24.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

Benzema amefanya maamuzi sahihi kuitosa Ufaransa

NA BADI MCHOMOLO

SIKU zote kwenye soka hakuna mchezaji au kiongozi aliye juu dhidi ya timu au shirikisho bila ya kujali mafanikio makubwa aliyonayo mchezaji au kiongozi husika.

Siku zote wachezaji wenye mafanikio makubwa wamekuwa wakiongoza kufanya baadhi ya mambo ambayo hayakubaliki na jamii, lakini wamekuwa wakipewa nafasi kubwa kutokana na mafanikio yao au jinsi wanavyo peperusha bendera ya nchi.

Mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, nyota wa timu ya taifa ya Misri, Mohamed Salah, aliingia kwenye mgogoro na taifa hilo baada ya kuomba aongezewe ulinzi huku mchezaji huyo akiitwa kulitumikia taifa hilo kwenye michuano mbalimbali.

Kauli hiyo aliitoa hasa kutokana na kiwango kikubwa alichokionesha mchezaji huyo msimu uliopita akiwa na klabu yake ya Liverpool, hivyo kumfanya mchezaji huyo kuwa na jina kubwa Afrika.

Hata hivyo shirikisho la soka Misri liliweka wazi kuwa, hakuna mchezaji ambaye yupo juu ya timu au shirikisho, hivyo wachezaji wote wana haki sawa.

Oktoba 2015 mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa na klabu ya Real Madrid, Karim Benzema aliingia kwenye mgogoro mkubwa na taifa lake baada ya kudaiwa kuwa anamiliki mkanda wa ngono wa mchezaji mwenzake Mathieu Valbuena huku akiwa na lengo la kutaka kujipatia fedha.

Kitendo hicho kilionekana kuwa cha utuvu wa nidhamu na uzalilishaji, hivyo shirikisho hilo la soka lilitangaza kumfungia Benzema kushiriki katika kulitumikia taifa hilo.

Ilionekana kuwa ni kitendo cha kuhatarisha baadhi ya mafanikio ya taifa hilo, lakini shirikisho lilifanya jambo sahihi kumfungia mchezaji huyo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Wadau mbalimbali wa soka wakiwa makocha wakuu, mashabiki na viongozi walijaribu kutoa ushauri kwa shirikisho hilo kwa kuomba mchezaji huyo apewe masamaha kwa ajili ya manufaa ya taifa, lakini hakuweza kusamehewa.

Benzema aliamua kupeleka nguvu zake ndani ya klabu ya Real Madrid na kuweza kuisaidia timu hiyo kuweza kuandika historia mpya ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo pamoja na mataji mengine ikiwa pamoja na Ligi Kuu Hispania.

Tayari miaka mitatu ya kifungo cha mchezaji huyo imefikia mwisho, hivyo shirikisho la soka nchini Ufaransa kupitia kwa rais wake Noel Le Graet, mwishoni mwa wiki iliopita ilimuashia taa ya kijani kwa maana kuwa, muda wowote kuanzia sasa mchezaji huyo anaweza kuitwa ndani ya kikosi cha kocha wao Didier Deschamps.

“Sina tatizo na Benzema, tayari amemalizana na taifa lake, hivyo muda wowote anaweza kuitwa kikosini,” alisema Noel Le Graet mwishoni mwa wiki iliopita.

Saa chache baada ya rais huyo kutoa kauli hiyo, Benzema alitumia ukurasa wake wa Twitter kuweka wazi kuwa, hana mpango tena wa kurudi kulitumikia taifa hilo.

“Mr Le Graet naomba niache peke yangu, Ufaransa kwa sasa ni mabingwa wa dunia, hivyo inatosha naomba niacheni nipumzike,” aliandika Benzema kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Kitendo cha Benzema kuachana na timu hiyo ya taifa ni cha kiungwana, amefanya maamuzi sahihi na ameangalia mbali sana.

Kwanza tayari taifa hilo linaonekana kuwa juu kisoka baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Urusi, hivyo Benzema ameona hakuna kitu kipya ambacho atakwenda kukifanya kwa ajili ya taifa katika siku za hivi karibuni hasa kutokana na umri wake wa miaka 30.

Pia inawezekana kuwa ameangalia mbali sana endapo atarudi kuitumikia timu hiyo na kushindwa kuisaidia na kujikuta akikosolewa mara kwa mara na mashabiki.

Aliyekuwa nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani, Mesut Ozil, mara baada ya kumalizika kwa michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, alitangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo kutokana na mashabiki kumshambulia juu ya kiwango chake pamoja na kupiga picha na rais wa Uturuki.

Ujerumani walisahau kuwa, mchezaji huyo alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio makubwa ya taifa hilo katika kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia nchini Brazil, lakini baada ya timu hiyo kutolewa katika hatua ya makundi alionekana kuchangia kwa kiwango kibovu.

Benzema amefanya maamuzi sahihi, ukweli ni kwamba ameangalia mbali ikiwa pamoja na kuwapa nafasi wachezaji chipukizi wenye kasi kubwa ambao wana nafasi kubwa ya kulipigania taifa hilo kama vile Paul Pogba, Kylian Mbappe, Ousmane Dembele na wengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles