BOBI WINE AAMUA KURUDI UGANDA

0
528WASHINGTON, MAREKANI

MWANAMUZIKI maarufu na Mbunge wa upinzani wa Jimbo la Kyaddondo Mashariki nchini Uganda, Robert Kyagulanyi, anayefahamika kwa jina la Bobi Wine, anasema kuwa, ameamua kurudi nyumbani baada ya matibabu nchini Marekani, licha ya kushtakiwa kosa la uhaini.

Akizungumza juzi mbele ya waandishi wa habari mjini Washington nchini Marekani, Kyagulanyi, mwenye umri wa miaka 36, ameibuka kama msemaji wa vijana nchini Uganda na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Rais Yoweri Museveni, ambaye yuko madarakani tangu mwaka 1986.

Bob Wine alishtakiwa pamoja na watuhumiwa wengine 32 wa kufuatia kile kilichoelezwa kuwa alishiriki katika vurugu za uchaguzi mdogo, ambapo gari la msafara wa Rais lilishambuliwa kwa mawe Agosti 14, 2018.

Mbunge anakabiliwa na makosa ya uhaini, kufuatia tukio la kushambuliwa kwa mawe gari la Rais Yoweri Kaguta Museveni. Aliachiliwa kwa dhamana kutoka kizuizini alikokuwa akishikiliwa huko Gulu.

Wakati wa vurugu hizo, dereva wa Bobi Wine aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi na yeye mwenyewe alikamatwa na kusababisha maandamano makubwa katika miji mbalimbali nchini humo, ambayo licha ya kukabiliana na vikosi vya ulinzi na usalama, lakini wananchi waliendelea kuandamana.

“Ninataka kurudi nyumbani, nataka kuendelea kutoa wito kwa Waganda wote kupigana kwa hali na mali kwa ajili ya kile wanachoamini. Ninaweza kwenda jela, kuna hatari ya kuhukumiwa adhabu ya kifo, lakini pia ninaweza kuuawa,” amesema Bob Wine, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington.

Mbunge huyo anaseme kuwa majeraha aliyonayo yametokana na vipigo alivyokuwa akipata alipokuwa kizuizini katika kambi mbalimbali za kijeshi kabla ya kufikishwa mahakamani. Hata hivyo,  Serikali ya Uganda imetupilia mbali shutuma hizo za kumjeruhi mbunge huyo.

Aidha, mwanasiasa huyo wa upinzani, alichaguliwa kuwa Mbunge mnamo mwaka 2017 na alizungumza kwa mara ya kwanza tangu aliwasili nchini Marekani siku chache zilizopita.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Bob Wine, Robert Amsterdam, ameiomba Marekani kulaani vitendo vya kihalifu na ukiukaji wa kila siku wa haki za binadamu na vikosi vya usalama vya Uganda.

“Silaha na vifaa vya kijeshi vya Marekani hutumiwa kwa kutesa Waganda. Afadhali kusitishwe mara moja kufadhili Jeshi la Uganda,” alisema mwanasheria huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here