BOBI WINE AENDA MAREKANI, JAJI MKUU AWAONYA POLISI

0
437

KAMPALA, UGANDA


MBUNGE wa upinzani, Robert Kyagulanyi, maarufu kwa jina la Bob Wine, ameruhusiwa kuondoka nchini Uganda kuelekea mjini Washington, nchini Marekani kwa matibabu zaidi baada ya awali kuzuiwa kusafiri na Jeshi la Polisi.

Robert Kyagulanyi, mwenye umri wa miaka 36, ambaye ni mwanamuziki maarufu, alizuiwa akiwa Uwanja wa Ndege wa Entebbe wakati akisubiri kuondoka kwenda Marekani kufuata matibabu baada ya kupata majeraha makubwa mwilini kutokana na kupigwa na wana usalama waliomkamata mjini Gulu kwa madai ya kuwachochea wafuasi wake kurushia mawe msafara wa Rais Yoweri Museveni.

Vyombo vya habari nchini Uganda vimeripoti kuwa baada ya mvutano wa muda mrefu, Bob Wine aliruhusiwa kusafiri kwenda Washington, Marekani.

Mwanasheria wake, Nicholas Opiyo amethibitisha kuwa mbunge huyo ameshaondoka Uganda, huku akiwa na magongo na baiskeli ya wagonjwa ambavyo vinamsaidia kutembea kutokana na mwili wake kukosa nguvu.

“Sasa naweza kuthibitisha kuwa Mheshimiwa Bob Wine ameondoka Entebbe kwa ndege ya KLM. Nimeshuhudia tukio hilo mwenyewe. Akiwa Uwanja wa Ndege Entebbe kabla ya kuondoka alikuwa na mkewe, Barbie na kaka yake Daks Sentamu,” alisema Opiyo alipozungumza na Shirika la Habari la AFP.

Kyagulanyi alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhaini Agosti 13, mwaka huu, baada ya wanaandamanaji kurushia mawe msafara wa Rais Museveni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Arua huko wilayani Gulu.

Kukamatwa kwake kumesababisha maandamano makubwa nchini Uganda tangu Agosti 20 mwaka huu bila kikomo, ambako wafuasi wake wanasema Bob Wine alipigwa na kuumizwa vibaya akiwa rumande katika Kituo cha Polisi cha Makindye, hivyo kuhitaji matibabu zaidi nje ya nchi.

Hata hivyo, Kyagulanyi aliachiliwa kwa dhamana Jumatatu wiki hii na kuondolewa kikwazo vya kusafiri nje ya nchi. Lakini alikamatwa tena na Polisi Alhamisi jioni akiwa uwanja wa ndege.

Wakili wa Mbunge huyo, Robert Amsterdam, aliliambia shirika la habari la Al Jazeera kuwa Kyagulanyi aliumizwa vibaya wakati akisafirishwa kutoka Hospitali ya Kiruddu kwenda Hospitali ya Taifa Mulago, mjini Kampala.

“Familia ya Bob Wine inahofia usalama wao. Mwili wa Bob umeumizwa sana. Tulipanga aondoke Uganda ili apate matibabu ya uhakika katika hospitali huru,” alisema wakili  Amsterdam.

Kwa upande wake, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Emilian Kayima, ameziita tuhuma dhidi ya polisi ni feki, kwani hazina ushahidi wowote.

Katika taarifa yake kwa umma juzi, Kayima alisema mwendesha mashtaka mkuu alilielekeza Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za kujeruhiwa Bob Wine wakati akitibiwa kwenye Hospitali ya Mulago.

“Kabla ya kufanyiwa vipimo, Jeshi la Polisi lilipewa taarifa kuwa Bob Wine anasafiri kwenda Marekani Agosti 30. Kutokana na hali hiyo, mheshimiwa Bob Wine alizuiwa kwa muda kabla ya kuendelea na safari yake,” alisema Kayima.

Kuzuiwa huko kulisababisha maandamano mengine zaidi mjini Kampala, huku wakichoma moto matairi, kurusha mawe na kuweka vizuizi barabarani.

Kyagulanyi ni mwanamuziki ambaye tangu alipoingia kwenye siasa na kuchaguliwa kuwa mbunge amekuwa tishio kwa utawala wa miaka 32 wa Rais Museveni, huku akipata sapoti kutoka kwa maelfu ya watu.

Julai mwaka huu kwenye muswada wa mabadiliko ya sheria ya kuondoa ukomo wa umri wa kugombea urais yamemaanisha Museveni atagombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2021.

Museveni, mwenye umri wa miaka 74, ni mtu wa karibu sana wa majeshi ya Marekani tangu alipoingia madarakani mwaka 1986.

KUGHARAMIA MATIBABU

Kinyume cha matarajio ya wengi kuwa Mbunge yeyote anapoumia au kuugua basi Bunge linahusika kugharamia matibabu yake, hata hivyo hali ni tofauti, kwani Mbunge huyo wa Kyadondo mashariki amelibeba jukumu hilo mwenyewe.

“Anagharamia mwenyewe mahitaji yote ya matibabu yake huko Marekani. Hatuna makubaliano na mtu yeyote kuwa atagharamia matibabu yake, lakini maisha yake ni muhimu sana kuliko fedha, kwahiyo hana masihara kwenye hilo, ndiyo maana ametafuta hospitali ya kiwango cha juu,” amethibitisha Mwanasheria wake Nicholas Opio.

POLISI WAMNG’ANG’ANIA BODIGADI

Katika hatua nyingine, polisi wamekiri kumshikilia Bodigadi wa Bob Wine, Eddie Ssebuufu au maarufu kwa jina la Eddie Mutwe.

Msemaji wa jeshi hilo mjini Kampala, Luke Owoyesigyire, amesema Mutwe anashikiliwa katika kituo cha polisi cha barabara ya Jinja kwa maelekezo ya idara ya upelelezi.

Inaelezwa kuwa Mutwe alitekwa nyara na kikundi cha watu wenye sare za jeshi mnamo Agosti 25, mwaka huu mjini Kampala.

“Ninachofahamu kuwa Mutwe yupo rumande kwa madhumuni ya upelelezi kutoka makao makuu. Sifahamu ni tuhuma zipi zinachunguzwa dhidi yake,” alisema Owoyesigyire.

Mutwe alikamatwa baada ya Bob Wine kutiwa nguvuni na kikosi cha kumlinda Rais Museveni.

Awali polisi walikanusha madai ya kumkamata Mutwe kwa muda wa wiki mbili hadi Mahakama Kuu ilipomwamuru Mkuu wa Intelijensia wa Jeshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkuu wa Majeshi ya Uganda kumfikisha mtuhumiwa huyo mahakamani.

Kupitia Mwanasheria wake, Anthony Kusingura wa kampuni ya uwakili ya Kiiza Mugisha, aliwasilisha ombi la kufikishwa mahakamni Mutwe.

MAANDAMANO

Maandamano makubwa yalianza kujitokeza Agosti 20, mwaka huu, huku waandamanaji wakishinikiza kuachiliwa huru kwa Bob Wine. Maandamano hayo ambayo hayajakoma yalisababisha shughuli mbalimbali kusimama, maduka kufungwa mitaani, hali ambayo ilisababisha mapambano makali kati ya polisi na wananchi.

JAJI MKUU ATOA ONYO KALI

Wakati huo, Jaji Mkuu wa Uganda, Bart Katureebe amevionya vyombo vya dola nchini humo kuwapeleka watuhumiwa wagonjwa Mahakamani.

Akizungumza  wakati wa uzinduzi wa mpango wa Haki, Sheria na Taratibu katika wilaya ya Rubirizi alisema kwa mujibu wa Katiba ya Uganda Ibara ya 44 ya mwaka 1995 ni marufuku kumpeleka mtuhumiwa yeyote anayeugua au kuumizwa.

“Vyombo vya dola vinapomkamata mtuhumiwa Mganda yeyote watambue ni binadamu si mnyama. Hatuhitaji kupokea watu mahakamani wakiwa wanavuja damu,kushindwa kutembea,wagonjwa kwa sababu hao wanapaswa kufikishwa mahakamani,” alisema Jaji Katureebe.

Kauli ya Jaji Mkuu Katureebe imekuja siku chache baada ya wabunge wa upinzani Robert Kyagulanyi (Bob Wine), Kassiano Wadri,Francis Zaake, Gerald Karuhanga, Paul Mwiru na watu wengine 33 kukamatwa na baadaye kupigwa na wana usalama.

Aliongeza kuwa, “Mnapaswa kuacha mwenendo huo mara moja. Zipo sheria zinazozuia kupiga na kuumiza watuhumiwa, kama umejikuta umemuumiza mtuhumiwa yeyote, nadhani sehemu sahihi ni Hopsitali si mahamani,”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here