24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BOMOABOMOA YAGUSA NYUMBA ZA IBADA

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SIKU moja baada ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kutangaza kuanza kuvunja nyumba 24 za ibada pembezoni mwa Barabara ya Morogoro, baadhi ya nyumba hizo zimeanza kuvunjwa huku wengine wakikataa kuvunja au kuhamisha chochote.

Jana, MTANZANIA lilitembelea baadhi ya maeneo ya barabara hiyo na kushuhudia makanisa matatu yakiwa yamekwisha kuvunjwa kabla ya taarifa ya juzi huku Kanisa la Mtakatifu Peter Claver Parokia ya Mbezi Louis likiendelea kuvunjwa.

Akizungumza na MTANZANIA, mmoja wa watu walioshiriki uvunjaji huo ambaye   pia ni muumini wa Kanisa la Mtakatifu Peter Claver Parokia ya Mbezi Louis, Mathew Zakayo, alisema wameamua kuvunja wenyewe kunusuru matofali na mbao waweze kuyatumia katika ujenzi sehemu nyingine.

“Kwa sababu hii ni amri imetolewa, huwezi kupingana na Serikali kwa sababu  ndiyo yenye mamlaka,” alisema Zakayo.

Baadhi ya makanisa yaliyokuwa tayari yamevunjwa ni pamoja na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba ambalo liliondolewa wakfu na Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, Agosti 6 mwaka huu.

Mengine ni Kanisa la Evangelical Assemblies of God lililo karibu na Kanisa la KKKT Kibamba na Kanisa la EAGT Mbezi kwa Yusuf.

Makanisa mengine yanayotarajiwa kubomolewa ni Parokia ya Kiluvya, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, The River Hilling Ministry of Tanzania la Kibamba, Anglikana Stop Over na Calvary Salvation Church lililopo Kibamba.

Vilevile kuna KKKT Usharika wa Mbezi Luis, Kaprenan lililopo Kibamba, TAG – Suka, Pentekoste Of Tanzania Kiluvya, Nayoth Church Kiluvya, KLPT la Bwawani, Kapernan Centre Mbezi, TAG Carvary Tample Mbezi Inn, GRC Mbezi Inn, TAG Rejoice Centre Mbezi na Moravian Kimara Stop Over.

Kwa upande wa misikiti inayotarajiwa kubomolewa ni Masjid Kilumbi Islamic Centre – Kimara Mwisho, Dalul Mustafah wa Kimara Stop Over, Masjid Baitul Maamur, Masjid Jaaria, Masjid Baitul Maamur na Almasjid Nuur iliyopo Kiluvya.

Misikiti mingine ni Masjid Jaalia Gogan, Masjid Nuur Kibamba CCM. Pia imo misikiti mitatu ya Mbezi Inn, Mbezi Luis na Temboni.

VIONGOZI WA DINI

Imam Mkuu wa Msikiti wa Al-Masjid Kirumbi Islamic Centre uliopo Kimara Mwisho, Ramadhan Juma, alisema wao hawatavunja wala kuondoa vitu vilivyomo katika msikiti huo kwa sababu hiyo ni nyumba ya Mungu.

“Hatutavunja wala kuondoa chochote maana hatuna pa kuvipeleka, tunawaachia waje wavunje wenyewe kwa sababu hii ni nyumba ya Allah,” alisema Juma.

Alisema kitu pekee watakachokitoa katika msikiti huo ni jeneza la kuzikia kwa sababu hutumika katika shughuli za  jamii.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum, alisema amesikia idadi ya misikiti 10 na makanisa 14 yapo katika orodha ya kuvunjwa.

Hata hivyo, alisema   misikiti ina viongozi wao ambao ni wadhamini lakini hawajawasiliana naye juu ya bomoa bomoa hiyo.

“Mimi sijawaona wakija hapa  labda hakuna kitu wanachohitaji, lakini kama kuna msaada watakuwa wanahitaji na kama kuna umuhimu wa kufuatilia wao watafuatilia,” alisema Sheikh Alhad.

Naye Paroko wa Parokia ya Kiluvya, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Maximilian Wambura, alisema wamebaini kuwa walijenga kwa makosa katika eneo hilo hivyo hawawezi kushindana na Serikali.

“Tulifanya makosa wakati tunajenga, tulijenga katika eneo la hifadhi ya barabara na hatutaki kushindana na Serikali,” alisema Padri Wambura.

Paroko huyo alisema tayari wana mipango ya kujenga kanisa jipya ambako wanatarajia kuhamia mwakani.

Kanisa jingine ambalo limekumbwa na bomoa bomoa hiyo ni lile la Mtakatifu Maria Parokia ya Kimara  ambalo linatakiwa kubomolewa nusu.

VITUO VYA AFYA, MAFUTA

Katika bomoa bomoa hiyo, vituo vya afya vilivyoguswa ni Hospitali ya Boch na Kituo cha Afya cha Kimara vilivyobomolewa nusu, Hospitali ya Neema iliyopo Kimara Stop Over, Kimara Centre Dispensary na Zahanati ya Arafa.

Vituo vya mafuta vinavyotakiwa kubomolewa ni Henry Filling Station Mbezi kwa Yusuph, Camel Oil- Kibamba, Uduru Oil Station-Kibamba, Total Stop Over na Camel Oil Kimara Stop Over.

Mbali na nyumba hizo pia Kituo cha Polisi Mbezi kwa Yusuf nacho kitabomolewa. Kingine ni kituo kidogo cha polisi Kiamara Mwisho.

WALIOVUNJIWA WAENDELEA KULALA NJE

Baadhi ya wananchi waliovunjiwa nyumba zao katika maeneo hayo wameendelea kulala kwenye vibanda wakiwa wamepanga matofali na kufunika kwa mabati huku baadhi wakilala nje.

Wananchi hao walisema wamelazimika kuendelea kubaki katika maeneo hayo kwa sababbu hawana mahali pa kwenda kwa sababu wameishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50.

Mmoja wa wananchi hao, Halima Salum (80), alisema analazimika kuishi kwenye kibanda cha mabati baada ya nyumba yake kuvunjwa.

Mwananchi mwingine, Helman Mramba (75), alisema pamoja na eneo hilo kuwekwa mipaka ya hifadhi ya barabara umbali wa mita 120 tangu miaka ya 1970, hawakuwahi kulipwa fidia na badala yake waliahidiwa kuwa watakapotakiwa kuhamisha watalipwa.

TANROADS

Mkurugenzi Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alipoulizwa, alisema yeye hawezi kuzungumzia  suala hilo kwenye vyombo vya habari na kuwataka wenye malalamiko waende katika vyombo vya sheria.

Habari hii imeandaliwa na LEONARD MANG’OHA, NORA DAMIAN na ASHA BANI.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles