27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

BILIONEA BILL GATES AIMWAGIA MAMILIONI TANZANIA

NA MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

TAASISI ya Bill na Mellinda Gates imetenga dola za Marekani milioni 350 (takribani Sh bilioni 777.084) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali nchini.

Miradi hiyo ni pamoja na ya sekta ya kilimo, afya na mifumo ya  elektroniki ya upatikanaji wa taarifa.

Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni tajiri namba mbili duniani, Bill Gates, alitoa kauli hiyo Ikulu Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya   mazungumzo na Rais Dk. John Magufuli.

Gates ambaye pia ni mmiliki wa kampuni za Microsoft na Cascade Investement LLC, alisema kama ambavyo taasisi yake imeshirikiana na Tanzania katika kuimarisha huduma za afya  nchini, fedha hizo zitaelekezwa zaidi katika utekelezaji wa miradi ya afya.

“Tutaelekeza fedha hizi zaidi katika kupunguza vifo vya uzazi, kukabiliana na  malaria, kuimarisha lishe na kukabiliana na utapiamlo.

“Pia zitaelekezwa katika sekta ya kilimo ambako zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao, kuzalisha mbegu bora na kuboresha ufugaji utakaoongeza chakula na pia zitasaidia kuweka mifumo ya kisasa ya upatikanaji wa taarifa,”alisema raia huyo wa Marekani.

Alieleza kufurahishwa na maendeleo ya uchumi wa Tanzania   na uongozi na msimamo wa Rais Magufuli juu ya kutaka miradi hiyo ilete matokeo yenye manufaa.

Pia aliahidi kuwa ataendelea kuja nchini   kuimarisha zaidi ushirikiano na kufuatilia utekelezaji wa miradi.

Rais Magufuli alimshukuru tajiri huyo kwa mchango mkubwa unaotolewa na taasisi yake katika miradi mbalimbali  nchini.

Alisema taasisi hiyo itazitoa fedha hizo katika kipindi cha miaka mitano kuanzia sasa, huku akimhakikishia Gates kuwa fedha hizo zitaleta maendeleo yaliyokusudiwa.

Mazungumzo hayo kati ya Rais Magufuli na Gates yalihudhuriwa pia na Waziri wa Kilimo, Ufugaji na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba  a na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kuwa na mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani  nchini, Dk. Inmi Patterson ambaye alisema Marekani itatoa fedha za nyongeza Sh bilioni 499.500 katika mwaka ujao kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayogusa sekta za elimu, afya, lishe bora na utawala bora.

Patterson alisema Marekani imeongeza fedha hizo katika miradi inayotekelezwa   nchini kwa sababu ina dhamira ya dhati ya kushirikiana na Tanzania.

Rais Magufuli alimshukuru Patterson kwa mchango mkubwa ambao Marekani imekuwa ikiutoa kwa Tanzania.

Aliiomba Marekani kusaidia kujenga hospitali kubwa ya  taifa katika makao makuu ya nchi mkoani Dodoma kuongeza uwezo wa mkoa huo kutoa huduma za matibabu ikilinganishwa na ilivyo hizi sasa.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles