25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

BOSI JAMII FORUMS ASOMEWA MASHTAKA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo (kulia), akitoka katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana baada kusomewa mashtaka matatu tofauti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Maxence Melo (kulia), akitoka katika chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana baada kusomewa mashtaka matatu tofauti.

MANENO SELANYIKA Na BRIGHITER MASAKI (TSJ)

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Jamii Media Limited, Mexence Melo, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashtaka manne katika kesi tatu tofauti.

Melo alipandishwa mahakamani hapo Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti kisha kusomewa mashtaka yanayomkabili kwa mahakimu watatu wa mahakama hiyo na kati ya hayo moja ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kusababisha kupelekwa rumande katika Gereza la Keko hadi Jumatatu.

Katika shtaka la kwanza lililosomwa kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, upande wa Jamhuri ulikuwa unasimamiwa na Mohamed Salum, wakati ule wa utetezi ukiongozwa na Wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole.

Wakili Salum alidai kwamba kati ya Aprili mosi na Desemba 13, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Melo akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo inayoendesha mtandao maarufu wa Jamii Forums, alishindwa kutoa taarifa za kiuchunguzi za makosa ya mtandao kwa maofisa wa Jeshi la Polisi nchini kupitia mtandao wake.

Pia anakabiliwa na kesi nyingine namba 458 ambapo alipandishwa tena kizimbani na kusomewa mashtaka mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Kisutu, Victoria Nongwa.

Wakili wa Serikali, Salum alidai kwamba mtuhumiwa anakabiliwa na kosa la kumiliki na kutoa huduma katika mtandao wa kijamii bila kuwa na kibali kitu ambacho ni kinyume cha sheria na taratibu za mitandao nchini.

Salum alidai kuwa kati ya Desemba 9, 2011 na Desemba 13, mwaka huu huko Mikocheni akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alikuwa anamiliki mtandao huo kinyume cha sheria kwa sababu hakusajili katika tovuti ya Tanzania.tz.

Katika shtaka la pili katika kesi hiyo, Melo, anadaiwa kati ya Januari 26 na Desemba 13, mwaka huu huko Mikocheni akiwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, alishindwa kutoa taarifa ili kukamilisha upelelezi wa Jeshi la Polisi.

Kesi namba 457 iliyokuwa kwa Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa, Wakili Salum alidai kwamba mtuhumiwa anakabiliwa na kosa la kuzuia upelelezi.

Katika maelezo ya kosa hilo, Wakili Salum alidai kwamba tukio hilo lilitokea kati ya Mei 10 na Desemba 13, mwaka huu katika ofisi za Jamii Forums zilizopo huko Mikocheni, Dar es Salaam.

“Mtuhumiwa unatuhumiwa kwamba ukiwa unafahamu kuwa Jeshi la Polisi linafanya upelelezi wa makosa ya mitandao mbalimbali ya kijamii kwa makusudi ulizuia uchunguzi katika ofisi yako,” alidai Wakili Salum.

Baada ya kusomewa maelezo hayo mtuhumiwa alikana kutenda makosa yanayomkabili na upelelezi bado unaendelea ambapo kesi iliyokuwa kwa Hakimu Mwambapa mtuhumiwa alishindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyokuwa yanamtaka kuwa na wadhamini wawili watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni tano kwa kila mmoja na kwamba hakutakiwa kutoka nje ya Jiji la Dar es Salaam bila kibali lakini alikosa dhamana.

Kambole ambaye ni wakili wa utetezi, aliomba mahakama hiyo impatie mteja wake masharti nafuu.

Katika mashtaka mengine, mtuhumiwa alifanikiwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa na mahakimu ambapo walimtaka awe na wadhamini wawili wenye barua na watakaoweka saini ya maandishi ya Sh milioni 10 kwa kila mmoja.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles