28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

BOCCO AING’ARISHA SIMBA

Na GRACE HOKA-MBEYA

TIMU ya Simba imeifunga Tanzania Prisons bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa katika Uwanja wa Sokoine, Mbeya jana.

Bao hilo pekee la Simba lilipatikana katika dakika ya 83, kupitia kwa mshambuliaji wake, John Bocco, aliyeachia shuti baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Prisons.

Kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kukalia usukani wa ligi hiyo kutokana na kufikisha pointi 22, baada ya kucheza michezo kumi, wakishinda sita na kutoka sare minne.

Simba walianza kwa kasi mchezo huo ambapo dakika ya tisa Shiza Kichuya alishindwa kutumia vema nafasi aliyoipata, baada ya kuwazidi ujanja mabeki wa Tanzania Prisons na kupiga shuti lililotoka nje, akipokea pasi kutoka kwa Mzamiru Yassin.

Tanzania Prisons walijibu shambulizi hilo katika dakika ya 11, kupitia kwa Salum Kimenya, aliyepiga shuti lililookolewa na beki Erasto Nyoni.

Simba walionekana kusaka ushindi tangu mwanzo wa mchezo huo, ambapo katika dakika ya 20, kiungo Haruna Niyonzima alikosa bao baada ya kupiga shuti lililopaa juu na kutoka nje.

Prisons nao walikuwa imara kuliandama lango la Simba na katika dakika ya 25, Eliuter Mpepo aliwapiga chenga mabeki wa Simba na kuingia ndani ya eneo hatari, lakini alizuiliwa na beki James Kotei, aliyeokoa mpira.

Simba waliendelea kuliandama lango la Prisons, katika dakika ya 27, Mwinyi Kazimoto alishindwa kutumia vema nafasi aliyoipata baada ya kupiga shuti lililopaa juu.

Prisons walionekana kuwadhibiti Simba, huku wakifanya mashambulizi ya mara kwa mara, ambapo katika dakika ya 44, Eliuter Mpepo aliambaa na kupiga shuti lililopaa juu ya lango la Simba akiwa na kipa Aishi Manula.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, timu hizo hazikufungana.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu hizo kuendelea kushambuliana kwa zamu, huku kila moja ikitafuta ushindi.

Simba walifanya mabadiliko katika dakika ya 60, kwa kumtoa Haruna Niyonzima na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Ibrahim, huku pia ikimtoa Mwinyi Kazimoto katika dakika ya 66 na nafasi yake kuchukuliwa na Laudit Mavugo.

Mabadiliko hayo yaliisaidia Simba, ambao waliongeza kasi ya kupeleka mashambulizi langoni mwa Prisons, lakini mabeki wa Prisons walikuwa imara.

Simba walifanya tena mabadiliko katika dakika ya 78 kwa kumtoa Mzamiru Yasin na kuingia Ally Shomary.

Mabadiliko hayo yaliongeza nguvu zaidi katika kikosi hicho cha kocha Joseph Omog, kwa kufanya mashambulizi mara kwa mara na ndiyo yaliyozaa bao hilo katika dakika ya 83, kupitia kwa John Bocco.

Tanzania Prisons walifanya mabadiliko katika dakika ya 85 kwa kumtoa Salim Kimenya na kuingia Hamis Maunga.

Hadi dakika 90 za mchezo huo, Simba walitoka kifua mbele kwa ushindi huo wa bao 1-0 na kuzidi kuendelea kukaa kileleni katika msimamo wa ligi hiyo.

Katika michezo mingine ya ligi hiyo jana, timu ya Ruvu Shooting iliichapa Ndanda FC bao 1-0, huku Majimaji wakiifunga Mbao FC mabao 2-1 katika Uwanja wa Majimaji, mjini Songea, mkoani Ruvuma.

Stand United waliokuwa katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, walitoka suluhu na Mwadui.

Tanzania Prisons:

Arom Kalambo, Michael Ismail, Laurian Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhili, Salum Kimenya, Kasim Hamis, Eliuter Mpepo, Mohamed Rashid, Lambart Sabiyanka.

Simba:

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohamed Hussein, James Kotei, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, John Bocco, Mwinyi Kazimoto, Haruna Niyonzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles