22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

BoT: Tumefunga maduka 30 ya kubadili fedha

Na WAANDISHI WETU-ARUSHA


ZAIDI ya maduka 30 ya fedha za kigeni jijini Arusha yamefungwa kutokana na kudaiwa kuendesha biashara haramu ya fedha za kigeni na kukiuka sheria ya uendeshaji wa biashara hiyo.

Hatua hiyo inatokana na operesheni ya kushtukiza iliyofanyika juzi chini ya uratibu wa Benki Kuu ya Tanzana (BoT).

Katika operesheni hiyo, baadhi ya maduka yalibainika kufanya biashara hiyo bubu bila kuwa na leseni kwa mujibu wa sheria.

Operesheni hiyo ilifanyika baada ya uchunguzi kubaini ongezeko la biashara za kubadilisha fedha kinyume na sheria na kukua kwa biashara haramu ya fedha za kigeni na utakatishaji fedha haramu kupitia maduka hayo.

Akizungumza na wanahabari jana jijini hapa, Gavana wa BoT, Professa Florens Luoga, alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa kushtukiza baada ya uchunguzi wa miezi sita kwa maduka hayo.

Alisema ukimya na usiri mkubwa ulitokana na awali kusambaa kwa taarifa kila walipokuwa wakitaka kutekeleza operesheni hiyo iliyofayika mara mbili bila kuzaa matunda.

Kutofanikiwa huko kulitokana na kuwapo kwa mtandao mpana wa kuhakikisha shughuli za udhibiti hazifanikiwi kila walipokuwa wakipanga.

“Baada ya mashauriano na wataalamu na kushirikisha vyombo vya upelelezi na usimamizi, ilionekana ili kufanikisha kazi iliyokusudiwa ni muhimu wahusika wote wadhibitiwe kwa wakati mmoja na kufanyiwa ukaguzi,” alisema Profesa Luoga.

 

KUTUMIA JWTZ

Akizungumzia kuhusu kutumia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika operesheni hiyo, Profesa Luoga alisema walilazimika kufanya hivyo kutokana na polisi wengi kusimamia usalama katika mitihani ya kidato cha pili inayoendelea.

“Hii ilihitaji ushiriki wa maofisa wengi sana kutoka vyombo mbalimbali na kuhakikisha kila mahali ambako ukaguzi uliendeshwa kuna usalama wa kutosha na wananchi wanaarifiwa kutokuingia sehemu husika kwa wakati huo.

“Zoezi hili lilihitaji watu zaidi ya 100, kwa sababu tulihitaji kuwafikia wote kwa wakati mmoja, baadhi ya askari wa JWTZ wakiwa katika sare zao bila silaha walishiriki zoezi hili, kwa sababu siku hiyo askari polisi wengi wapo kwenye kusimamia usalama katika vituo vya mitihani ya kidato cha pili inayoendelea,” alisema.

 

HATUA ZITAKAZOCHUKULIWA

Profesa Luoga alisema operesheni hiyo imemalizika salama bila kuathiri mtu yeyote na taratibu za kisheria zinaendelea, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wahusika na watakaokutwa na tuhuma za ukiukwaji wa sheria watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Hatua zinazochukuliwa na BoT kuzuia kuendelea kwa ukiukwaji wa sheria na kudhibiti uendeshaji wa biashara ya ubadilishaji fedha, ni pamoja na kusitisha utoaji wa leseni za biashara ya ubadilishaji fedha.

“Kwa takribani miezi mitatu BoT imesitisha utoaji wa leseni za biashara ya ubadilishaji fedha, maombi yote yamesitishwa na maombi mapya hayatapokewa hadi taratibu mpya za uendeshaji wa biashara hiyo zitakapokuwa tayari,” alisema.

Alisema kwa wale watakaopatikana na makosa ya uvunjaji wa sheria, leseni zao zitafutwa na hawataruhusiwa kufanya biashara hiyo tena.

“Katika kipindi hiki wakati kesi zao zinashughulikiwa kisheria ili kuzuia kuendelea kwa biashara haramu, leseni zao zitasitishwa na wanatakiwa kuzirudisha Benki Kuu hadi kesi zao zitakapokamilika na baada ya hapo taratibu mpya zitatumika,” alisema.

Kuhusu waliopatikana na tuhuma za ukiukwaji wa sheria katika operesheni mbili zilizopita na kufikishwa Polisi, alisema wanatakiwa kurejesha leseni zao Benki Kuu na leseni hizo zitasitishwa hadi kesi zao zitakapokamilika.

Aliongeza kuwa uchunguzi uliofanyika umebaini waendeshaji wengi wa maduka hayo hawakukidhi vigezo vyote japokuwa leseni zilitolewa kwao baada ya taarifa kupotoshwa.

“Hao wote watapewa notisi ya kusitisha leseni na maduka yao kufungwa, hivyo yeyote ambaye anajua kuwa upatikanaji wa leseni yake una dosari, anashauriwa kuirejesha leseni hiyo kwa hiari.

“Wale  ambao wanaendesha maduka ya kubadilisha fedha bila leseni au kwa kutumia leseni zisizo zao, wanatakiwa kufunga maduka hayo mara moja kabla hawajafikiwa na mkono wa sheria,” alisema.

Alidai kuwa ili kuzuia watu wasiostahili kupenyeza na kujipatia leseni za biashara ya ubadilishaji fedha, Benki Kuu imefanya mabadiliko ya ndani na inakamilisha taratibu mpya kuhusu uendeshaji wa biashara hiyo na taarifa zitatolewa baadaye.

 

UWEPO WA FEDHA ZA KUTOSHA

Profesa Luoga alikanusha madai kuwa operesheni hiyo imefanyika kwa sababu ya kutokuwepo kwa akiba ya kutosha ya fedha za kigeni.

Alisema BoT ina hifadhi ya kutosha ya fedha za kigeni ambazo zinaweza kuendesha nchi ikiwa ni pamoja na kulipa madeni ya Serikali kwa kipindi cha miezi mitano mfululizo.

“Zoezi hili kuhusishwa na kutokuwepo kwa fedha za kigeni nchini siyo kweli, BoT ina hifadhi ya fedha za kigeni za kutosha na Tanzania ina hifadhi ya fedha za kigeni kuliko nchi yoyote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo hakuna wasiwasi juu ya hili,” alisema Profesa Luoga

Katika hatua nyingine, baada ya kusoma taarifa yake, Profesa Luoga aligoma kuulizwa maswali na wanahabari.

HABARI HII IMEANDALIWA NA JANETH MUSHI, ABRAHAM GWANDU NA ELIYA MBONEA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles