27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Blessing Group wajivunia mafanikio ufugaji nyuki, mazingira

nyuki

Na Lilian Justice, Morogoro

KUTOKANA uharibifu wa mazingira unaojitokeza kila mara katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu umeifanya serikali  kuweka mkakati maalumu wa   kuweza kuzuia uharibifu huo.

Uharibifu  wa mazingira unaofanywa na binadamu kutokana na kutafuta mahitaji yake unaweza kudhibitiwa kwa njia mbalimbali  kama kutakuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya serikali na taasisi binafsi zinazopambana na utunzaji wa mazingira kila wilaya na kila mkoa kwa elimu endelevu ya mazingira.

Katika Mkoa wa  Morogoro  kuna changamoto ya  uharibifu wa mazingira japokuwa kuna taasisi nyingi binafsi  ikiwemo mashirika zinazopambana na changamoto hii  inayochangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko  ya tabia ya nchi yanatokea mara kwa mara kutokana na ukosefu mkubwa elimu ya mazingira hasa katika Milima ya Uluguru.

Katika kuhakikisha changamoto hiyo inavaliwa njuga Taasisi isiyo ya kiserikali yenye makao yake katika wilaya ya Mvomero inajulikana kwa jina la Blesssing Group inayojishughulisha na ufugaji wa nyuki na samaki pasipo kuharibu mazingira imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutekeleza majukumu yake katika sehemu mbalimbali za mkoa wa Morogoro na kuhimiza ufugaji salama ambao haugusi mazingira.

Aidha Mwenyekiti wa asasi ya Blessing Group Aron Mlemi  anaeleza  kuwa lengo la taasisi hiyo  ni kuinua uchumi, maendeleo ya wananchi sambamba na Mkakati wa Taifa wa Kukuza uchumi na kupunguza Umaskini Tanzania pamoja na utunzaji wa mazingira  na misitu kwa kutoa elimu na upandaji wa miti  sambamba na kutokana miti hovyo.

Anasema kuwa asasi yao inatoa mafunzo kwa ajili ya kujenga uelewa kwa jamii na wadau   kushiriki katika ufugaji wa nyuki kitaalamu na utunzaji wa mazingira na kuhamasisha kila kijiji katika wilaya ya Mvomero kutenga maeneo maalum ili  kufanikisha zoezi hilo.

Mlemi anafafanua kuwa kupitia mradi wa ufugaji wa nyuki kwa njia bora ya kisasa wamehamasisha kujenga uelewa kwa jamii kuonyesha uthubutu kwani unasaidia katika suala zima la utunzaji wa mazingira na kuongeza kipato katika jamii wanazoishi.

Vile vile anaeleza kuwa  kuanzisha na kuendeleza ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa Wilayani Mvomero unazingatia utunzaji wa mazingira na unaochangia kikamilifu kwenye uchumi wa wafugaji pamoja na juhudi za asasi kuhakikisha jamii inajiletea maendeleo endelevu kupitia mradi huo.

Anataja malengo ya asasi hiyo kuwa ni kuhamasisha ufugaji wa samaki,kuhimiza matumizi bora ya ardhi,matumizi bora ya misitu na bioanuwai, kuanzisha vitalu vya miti na mazao mengine rafiki wa mazingira na nyuki, kilimo kinachochochea utunzaji wa mazingira kuhimiza wafugaji wa nyuki kwamba ufugaji uwe wa kisasa na kuhimiza uzalishaji wenye tija katika jamii .

Anafafanua kuwa  kuna tatizo kubwa sugu katika Wilaya Mvomero ya uchomaji wa misitu hovyo hasa nyakati za kiangazi, maeneo mengi ya mlimani yanakuwa tayari yameshawashwa moto kutokana na shughuli za kilimo sababu kubwa ni kundi kubwa huishi kwa kutegemea shughuli za uchomaji mkaa kama njia ya kujipatia kipato na hivyo kujikuta wanachangia kwa asilimia kubwa kuharibu mazingira .

Asasi ya Blessing Group imejipanga kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo serikali katika kuelimisha jamii umuhimu  wa kutunza mazingira kwa kutambua miti/misitu ni rafiki kwa binadamu na zawadi ya asili na na faida nyingine kama mbao, asali na anta, dawa za asili, malisho ya mifugo, hali ya hewa nzuri na vyanzo vya maji.

Kupitia mradi wa ufugaji wa nyuki asasi ya Blessing Group inaamini kuwa pamoja na kuongeza pato la taifa na kaya kwa kiasi kikubwa pia inasaidia kulinda misitu na utunzaji wa mazingira kwa faida ya vizazi vilivyopo na vizazi vijavyo kwani mazingira mazuri ndiyo yatachangia kuwepo kwa huduma hizo muhimu ndani ya jamii

“Wafugaji wengi wa nyuki wakihamasishwa katika kila kijiji na kutenga maeneo wanajikuta wameingia katika utunzaji wa mazingira  kwani bila miti huwezi kufuga nyuki na watakosa chakula kwani nyuki wanategemea kwa asilima kubwa kupata vyakula vyao katika miti,’’anasema .

Aidha anaeleza kuwa katika zoezi zima la ufugaji wa nyuki hakuna mfugaji anayekubali shamba lake  la mizinga likachomwa moto, na jamii ikiwa na uelewa umuhimu wa misitu itasaidia katika kulinda na kutunza mazingira pasipo ya kuwa wanaelewa tayari faida wanayoipata kutokana na kuweka mazingira yote  katika hali ya usalama .

Akibainisha changamoto zinazojitokeza katika suala zima la ufugaji wa nyuki kwa njia za kisasa na utunzaji wa mazingira anasema kuwa ni pamoja na  kutokuwa na elimu endelevu ya ufugaji wa nyuki kitaalamu kwa njia bora za kisasa badala ya ufugaji uliojengeka wa mizinga ya magome ya magogo ambao huchangia kwa asilimia kubwa uharibifu wa mazingira.

Changamoto nyingine ni  asali kuuzwa kabla ya kuchakatwa na mwingiliano mkubwa wa matumizi ya ardhi ambayo siyo rafiki kwa ufugaji nyuki kwa njia bora ya kisasa, nyuki kuhama kwa kukosa chakula kwa tatizo la uchomaji moto ovyo misitu, ukosefu wa vitendea kazi, ukosefu wa rasilimali fedha na mwamko mdogo katika ufugaji wa nyuki.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa ufugaji nyuki kwa njia za kisasa na utunzaji wa mazingira Richard Haule, anasema kuwa asasi imejikita katika mradi wa ufugaji nyuki kama chanzo kikuu cha mapato na kushirikisha  kikamilifu  vikundi ambao ni wadau wakuu wa maendeleo katika jamii kwa kadri ya fursa kwa kufuga na kutunza mazingira kwa kushirikiana na serikali kama mdau mkubwa wa maendeleo ya umma.

Haule anasema asasi inatoa elimu kwa jamii na kujenga uelewa kupitia vikundi mbalimbali vya kijamii kuamsha na kushirikisha kikamilifu katika mradi wa ufugaji wa nyuki kwa njia bora ya kisasa na utunzaji wa misitu ya kupandwa na misitu asili pia ufugaji wa samaki ikiwa ni jitihada za kupambana na umaskini katika jamii.

Naye mmoja wa wafugaji wa nyuki Katika Wilaya ya Mvomero Msafiri Kimath anaeleza kuwa   ufugaji wa nyuki unaweza kumkwamua mwananchi kiuchumi na kuweza kutatua changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo kusomesha watoto , ujenzi wa nyumba ya kuishi na hata kuweza kumudu gharama mbambali za matibabu kwa familia.

Kimath anasema kuwa ni vyema wananchi wakaachana na kasumba kuwa ufugaji wa nyuki hauna tija kwa maendeleo jambo ambalo sio sahihi na  badala yake wananchi wanaotaka kujikita katika ufugaji wa nyuki kuwasiliana na maafisa ugani ili waweze kuwapa elimu juu ya ufugaji bora wa kisasa wa nyuki .

Hata hivyo ili serikali iweze kufikia malengo hayo ni vyema ikahakikisha maafisa ugani wanawafikia wananchi katika maeneo ya vijini kwani ndiko  kuliko na wananchi wengi ambao bado hawana uelewa mkubwa juu ya ufugaji wa nyuki jambo ambalo linawafanya baadhi yao kujikuta wakiharibu mazingira na baadhi yao wakikumbwa na ulipaji wa fidia kutokana na uharibifu huo.

Kwa upande mwingine  ufugaji wa nyuki hauna gharama kubwa ila kinachotakiwa ni mfugaji kuwa na elimu ya kutosha na kufuata mbinu sahihi za ufugaji kwa lengo la kupata mazao bora pasipo kuharibu mazingira kwa kuchoma moto misitu ya asili ambayo ni rasimali muhimu katika  jamii na Taifa kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles