24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

BITEKO ABAINI USANII KAMPUNI ZA UCHIMBAJI DHAHABU TANGA

Greyson Mwase, Tanga

Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko, amebaini usanii uliofanywa na Kampuni ya CANACO Tanzania Limited iliyokuwa ikifanya utafiti wa dhahabu Magambasi, Handeni mkoani Tanga, kuingia mkataba batili na Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Tanzania Gold Field Limited ya Canada huku makubaliano ya kodi ya serikali yakiwa hayatambuliki.

Kutokana na hali hiyo, Biteko ameipa kampuni hizo siku saba kuwasilisha nyaraka na mikataba yake yote serikalini ili ipitiwe.

Biteko ameyasema hayo leo Mei 9, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyasa, kilichopo wilayani Handeni mkoani Tanga, mara baada ya kufanya ziara katika kampuni ya CANACO na kutoridhishwa na utendaji wake.

“Kampuni hiyo ya Canada iliwaondoa wachimbaji wadogo kwenye eneo hilo ili wao waanze uchimbaji na wakaanza shughuli zake bila kuwasilisha makubaliano ya kimaandishi kati yake na Kampuni ya CANACO serikalini jambo ambalo ni kinyume na sheria za nchi.

“Haiwezekani wachimbaji wadogo ambao ndiyo wamiliki wa madini ya dhahabu katika eneo la Magambasi wakaondolewa kisha apewe mwekezaji mkubwa ambaye hadi sasa hakuna alichofanya,” amesema Biteko.

Pamoja na mambo mengine, amesema anachofanya mwekezaji huyo kwa sasa ni kuchenjua mabaki ya udongo wenye dhahabu na kuuza huku akiharibu mazingira na wachimbaji wadogo wenye uwezo wa kuchimba dhahabu katika eneo hilo wakiwa wanahangaika.

Aidha, Biteko amemtaka Kaimu Ofisa Madini Mkazi wa Handeni, Idrissa Yahya, kuanza uchambuzi wa vipengele vyote vya sheria na kanuni za madini  ili kuangalia namna vilivyokiukwa na kuwasilisha ripoti ofisini kwake.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe, alimpongeza Biteko kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles