25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BILIONEA WA LUGUMI KUPIMWA AKILI

Na PATRICIA KIMELEMETA


DAKTARI Luis Shika (48), ambaye wiki iliyopita alitaka kununua nyumba za mfanyabiashara Said Lugumi, anatarajiwa kupelekwa hospitali kupimwa afya ya akili.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu yaliyofanyika Dar es Salaam jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Jeshi la Polisi (SACP), Benedict Kitalika, alisema uamuzi wa kumpeleka hospitali Dk. Shika  kuchunguzwa afya ya akili yake, umetokana na uchunguzi wa awali ulioonyesha anaweza kuwa na tatizo hilo.

Alisema uchunguzi wa afya ya akili ya Dk. Shika utalisaidia Jeshi la Polisi kwenye upelelezi wake.

Kamishna Kitalika alisema uchunguzi wa awali ulihusisha historia ya maisha yake inayoonyesha ni msomi aliyewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini Urusi kabla ya kurudi nchini na kuishi kwenye chumba kimoja cha kukodi, huku sababu za kurudi kwake zikiwa hazijulikani.

Alisema uchunguzi wa polisi umelazimika kwenda mbali zaidi kuangalia tatizo lililomsibu na kama kuna jinai yoyote.

“Na sisi tumejiuliza sana kuhusu utimamu wa akili kama upo sawa au kuna tatizo la kisaikolojia, kwa sababu ukiangalia historia yake inaonyesha wazi ni msomi mzuri ambaye ameshika nafasi za uongozi nchini Urusi, lakini maisha anayoishi nchini si ya kuridhisha.

“Hatujui amepatwa na nini hadi kufikia hatua ya kukodi chumba kimoja cha kuishi katika Mtaa wa Tabata, huku mwonekano wake ukiwa haupo sawa kisaikolojia,” alisema Kamishna Kitalika.

Aidha, Kamishna Kitalika alisema polisi haiwezi kuangalia jinai peke yake iwapo kuna kitu cha ziada kimeongezeka na hakipo sawa, hivyo wanapaswa kwenda mbali zaidi kiuchunguzi ili waweze kujua chanzo cha tatizo na kukifanyia kazi.

“Tunatarajia kumpeleka hospitali wakati wowote ili kuangalia kama kuna tatizo katika afya ya akili au la kutokana na historia yake ya maisha inavyojionyesha, hali ambayo inaweza kutupa majibu sahihi,” alisema Kamishna Kitalika.

Wakati huo huo, jalada la kesi ya Dk. Shika limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) ili aweze kuangalia kama kuna jinai yoyote iliyotendeka kwa mtuhumiwa huyo au la.

Akizungumzia hilo, Kamishna Kitalika alisema licha ya jalada hilo kuwa mikononi mwa AG, imebainika kuwa baadhi ya kanuni wakati wa mnada wa nyumba za Lugumi hazikufuatwa.

Aliitaja moja ya kanuni hizo kuwa ni kulipa asilimia 25 pale pale baada ya mteja kujitokeza hali ambayo inaongeza shaka.

“Katika mnada ule, baadhi ya kanuni hazijafuatwa ikiwamo ya kumtaka kulipa asilimia 25 pale pale mara baada ya kununua, lakini suala hilo halijafanyika badala yake waliendelea kupiga mnada nyumba nyingine, hivyo kama taasisi za uchunguzi tunapaswa kufuatilia hatua kwa hatua,” alisema Kamishna Kitalika.

Wiki iliyopita, Dk. Shika alijitokeza kwenye mnada wa nyumba tatu za Lugumi, mbili zipo Mtaa wa Mbweni JKT na moja ipo Upanga na kushinda minada yote.

Mnada huo ulifanywa na Kampuni ya Udalali ya Yono kwa amri ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Dk. Shika aliahidi kununua nyumba hizo kwa thamani ya Sh bilioni 2.3 na kutakiwa kulipia asilimia 25 ya fedha hizo ambazo ni Sh milioni 800.

Alishindwa kulipa na badala yake alieleza kuwa anasubiri aingiziwe fedha benki na hivyo kukamatwa na polisi akidaiwa kuharibu utaratibu wa mnada.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles