27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BUFFON: MSIMU UJAO NITASTAAFU SOKA

 TURIN, ITALIA


MLINDA mlango namba moja wa klabu ya Juventus na timu ya Taifa ya Italia, Gianluigi Buffon, amesisitiza kuwa msimu ujao lazima astaafu soka, hata kama klabu yake itafanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 39, amedai anaweza kutangaza kustaafu soka mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi.

Kipa huyo amekuwa kwenye kikosi cha Juventus kwa miaka 17, hivyo amedai umri wake umekuwa mkubwa na ni wakati wa kuwapisha wengine waoneshe uwezo wao na kuisaidia timu hiyo.

“Ninaamini msimu mpya wa Ligi utakuwa wa mwisho kwangu katika maisha ya soka, nimeona bora niweka sawa jambo hilo, nataka nijaribu kufurahia maisha nje ya soka, ni maamuzi magumu, lakini huo utakuwa wakati wake.

“Nitahakikisha ninaondoka kwenye soka huku nikiwa nimewaachia Juventus jambo muhimu katika maisha yao, najua nimefanya makubwa, lakini ni vizuri kufanya makubwa zaidi katika kipindi changu cha mwisho,” alisema Buffon.

Kipa huyo mzoefu amefanikiwa kutwaa mataji nane ya Ligi Kuu nchini Italia, Kombe la Dunia mwaka 2006, lakini hadi sasa hajafanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya katika maisha yake, lakini amesema atastaafu tu hata kama atashindwa kulitwaa taji hilo kwa kuwa muda wake umefika.

“Kukosa taji la Ligi ya Mabingwa ni jambo la kawaida na nadhani haikuwa bahati yangu, lakini muda wa kustaafu umefika na siwezi kujisikia vibaya kwa kuwa soka ndivyo lilivyo, nimeweza kutwaa mataji makubwa mbalimbali.

“Kila mmoja anatamani kutwaa taji hilo la Ligi ya Mabingwa, kwa kuwa ni taji la aina yake na lina hisia tofauti, sawa na kukutana na mchezaji ambaye ulikuwa unatamani kuwa naye pamoja na unakutana kwenye mazingira ambayo hukuyatarajia.

“Nimekuwa nikilipigania kwa kipindi kirefu, kipindi chote hicho naweza kusema Juventus hatukuwa na bahati hiyo na siyo mimi peke yangu, ila wapo ambao wamekuwa na bahati na taji hilo katika kipindi chao cha soka, wanaweza kuhama timu na kujikuta wakifika na mafanikio ya taji hilo,” aliongeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles