25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

BOTSWANA NA NUSU KARNE YA ‘MIUJIZA’ YA MAFANIKIO YALIYO HATARINI

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


BOTSWANA  ilikuwa moja ya mataifa maskini zaidi duniani wakati ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1966.

Taifa hilo lisilo na bahari lilikuwa na wahitimu 22 tu wa vyuo na kilomita 12 za barabara za lami.

Lakini kutokana na akili nyingi za mwasisi wa Taifa hili la Kusini mwa Afrika kama tutakavyoona baadaye likapaa kwa kasi kupata ukuaji mkubwa wa uchumi kuliko mataifa mengi si tu barani Afrika bali pia duniani.

Kwa sababu ya mafanikio haya makubwa, wataalamu wa siasa ya uchumi wakaiita Botswana “simulizi ya mafanikio Afrika.”

Hata hivyo, likiwa na chama kile kile cha siasa cha tangu uhuru, kuna ongezeko la wasiwasi kuhusu kudidimia kwa uhuru na utawala bora.

Wakati wa kuelekea Uchaguzi M kuu wa mwaka 2014, mwanasayansi wa siasa wa Botswana Amy Poteete aliashiria uwapo wa pengo baina ya sifa inayomwagiwa Botswana na uhalisia.

Ukuaji wa uchumi ulikuwa ukipungua, kulikuwa na hali ya wasiwasi katika miungano ya sekta za umma na raia walikuwa wakikabiliwa na ukosefu wa maji na umeme kukatika mara kwa mara.

Wakati uchaguzi mkuu ulipokaribia, wanasiasa wa upinzani na waandishi wa habari walidai kuandamwa mikononi mwa mawakala wa Serikali na wanachama wa Chama tawala cha Botswana Democratic (BDP).

Ijapokuwa uungwaji mkono wa BDP katika uchaguzi wa 2014 ulipungua, chama hicho kiliweza kujilimbikizia nguvu.

Pamoja na kupata asilimia 46.7 ya kura kuonesha kupungua kwa umaarufu, shukrani zikiuendea mfumo wa uchaguzi BDP iliweza kupata viti 37 kati ya 57 vya ubunge sawa na asilimia 64.9 ya viti vyote.

Kwa msingi huo, uchaguzi wa 2014 uliashiria kitu kimoja; Kuchokwa kwa BDP na hivyo kupungua kwa umaarufu wake na haitakuwa ajabu katika siku za usoni kikapotea.

Lakini pia kutokana na matukio yaliyouzingira Uchaguzi Mkuu wa 2014, wakosoaji wanamtuhumu Rais Khama kwa kujikita zaidi kwenye uimla.

Wakati Botswana ikiendelea kuzitimulia vumbi nchi nyingi za  Afrika kiuchumi, wastani wake wa alama zinazopimwa na vigezo vya utawala bora wa Asasi ya Mo Ibrahim Foundation, Botswana imekuwa daima ikipata alama za juu katika utawala bora.

Mbali ya hiyo Taifa hilo lina utamaduni imara wa kidemokrasia tangu uhuru na inashika nafasi ya pili kwa viashiria vya maendeleo ya binadamu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika.

Kadhalika linahesabiwa kuwa moja ya mataifa yasiyo na vitendo vya rushwa na ufisadi duniani.

Lakini namna gani wananchi wa Botswana wanaipima Serikali yao? Tuangalie ripoti za Afrobarometer — mtandao unaoongoza kwa utafiti barani Afrika, ambao moja ya ripoti zake za karibuni ilipima mtazamo wa umma kuhusu demokrasia.

Ripoti ilijaribu kutazama mlolongo wa tafiti zilizofanyika kati ya mwaka 1999 na nusu ya kwanza ya mwongo huu.

Wananchi waliohojiwa waliripotiwa wakisema Taifa lao lina demokrasia kamili au demokrasia lakini yenye matatizo kidogo. Tangu upimaji huo uanze Botswana haikuwahi kushuka chini ya alama 59.

Hilo linatosha kutuambia namna raia wa Botswana wanavyoridhishwa na mwenendo wa demokrasia ya Taifa lao, bila kujali kuhodhiwa kwa siasa na kundi la watu wachache tu ndani ya chama tawala.

Hata hivyo, chambuzi zinaonesha kwamba imekuwa alama zimekuwa baada ya mwaka 2008, wakati Rais Khama, alipoingia madarakani.

Pia kilichopungua tangu mwaka huo ni imani ya waliohojiwa namna walivyo huru kuzungumza mitazamo yao.

Wakati asilimia  83 ya raia wa Botswana walijihisi kuwa wako huru kikamilifu mwaka 2008, idadi hiyo ilishuka hadi asilimia 65 mwaka 2014.

Botswana inahesabiwa kama demokrasia kongwe barani Afrika, ambayo baada ya uhuru haikupiga marufuku siasa za vyama vingi kama yalivyofanya mataifa mengine kama vile Tanzania na Kenya, ambayo, hata hivyo yalizirejesha siasa hizo katika miaka ya 1990 kufuatia upepo wa mabadiliko ulioikumba dunia.

Raia wake wamekuwa wakifurahia miongo mingi ya utulivu wa kisiasa na ushindani wa vyama vingi— hata kama ni chama kile kile kinachoongoza Taifa kuanzia Ikulu hadi Bunge kwa miaka yote hiyo.

Hata hivyo, iwapo mwenendo unaotia wasiwasi wafuatiliaji wa Taifa hilo utaendelea kuna uwezekano wa kuweka rehani mafaniko yake iliyotengeneza katika miaka zaidi ya 51 ya uhuru. Taifa hili litasherehekea miaka 52 ya uhuru Septemba 30 mwaka huu.

Taifa hilo kwa sasa limepitwa na mataifa mengi barani Afrika kama vile Ghana linapokuja ushindani wa demokrasia ya vyama vingi.

Sambamba na hilo la kisiasa Taifa hili linaelekea hatarini kupoteza mafanikio yake ya kiuchumi.

“Hata bila mdororo wa uchumi duniani, tutaweza kuishi na kuzipita nyakati ngumu zenye changamoto kwa namna ile ile ambayo tunaanza kuondokana na utegemezi wa mapato yatokanayo na madini ya almasi,” ni kauli ya Rais wa Botswana, Ian Khama katika moja ya hotuba zake kwa Taifa.

“Utegemezi katika kitu chochote kamwe hauleti afya,” aliongeza Khama.

Rais Khama hakukosea kwani  rasilimali ya almasi ya Botswana, ambayo inachangia karibu nusu ya mapato ya Serikali na asilimia 80 ya mauzo ya nje ya nchi hiyo, inatarajia kutoweka ndani ya kipindi cha miaka 20 ijayo.

Hilo linalotarajia kutokea Botswana linatukumbushia mgodi wetu hapa Tanzania wa almasi wa Mwadui, mkoani Shinyanga, huwezi kusema kama umelinufaisha Taifa ipasavyo.

Licha ya matatizo ya hapa na pale Botswana, kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Ujasusi Marekani (CIA) mwaka 2013 lina pato kwa ndani kwa kila kichwa la dola 16,400, likiyapiku mataifa kama Mexico na Uturuki.

Kipindi hicho kwa mujibu wa CIA, pato hilo kwa kila mwananchi nchini Tanzania lilikuwa dola 1,700.

Kwa maana hiyo Botswana imeweza kutumia vyema rasilimali zake na hivyo mawe hayo ya thamani yameweza kuinufaisha kwa kiasi kikubwa.

Lakini pia bado linakabiliwa na changamoto baada ya ustawi wa miaka mingi.

Madini ya almasi yaliyolifanya Taifa hilo kuwa la kipato cha kati duniani, kwa sasa yamebakiwa na muda mchache kabla hayajatoweka.

Namu, si kipindi kirefu, ni umri wa kijana wa sekondari kwa mfumo wetu wa elimu, japokuwa kwa mifumo ya mataifa mengine huo ni umri wa kijana aliyeko mwaka wa pili au wa tatu chuo kikuu.

Akiba ya almasi ya Botswana iligunduliwa muda mfupi baada ya kupata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1966, wakati ambao kama tulivyoona ilikuwa moja ya mataifa maskini kabisa duniani.

Taifa hilo ambalo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012, lina watu 2,003,910, na idadi ndogo mno ya mtawanyiko wa watu kwa kila kilomita za mraba (population density).

Ina wastani wa watu watatu kwa kila kilomita ya mraba na hivyo kushika nafasi ya saba duniani kwa kiwango kidogo cha msongamano wa watu.

Kwa kiasi kikubwa hali hiyo inachangiwa na sehemu kubwa ya Taifa hilo la Kusini mwa Afrika kuwa jangwa lisilokaliwa na watu.

Ili kuchimba rasilimali hiyo mpya kipindi hicho, aliyekuwa Rais Seretse Khama, baba wa Ian, aliingia mkataba muhimu na wenye akili na kampuni kubwa ya madini ya Afrika Kusini, De Beers.

Chini ya makubaliano hayo, uchimbaji madini ulipaswa kuwa mradi wa pamoja kwa asilimia 50 kwa asilimia 50 baina ya  Serikali na De Beers.

Aina ya mkataba huo, moja ya mikataba mizuri na nadra kufanyika barani Afrika ambako viongozi wake wanajulikana kwa kuingia mikataba mibovu isiyo na manufaa kwa Taifa husika zaidi ya kuwanufaisha wao na mabwana zao hao.

Mkataba huo uliiruhusu nchi inufaike moja kwa moja na mapato ya almasi badala ya kutegemea kodi kama ilivyo kwa mataifa mengi.

Utaratibu huo wa kutegemea kodi, mirahaba midogo na huduma nyingine ndogo ndogo za kijamii kutoka kampuni wekezi za kigeni, haiwezi kuchangia pato la Taifa kwa namna inavyotakiwa wala kufidia athari za kimazingira zinazoachwa wakati madini yanapokauka.

Ubia  baina ya Botswana na De Beers unaongoza duniani kwa uzalishaji wa madini linapokuja suala la ukubwa wa thamani.

Botswana kwa sasa inahusika na zaidi ya moja ya tano ya uzalishaji wa almasi duniani na ni mzalishaji anayeongoza kwa madini ya almasi yenye ubora wa juu duniani.

Mawe hayo ya thamani yakijumuisha na utulivu wa kisiasa nchini humo, yaliliruhusu Pato la Ndani (GDP) la Botswana lipae kwa kasi kubwa kutoka Dola za Marekani 70 mwaka 1966 hadi dola 8,332 mwaka huu kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF).

Wakati GDP hiyo ikiwa ni ya nne kwa ukubwa barani Afrika, kipimo kinachotumika kulinganisha uchumi na mataifa mengine PPT (purchasing power parity) ni dola 16,758 kwa kichwa mwaka huu.

Kipato na akiba ya fedha za kigeni zilizopatikana kwa mauzo ya almasi nje pia yaliiwezesha nchi hiyo ijitegemee kwa sera zake za uchumi bila utegemezi wa mashirika ya kimataifa kama vile IMF.

Mbali ya mwendelezo wa utulivu wa kisiasa na kuimarika kwa viashiria vya maendeleo ya binadamu, kabla ya kuibuka kwa janga la Ukimwi, wadadisi wengi wa uchumi wanaieleza Botswana kama ‘muujiza wa Afrika.

Mahali ilipofikia kiuchumi panatia moyo mno. Lakini kama ambavyo Ian Khama na wengine wengi wanavyosisitiza, Botswana imeendelea kuwekeza utegemezi wake kwa kiasi kikubwa kwa almasi kwa kiwango cha hatari.

Pamoja na ukuaji wa baadhi ya sekta kama vile benki na utalii, almasi bado ni muhimu kwa uchumi wa Botswana. Hali hii ni tishio si tu kwa sababu akiba zimetabiriwa kutoweka katika kipindi cha miongo miwili, bali pia kwa sababu inaacha sehemu kuu ya uchumi wa Botswana ‘uchi’

Ili kukabiliana na changamoto hizo Botswana imeangalia njia mbadala si tu za kukabiliana na bei isiyotabirika ya almasi na hatari ya kutoweka kwa madini hayo, bali pia kujikita zaidi katika sekta nyingine.

Sekta zinazotupiwa jicho ni pamoja na utengenezaji bidhaa, ukandarasi na huduma.

Sekta ya kifedha pia imeshuhudia ukuaji huo hasa Benki ya Botswana na Umoja wa Forodha Kusini mwa Afrika (SACU), ambayo imesababisha ongezeko la ajira mijini.

Njia nyingine ni kuachana na uuzaji wa almasi ghafi ili kuzisindika nchini humo.

badala ya kuuza almasi ghasi, kuzisindika nchini Botswana na moja ya hatua zilizochukuliwa katika miaka ya karibuni ni kitendo cha De Beers kukubali kuhamisha operesheni ya usindikaji kutoka London hadi Mji Mkuu wa Botswana, Gaborone.

Hilo linaweza kusaidia pia kuchochea ukuaji wa sekta ya utengenezaji na ajira nchini humo na kunusuru mafanikio iliyopitia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles