26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lapitisha Muswada wa Sheria ya Habari

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), akichangia hotuba ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016 Dodoma jana.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), akichangia hotuba ya Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016 Dodoma jana.

BAKARI KIMWANGA Na GABRIEL MUSHI, DODOMA

MUSWADA wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016, umepitishwa jana na Bunge huku Serikali ikifanya marekebisho katika vifungu kadhaa kwenye muswada huo.

Hatua ya kupitishwa kwa muswada huo sasa kutawafanya wanahabari kuhakikisha wanazingatia sheria kwenye kazi zao huku wale watakaokwenda kinyume cha sheria wakijikuta wakifungiwa na Bodi Huru ya Habari kwa muda wa miezi mitatu ambapo awali walikuwa wakipoteza sifa moja kwa moja kabla ya mabadiliko hayo.

Kutokana na mvutano ulioibuka juzi kwenye hoja za wabunge, Serikali imelazimika kufanya maboresho 32 kwenye muswada huo na kuingiza vifungu vipya vitano ambavyo huenda vikatoa ahueni kwa wanahabari.

Hatua hiyo imekuja baada ya mvutano kuhusu muswada huo kudumu kwa zaidi ya miaka 23 ambao kwa mara ya kwanza uliwasilishwa bungeni mwaka 1993.

Hata hivyo, mwaka 2000 muswada huo ulifufuliwa tena lakini maoni ya wadau yalichukua muda mrefu na kusababisha kutofikishwa bungeni na baadaye mwaka 2015 uliwasilishwa kwa mara nyingine na kuibua mvutano mkali ambao ulisababisha uondolewe tena bungeni kabla ya safari hiyo kuhitimishwa mwaka huu na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

MAONI YA WABUNGE

Akichangia muswada huo kabla ya kupitishwa, Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Moleli (CCM), alisema muswada huo umekuja wakati mwafaka na unapigiwa kelele kwa sababu ni jambo zuri.

“Lakini nataka niwaambie kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji, kwa sababu tunaona kuwa Serikali yetu sikivu imeondoa vipengele vyote vilivyokuwa na utata, lakini pia muswada huu utawabana wamiliki wa vyombo vya habari kuboresha masilahi ya waandishi wa habari ikiwamo kupatiwa bima.

‘Lakini kulikuwapo na vyombo ambavyo ni kigeugeu kwani kuna kipindi gazeti la Mwanahalisi lilimkosoa mwanasiasa kama vile Lowassa lakini baadaye likaanza kumsafisha, hii inaonesha namna gani vyombo vinaweza kutumika,” alisema.

Wakati Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Devota Minja, alisema Serikali inaandika historia ya kupitishwa muswada ambao haujashirikisha wadau.

“Muswada huu unalenga kudhibiti waandishi ndio maana umeingiza vipengele vya dressing codes na mambo mengine,” alisema.

Kwa upande wake, Saada Mkuya, aliipongeza Serikali kwa kuwasilisha muswada huo kwa kuwa una mambo mengi muhimu kwa tasnia ya habari nchini ikiwamo mfuko wa mafunzo kwa waandishi wa habari.

“Naona utekelezaji unazidi kucheleweshwa hivyo namwomba waziri ajitahidi kuwahisha kanuni za muswada huu pia mwakani alete bajeti ya kuimarisha mfuko huo wa waandishi wa habari,” alisema.

SERUKAMBA NA JIPU

Katika kile kilichoonekana kujibu mapigo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, alisema yeye ni jipu ambalo limeshindakana kutumbuliwa licha ya kuitwa jina hilo na wadau.

“Ukitaka kujua muswada mzuri tazama wachangiaji, wanaopinga wengi ni masuala ya siasa tu, kwa sababu wadau awali walishiriki ila awamu ya pili hawakushiriki walikimbia wenyewe kwa makusudi na baadaye wanajadili kwenye televisheni.

Alisema wachangiaji hakuna ambaye alilenga katika kupinga vifungu vilivyo kwenye muswada huo bali walijikita katika siasa.

“Waheshimiwa wabunge mkitaka kujua muswada huu ni mzuri sikilizeni kuanzia jana (juzi) hadi leo (jana), hakuna mtu aliyepinga vifungu na kama yupo mtu asimame, wote mliamua kucheza siasa tu.

Lakini kwa maana ya sheria yenyewe hakuna mtu aliyeweka neno kwasababu kila kitu kimefanywa,” alisema. Serukamba.

Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alijikuta akirushiana maneno na mbunge mwenzake wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM).

Halima alitamka maneno (milioni 10 hizo) wakati Shonza anachangia jambo ambalo lilimkera Juliana na kumweleza mbunge huyo aache kuvuta bangi.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zainabu Zulu, alisema muswada huo unakwenda kutetea masilahi ya waandishi.

“Sote tunajua waandishi wa habari walikuwa wanahitaji jambo hili kwa muda mrefu sana… Kanuni ziharakishwe kwasababu ndizo zitasaidia katika mambo mengine,” alisema.

Zainabu alisema Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea, anauogopa muswada huo kwasababu amezoea kuwalipa kwa stori waandishi ambao anawaajiri.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema masharti ya Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 yameingizwa kama ilivyo kwenye muswada huo.

“Vifungu vyote vilivyokuwa katika sheria hii vimeingizwa kama vilivyo kwenye muswada huu kama ilivyo,” alisema Lissu.

NAPE: TUZIKE TOFAUTI

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya Bunge kupitisha muswada huo, Nape aliwataka wadau wa tasnia ya habari kuzika tofauti zao ili kutengeneza haraka kanuni za sheria hiyo.

“Nawashukuru sana wadau wote walioshiriki kupitisha kwa namna moja au nyingine muswada huu na baada ya kusainiwa na Rais Magufuli hatua inayofuata ni utungaji wa kanuni ambao utaanza mara moja.

“Niwaambie wadau kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nanyi kwa sababu ilifikia hatua kukatokea mgawanyiko ila ni matumaini yangu kuwa tutarudisha umoja wetu na kuitumia sheria hii kuboresha tasnia ya habari nchini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles