanga na Simba, Hemed anatoa maoni yake akisema:

“Suala la umiliki wa hisa na ukodishwaji wa klabu ni zuri kwa sababu utazifanya timu zetu hizi ziwe na maendeleo kuliko kutegemea mapato ya mlangoni, hivyo nawashauri wanachama wafanye marekebisho ya katiba zao ili zoezi hili lifanyike haraka iwezekanavyo.

“Klabu nyingi duniani zenye maendeleo makubwa kifedha zimefikia hatua hiyo siku nyingi baada ya kuachana na kutegemea mapato ya milangoni na badala yake kutoa nafasi kwa watu wenye uwezo kifedha kumiliki hisa.

“Hivyo na sisi klabu zetu kongwe Yanga na Simba kama zinataka kujikomboa kiuchumi ni vyema zikatoa mwanya kwa watu wenye uwezo kifedha kuwa na hisa.

“Wanachama wa klabu hizi mbili wanatakiwa wafahamu umuhimu wa suala la kumiliki hisa na ukodishwaji wa timu kuwa ndiyo njia bora na sahihi ambayo itakayowainua kiuchumi kuliko kutegemea mapato ya mlangoni na kutembea bakuli.

Burhan anamalizia kwa kuwashauri wanachama wa klabu kama wanataka maendeleo ya soka katika timu zao ni vyema kuwachagua viongozi wenye upeo mkubwa wa soka na kuachana na wale ambao wanataka uongozi kwa maslahi yao binafsi.

“Kiwango cha soka letu nchi hakipandi kwa kasi kubwa moja ya sababu ikiwa ni klabu zetu, vyama vya soka nchini kuanzia wilayani hadi ngazi yaTaifa kuongozwa na watu wenye upeo mdogo wa mchezo huu.

“Nchi nyingi duniani zilizoendelea kisoka wamefikia hatua hiyo moja ya sababu ni kwamba klabu zao, vyama vya soka vinaongozwa na watu wenye kufahamu kiundani mchezo huu, hivyo na sisi hatuna budi kuwachagua watu wenye upeo mkubwa wa soka na kuachana na wale wanaotaka uongozi kwa ajili ya kujenga majina yao, lakini si kuendeleza soka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles