25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge lamkataa CAG

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

BUNGE limeazimia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kwa madai ya kwenda kinyume na kifungu cha 26 cha Sheria ya Kinga ya Madaraka na Haki za Bunge.

Hata hivyo, mwenyewe amesema hana taarifa za azimio hilo na yupo likizo.

Mwenyekiti wa Kamati Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emmanuel Mwakasaka, akisoma taarifa yake bungeni kuhusu shauri la kudharau na kudhalilisha Bunge la Profesa Assad, alisema katika uchunguzi wao walibaini kwamba alikiuka masharti ya kifungu cha 26 E cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kwa kutamka maneno ya kulidhalilisha bunge.

Mwakasaka ambaye ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), alisema  Profesa Assad wakati akihojiwa na kamati yake, hakujutia kosa lake na alisema maneno aliyotumia ni ya uhasibu na ataendelea kuyatumia.

“Kwa kuwa alionyesha dharau kwa kamati wakati wa mahojiano na hakujutia kutenda kosa alilofanya la kudharau na kudhalilisha Bunge  na aliendelea kusititza kuwa ataendelea kutumia maneno
yanayolalamikiwa kudhalilisha Bunge.

“Kwa kuwa kamati ilimtia hatiani Profesa Assad kwa kosa la kudharau na kudhalilisha Bunge kinyume cha kifungu 26 E cha sheria ya kinga ya madaraka na haki za Bunge sura 296, kanuni ya 54 fasihi ya 123 kanuni za kudumu ya Bunge toleo 2016, inalipa Bunge mamlaka ya kupokea na kujadili mapendekezo ya kamati hii na kisha kufanya uamuzi kwa njia ya maazimio,” alisema Mwakasala.

UTETEZI WA PROF ASSAD

Alisema Profesa Assad alikiri ni yeye ndiye aliyetoa kauli inayolalamikiwa.

Alisema CAG alisema, “Ni kweli kwamba nilifanya mahojiano na UN Radio, New York Marekani. UN Radio ya Umoja wa Mataifa  ndani ya Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ikiwamo Tanzania

“Nilihojiwa na Mtangazaji Anord Kayanda aliniuliza swali ambalo mmelisikia au kulisoma na nilijibu kitaaluma maneno yaliyotumiwa ni udhaifu wa Bunge.”

Mwakasala alisema Profesa Assad alieleza kamati kuwa hakuwa na nia ya kudharau Bunge bali tatizo lililopo ni tofauti ya tafsiri  ya maneno yaliyotumia katika mahojiano.

“Udhaifu wa Bunge ni maneno ya  kawaida kwani udhaifu ni neno la kawaida katika lugha ya ukaguzi  wa hesabu.

 “Majibu yangu katika mahojiano hayakuwa na nia ya kudhalilisha Bunge hata kidogo… katika lugha ya ukaguzi udhaifu huja kwa namna mbili, kwanza ni katika tathmini  za taasisi  na mifumo na pili ni katika kukazia hoja kuonyesha kiwango cha upungufu  ndani ya taasisi moja.

“Hapa nashadadia kuwa neno dhaifu ni neno la kawaida sana katika mzungumzo yetu ya kazi ya ukaguzi, maneno yaliyotumika ni udhaifu wa Bunge (na si Bunge ni dhaifu) kama inavyosemekana.

“Tulikuwa tunaongelea udhaifu katika utekelezaji wa mapendekezo ambayo tumeyatoa…. Si jambo jingine katika utekelezaji wa majukumu ya Bunge,” Mwakasala alimnukuu Profesa Assad.

Mwakasaka alisema alipohojiwa kuhusu maana ya neno udhaifu kwa wananchi wa kawaida ambao taaluma yao siyo wahasibu au wakaguzi, Profesa Assad alijitetea kuwa yeye alikuwa na maana ya upungufu na si vinginevyo.

Baada ya Mwakasala kusoma taarifa ya kamati yake, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, aliyekuwa akiongoza kikao alitoa nafasi kwa wabunge kujadili taarifa hiyo.

Katika mjadala huo, wabunge walikuwa na maoni tofauti mbako wengi wa CCM waliiunga mkono huku baadhi wa upinzani wakiipinga.

Baada ya wabunge kutoa maoni yao,  Dk. Tulia alilihoji Bunge kuhusu hoja hiyo, akiwakata wanaokubaliana na jambo hilo kusema ndiyo na wasiokubaliana na suala hilo kusema siyo.  “Waliosema ndiyo wameshinda, ” alisema.

Akihitimisha ripoti yake, Mwakasala alisema, “Bunge linaazimia kwamba  haliko tayari kufanya kazi na Profesa Assad, Bunge haliko tayari kushirikiana naye kwa sababu  kutokana na majukumu yake ya udhibiti na ukaguzi wa hesabu Serikali kutakiwa kufanya kazi zake na Bunge ambazo tayari ameonyesha kulidharau na kulidhalilisha, kwa hiyo Bunge linaazimia haliko tayari kufanya kazi na CAG.”

Prof Assad azungumza

Alipoulizwa na MTANZANIA kuhusu uamuzi huo wa Bunge, Profesa Assad alisema hana taarifa yoyote kwa kuwa kwa sasa yuko likizo.

“Mimi sijui chochote, niko likizo kwa sasa. Hapa nilipo niko nje wala sijapata taarifa yoyote kuhusu hayo yanayoendelea,” alisema.

Alipoulizwa iwapo amefanikiwa kuona taarifa hiyo hata kwenye mitandao ya  jamii alijibu: “Sijui chochote. Wewe umepata taarifa ila mimi bado sijapata taarifa, niko nje. Nikipata taarifa itakuwa vizuri,” alisema.

Mdee asimamishwa mikutano viwili

 Katika ripoti hiyo pia, Bunge limepitisha azimio la kumsimamisha Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) mikutano miwili  baada ya kuunga  mkono kauli ya Profesa  Assad kuwa Bunge ni ‘dhaifu’.

Akiwasilisha taarifa ya kamati yake juu ya Mdee, Mwakasaka alisema kwa mipaka iliyoweka na ibara ya 30, Mdee alitumia uhuru wake kwa namna ambayo imeathiri haki na heshima ya bunge.

 “Hivyo kuathiri masilahi ya umma, kwa mantiki hiyo alikiuka masharti ya  katiba kwa kuingilia mhimili wa bunge,” alisema.

Alisema Kamati imezingatia maelezo ya shahidi alipokiri kutumia neno dhaifu kulieleza Bunge.

“Pamoja na ukweli huo shahidi hakuonyesha kujutia kabisa kitendo chake na kutoa kauli ambayo  inashusha hadhi ya Bunge.

 “Katika mazingira hayo kamati imejiridhisha kuwa shahidi alikuwa na nia ovu ya kulidharau na kulidhalilisha Bunge mbele ya umma wa Watanzania ambao wamekuwa wakiliamini Bunge na wawakilishi wao,”alisema.

 Mwakasaka alisema baada ya kuchambua ushahidi, kamati imeona shahidi amekiuka kifungu cha 26 (e) cha Sheria ya Kinga, Madaraka na Haki ya Bunge sura ya 296 kinachoeleza kwamba mtu yeyote atakuwa ametenda kosa endapo kwa makusudi atafanya kitendo cha kudharau shughuli za Bunge.

Alisema adhabu zinazotajwa kwa mujibu wa  kifungu hicho ni kumuonya na kumsimamisha mbunge husika kwa kipindi kinachoamriwa na Bunge.

 UTETEZI WA MDEE

Mwakasaka alisema katika maelezo yake, alitoa maana ya neno dhaifu kwa mujibu wa kamusi kuu ni hali ya kukosa nguvu, kimaumbele,  fedha,  uwezo na  utendaji.

“Katika mahojiano mbele ya kamati aliendelea kukiri kwamba alizungumza  na vyombo vya habari kuhusu Bunge na aliunga mkono kauli ya Profesa Assad aliyoitoa akiwa Marekani,”alisema.

 Alisema kutokana na ushahidi huo, Kamati inajiridhisha ni kweli mbunge huyo alitamka maneno hayo.

 Mwakasaka alisema katika kuufanyia kazi ushahidi huo, kamati ilifanya utafiti kwa kuangalia maana ya neno dhaifu katika Kamusi Kuu ya Kiswahili ambayo imeidhinishwa na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) na Baraza la Kiswahili la Taifa la Kenya (KICD).

 “Imetafsiri neno dhaifu ni isiyokuwa thabiti kiafya, nyonge, yenye kutokuwa na mashiko, goigoi, legevu, hafifu, isiyo imara, sahihi, thabiti, kiumbe kama vile mtu au mnyama asiye na nguvu , dhuli,” alisema Mwakasaka.

 MBOWE: Mtanaka kuwaziba Watanzania midomo

Akichangia taarifa ya Kamati ya Haki, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema taarifa hiyo inaonyesha azimio hilo lilishafanyiwa uamuzi na kuamua kutumia vifungu vya Katiba kutoa ushauri kwa Bunge.

“Kwa kuwa azimio hili  limeshafanyiwa uamuzi  sitazungumza,  nzungumza  kwa kifupi sana; historia ambayo mnaiandika leo, bunge mnalipa  upungufu, mnataka kuwaziba Watanzania midomo, watu wasiseme wakati sisi hapa bungeni  tunafanya uamuzi kwa niaba ya watanzania, mnataka tudhulumu haki za msingi za watu kwa sababu tuna mamlaka ya kufanya hivyo.

“Ibara ya 18 ya katiba ya nchi inasema, kila mtu ana uhuru wa kuwa na maoni, anayo haki ya kutafuta kupokea  na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi, anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.

“Katiba ni sheria mama, sheria ya kamati ya Bunge haiwezi kuvunja sheria mama, kifungu kilichomtia hatiani Profesa  Assad  kinavunja katiba ya nchi.

“Na katika siku za usoni  mnapounda kamati ya maadili kama tuna nia njema na nchi yetu, mwaangalie  ‘composition’ ya kamati za maadili, kwa sababu ‘composition’ ya kamati ya maadili leo haiwezi ikafanya ‘justice’ kwa vyama vya upinzani au kwa watu wanaoonekana pengine wanaikwaza Serikali,”alisema Mbowe.

Mbowe alitoa ushauri uangaliwe uwezekano kwa kufanya usawa  katika kamati kwa wajumbe wa kamati hiyo.

Alisema kuendelea kuweka wajumbe wengi kwenye kamati hiyo kutoka CCM, siyo jambo zuri.

 SALIM

Mbunge wa Chambani Yusuf  Salim (CUF) alimpongeza Profesa Assad kwa kusema ukweli na kutoisumbua kamati  ambako alidai kwamba  taaluma yake ndivyo inavyomtaka.

“Tunapokosolewa lazima tukubali kukosolewa, sisi ni binadamu hakuna aliyekamilika, kamati haijamtendea haki Profesa Assad.

“Kwani sisi ni nani hadi tusikosolewe, lazima tukubali kama ni udhaifu tunao kwa sababu sisi ni binadamu, tuangalie sasa udhaifu huu uko wapi na nini tufanye,”alisema Mbunge huyo.

KING

  Mbunge wa Jang’ombe Ally Hassan King (CCM) alisema maneno yaliyotumika siyo mazuri, na   Bunge jukumu lake ni kusimamia na kushauri Serikali huku CAG akiwa ni sehemu ya Bunge hivyo haiwezekani kwa yeye kusema bunge  ni dhaifu halafu aendelee kufanya kazi na watu dhaifu.

 MAGIGE

Mbunge wa Viti Maalum Catherine Magige (CCM), alisema Bunge siyo dhaifu huku akimshangaa Profesa Assad kwenda kulidhalilisha bunge nje ya nchi.

“Naunga mkono azimio la kamati maana pamoja na yote hayo tulisema labda CAG aliteleza, lakini hata alipoitwa na kamati ya bunge bado aliendeleza jeuri kwa kuendelea kuitumia lugha hiyo, hatupo tayari kuendelea kufanya naye kazi  maana alikuwa na muda hata wa kuomba msamaha lakini hakutaka kufanya hivyo,”alisema mbunge huyo.

 BILAKWATE

Mbunge wa Kyerwa, Innocent Bilakwate (CCM), alisema CAG alionyesha dharau lakini hakuonyesha kujutia kitendo kile.

“Yeye ni jicho la Bunge na serikali, ni mtu anayeaminika sana, nilikuwa najiuliza sana hivi jicho linaweza kumwambia mwili wewe hufai.

“Kitendo alichokionyesha ni cha dharau, kulidhalilisha Bunge na Serikali yetu, hakuonyesha uzalendo, hata katika mataifa mengine haijawahi kutokea kiongozi mkubwa akasimama na kuidhalilisha nchi yake,”alisema.

Lema akazia udhaifu, aingia matatani


Mbunge wa Arusha, Mjini Godbless Lema (Chadema), ametakiwa kuhojiwa  na  Kamati ya Haki  Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kuunga mkono kauli ya Mbunge wa Kawe,Halima Mdee (Chadema) Bunge ni dhaifu.

Naibu Spika Dk. Tulia alichukua uamuzi huo baada ya Lema kusema jana bungeni kuwa bunge ni dhaifu  wakati akichangia mjadala kuhusu ripoti ya mahojiano ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa

Mussa Assad na Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge.

“Kwa maneno  hayo uliyosema  na wewe unapelekwa kwenye kamati ya maadili  na ukae, hamna mchango tena. Sababu tunajadili adhabu kuhusu maneno hayo (ya CAG) nawe unasema, unathibitisha.

“Na wewe utaelekea kwenye kamati hiyo ukathibitishe vizuri kule, kwa hiyo kamati na huyu naye analetwa kwenu kwa utaratibu wa kawaida,”alisema Dk. Tulia.

Hata hivyo, wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wachache wa Chama cha Wananchi (CUF) waliamua kutoka nje kuonyesha namna walivyokasirishwa na hatua ya Dk. Tulia.

Akichangia mjadala huo, Lema alisema  Mbunge wa Kawe, Mdee  hakutendewa haki baada ya bunge hilo kutaka  asimamishwe kuhudhuria vikao viwili kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG.

Lema alisema alichokisema Mdee ni sahihi na anaungana naye kuwa Bunge ni dhaifu kama alivyosema Profesa Assad wakati wa mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa,   Marekani mwaka jana.

Wadu wazungumza

Kwa upande wake, CAG mstaafu, Ludovick Utoh alisema hayuko tayari kutoa maoni yoyote kwa sasa  kuhusu uamuzi huo wa Kamati ya Bunge.

“Kwa hilo la Kamati ya Bunge na yaliyotokea huko bungeni, kwa kweli siwezi kuzungumzia lolote kwa sasa, siko katika nafasi nzuri ya kutoa maoni yangu katika hilo,” alisema.

Jebra Kambole

Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea, Jebra Kambole alisema suala hilo ni la  sheria kwa sababu sheria ndiyo inayoweka majukumu ya CAG na ndiyo inayolitaka Bunge lifanye kazi na ofisi ya CAG, wala siyo suala la utashi wa Bunge.

Alisema ushirikiano wa Bunge na Ofisi ya CAG si hiari, ni maelekezo ya  sheria, kwa hiyo anashangaa Bunge linavyosema kwamba halifanyi kazi na ofisi ya CAG, akilitaka lieleze litawajibika vipi katika kuisimamia Serikali katika suala la taarifa zake za mapato na matumizi. 

“Watanzania tunahitaji maendeleo ambayo yanakuja kwa usimamizi mzuri wa rasilimali za umma. Bunge linatakiwa kuisimamia na kuiwajibisha Serikali kwa kudhibiti matumizi ya fedha za umma ambazo hesabu na matumizi yake yanachambuliwa katka ripoti ya CAG na si kwingineko.

“Kwa hatua hiyo Bunge limeamua kukiuka wajibu wake na kuamua kutowatendea haki Watanzania kwa kuamua kusimamia maslahi yao binafsi kwa utashi wao na kukwepa wajibu wake wa kuiwajibisha Serikali kupitia taarifa ya CAG, ambayo ndiyo inayoweka wazi matumizi ya mapato yote ya Serikali katika shughuli za maendeleo,” alisema.

ILIVYOKUWA

Januari 20 mwaka huu Profesa Assad alifika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge huku Kamati hiyo ikitumia zaidi ya saa tatu kumhoji.

Kuhojiwa huko kulikuja  kufuatia wito wa Spika Job Ndugai alioutoa Januari 7 mwaka huu  kumtaka kufika kwenye kamati hiyo kutokana na kauli yake ya kuliita bunge ni dhaifu vinginevyo angepelekwa akiwa amefungwa pingu.

  Profesa Assad alipokuwa akihojiwa na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na Mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Arnold Kayanda, alimuuliza CAG kuwa ofisi yake imekuwa ikijitahidi kila mwaka kufanya ukaguzi na kutoa ripoti zenye kuonyesha kuna ubadhirifu lakini baada ya hapo wananchi hawaoni kinachoendelea.

CAG alijibu: “Hilo ni jambo ambalo kimsingi ni kazi ya Bunge. Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.

“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”

“Sitaki kuwa labda nasema hili kwa sababu linahusisha watu fulani, lakini ninachotaka kusema ni kuwa Bunge likifanya kazi yake vizuri, hata huu udhaifu unaoonekana utapungua,”alisema.

Maagizo hayo ya Spika yaliibua sintofahamu katika mitandao ya  amii huku wasomi na watu wa kada mbalimbali wakiwamo wabunge wakionyesha kupinga msimamo huo wa Spika.

Walioonyesha kupinga hadharani alikuwamo Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe(ACT Wazalendo), ambaye alifungua kesi katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es salaam  kuzuia Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) asihojiwe na Bunge.

Lakini Mahakama Kuu Tanzania ilikataa kuipokea kesi hiyo na kuisajili  huku ikieleza kuwa ilikuwa na kasoro za  sheria kutokana na hati za viapo vya wadai wanne pamoja na hati ya wito wa Spika Ndugai na hati ya kiapo cha CAG kutokuambatanishwa kwenye hati ya maombi.

Katika kesi hiyo Zitto na wenzake walikuwa wanaiomba Mahakama itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kwa katiba na pia kutoa tafsiri ya sheria ya haki, kinga na madaraka ya bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau bunge.

Januari 17 mwaka huu, Profesa Assad aliibuka na kukubali  wito wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge , kama alivyotakiwa na Spika wa Bunge Ndugai.

Pia alinukuliwa na vyombo vya habari akidai kwamba   majibu yake katika mahojiano yaliyozua mjadala hayakuwa na nia ya kulidhalilisha bunge.

Mkaguzi huyo alisema  neno udhaifu ni la kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya utendaji wa mifumo ya taasisi mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles