26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

 Bilioni 83 zatolewa na Serikali ili kuimarisha elimu

                             Bethsheba Wambura  



Serikali imetoa jumla ya sh. bilioni 83.2 ili kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini kati ya Julai na Oktoba mwaka huu.

Kati ya fedha hizo  shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa kwenye shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 zilienda kwenye shule za sekondari ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila malipo.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Ijumaa, Novemba 16, bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa 13 wa Bunge ambalo  limeahirishwa hadi Januari 29, 2019.

Amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimumsingi bila malipo uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza umeimarika na kwamba kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu kwenye mitihani ya kumaliza darasa la saba.

“Kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu katika mitihani ya kumaliza darasa la saba, ambapo mwaka 2016 ilikuwa wastani wa asilimia 70 na mwaka 2018 ilikuwa ni wastani wa asilimia 78, hali hiyo imeongeza mahitaji mbalimbali ikiwemo miundombinu katika shule zetu za msingi na sekondari,” amesema.

Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu inaendelea na mikakati ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu muhimu ya shule.

“Kwa mfano, kupitia programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R), shilingi bilioni 53.4 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari.  Aidha, shilingi bilioni 9.2 zimeelekezwa katika uimarishaji wa miundombinu ya elimu kupitia programu ya kuboresha elimu ya shule za msingi (EQUIP-T),” amesema.

Aidha Waziri Mkuu ameziagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya taifa zihakikishe zinasimamia kikamilifu mitihani hiyo ili kuepuka udanganyifu, itakapobainika kuwepo kwa udanganyifu wa mitihani hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayehusika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles