23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

BORA TUPATE AKINA MAKONDA WENGI KULIKO…

Polisi akiwaondoa wafanyabiashara ndogondogo katika barabara ya Nyerere, jijini Mwanza.
Polisi akiwaondoa wafanyabiashara ndogondogo katika barabara ya Nyerere, jijini Mwanza.

NA INNOCENT NGANYAGWA,

JUMA lililopita niliandika kuhusu ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kusikiliza changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili wakazi wa jiji hilo.

Katika ziara hiyo alitatua baadhi ya changamoto papo kwa hapo na nyingine zinazohitaji mchakato kuahidi kuzishughulikia.

Inawezekana siku kumi alizotenga kuzungukia maeneo ya jiji hilo hazikutosha kuwafikia wote, lakini ziliibua kitu cha kujifunza kutokana na mwitikio wa wananchi na yaliyojiri baada ya hapo, Makonda alirudi ofisini kuendelea na majukumu yake mengine ya kiofisi.

 Sifanyi mwendelezo wa mada ya juma lililopita, lakini katika mambo kumi niliyobainisha, la tisa lilikuwa hivi kama ninavyojinukuu: “Kama kiongozi akitumia muda wake kushughulikia yaliyomweka uongozini ili kuwatumikia wananchi anakuwa ametimiza wajibu”, kwa muktadha wa mada ya juma lililopita sentensi hiyo ilikuwa ndefu zaidi ya nilivyoiandika.

Kinachotafakariwa katika tafakuri yangu ya leo ni yale niliyowahi kuyabainisha siku nyingi zilizopita, kwamba katika awamu hii ya tano ya utawala wenye kipaumbele cha kutumbua majipu bila ganzi, mtumbuaji mkuu amezungukwa na watumbuaji wasaidizi ambao hawazingatii weledi wa kitaaluma katika kutumbua, bali kutaka kuonekana wanatimiza wajibu unaotarajiwa na mkuu wao, wakifanya kazi kwa nidhamu ya woga badala ya kujikita katika misingi ya walichokasimiwa.

Kilichotokea Mwanza hivi karibuni na kukemewa na Rais John Magufuli ni udhihirisho tosha kwamba, majukumu yanatimizwa kwa kutafuta sifa badala ya kuzingatia uhalisia, kwamba viongozi wa sasa waliopewa madaraka ambao bila kutumbua na kuonyesha hulka ya mabavu wanakereketwa na kuhisi hawajakamilika katika nafasi zao na pengine hata taarifa zao hazitasikika na utekelezaji wa majukumu yao utaonekana dumavu.

Kwa makusudi kabisa wameamua kufanya  kazi kwa mtindo wa maigizo wakidhani kuwa hicho wanachokifanya ndicho bwana mkubwa anapendezwa nacho.

 Uongozi wa Mkoa wa Mwanza chini ya John Mongela una waliokasimiwa mamlaka katika nafasi mbalimbali, kwa yaliyofanyika nilitamani sana kuona Rais Magufuli akitumbua waliotumbua chunusi badala ya majipu, maana walichokifanya kwa kutumia vyombo vya dola inadhihirisha kuwa ama ni wavivu wa kufikiri au hawana kabisa uwezo huo wa kufikiri, pengine wanawaza, kwani kuna tofauti ya kimsingi baina ya kuwaza na kufikiri,  kuwaza ni kutopea kwenye  matamanio yasiyo na mkakati na kufikiri ni mchakato wa kimkakati.

Kwa kufurumusha walalahoi na kusikia fahari kuvunja na kuharibu rasilimali na mitaji ya wamachinga, inaelekea wote waliosimamia zoezi hilo walikengeuka, hawastahili kusimamia majukumu ya uongozi, huenda wanaweza kusimamia mambo yao binafsi.

Tafakuri yangu ilibaini mambo matatu kutokana na katazo la kuwanyanyasa wamachinga, wachimbaji wadogo na wengine wa kada hizo lililotolewa na Rais Magufuli: Kwanza, amewapa nafasi ya pili watumbuaji wake wasaidizi kujirekebisha, vinginevyo angeweza kuwatumbua bila kusita. Pili; ikaisukumia tafakuri yangu kwa Nabii wa kisiasa wa taifa hili, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

 Aliwahi kusema katika moja ya hotuba zake kuhusu viongozi wasioweza kusimamia majukumu yao, akitolea mfano kuwa mtu wa aina hiyo aende akaendeshe shughuli zake binafsi hata kama ni shamba lake. Jambo la tatu nililotafakari ni kuhusu ziara ya Makonda, ambayo kwa macho ya wengine ilionekana haina mashiko, lakini najiuliza hivi, kama Mkuu wa Mkoa wa Mwanza naye angefanya ziara kama ile na kuongea na wananchi wake si angeshafahamu kero za wamachinga wanaolazimishwa kuhamia pembezoni ambako hakuna miundombinu wala wateja wa bidhaa zao? Napata jibu moja kuwa, pengine tunahitaji akina ‘Makonda’ wengine katika maeneo mengine ya mikoani hapa nchini, ili watimize usimamizi wa majukumu yao kwa kuzingatia mamlaka na nafasi za kiweledi walizokasimiwa.

Ningepata nafasi ya kukutana na Rais Magufuli kuhusiana na hatua ya tamko alilolitoa kwa kilichotokea Mwanza na kuelekeza watendaji wa Tamisemi kushughulikia, ningemwambia kuwa jiji hilo mara kadhaa huwa na viongozi na wasimamizi wenye hulka ya ‘umungu-mtu’, hata viongozi wasimamizi kwenye vyombo vya dola, likiwamo Jeshi la Polisi lililolinda si usalama bali ni kama lilikuwa likilinda uamuzi kandamizi, nalo huwa lina hulka ya kujihisi kana kwamba nguvu zote za mabavu wanazo wao na kujigubika utopevu wa uzanduzandu wa ‘utapia-weledi’.

 Jambo la pili ambalo ningemwambia ni kwamba, pengine aliowateua wanaofanya mambo kinyume wanapaswa si kupewa semina elekezi, bali ‘semina tumbuzi’ kwamba mtoa mada wa semina atawadhihirishia kuwa, kwenda kinyume cha misingi ya kilichowaweka kwenye nafasi walizopo kutawasababishia kutumbuliwa kavukavu bila ganzi, pengine wangeogopa, maana walichokifanya ni kusababisha kihoro cha hofu inayoharibu juhudi za walalahoi za utafutaji maisha kwa kuwakimbiza kama digidigi.

Tafakuri yangu inapata picha kuwa, pengine wasaidizi wengi wa Rais Magufuli hawamwelewi, bali wanamwogopa, wakikurupuka kujikubalisha.

Kwa muktadha huo wateule hao wanafanya mambo bila kujipima wala kupambanua athari wa maamuzi wanayoyatoa katika utekelezaji wa dhima waliyopewa.

Bila shaka uamuzi wa Rais kuhusu wamachinga hasusani jijini Mwanza unaweza kuwa ni sehemu ya kuwafikishia ujumbe viongozi wengine wenye hulka kama za viongozi wa jiji hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles