25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya UBA kuwajengea nyumba mapacha

 NA VERONICA ROMWALD-DAR ES SALAAM

HATUA ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanikisha upasuaji wa kuwatenganisha mapacha waliozaliwa wakiwa wameungana kwa kiasi kikubwa katika ini, Precious na Gracious Mkono, imeandika historia mpya kwa hospitali hiyo.

Kutokana na hatua hiyo, uongozi wa Benki ya UBA umeamua  kuwapa ufadhili mapacha hao ikiwamo kuwapa bima ya afya kwa miaka 10 mfululizo kuanzia sasa, hivyo watatibiwa bila malipo kote nchini.

Benki hiyo pia imeahidi kuijengea nyumba ya kisasa familia hiyo itakayogharimu Sh milioni 18 na imewafungulia akaunti maalum kwa ajili ya kuwezesha makuzi yao.

Akizungumza na waandishi wa habari  hospitalini hapo jana, Mkurugenzi Mkuu wa UBA, Usman Isiaka alitaja namba ya akaunti hiyo kuwa ni 560105600013396.

“Tunawapongeza madaktari wa Muhimbili kwa kufanikisha upasuaji wa pacha hawa, UBA tunaungana nao kuwapatia bima hii, kuwajengea makazi na kufungua akaunti hii ambayo tayari wafanyakazi wetu wamechangia Sh milioni mbili.

“Tunaalika na watu wengine kuchangia katika akaunti hii  kuwezesha makuzi ya watoto hawa ambao ni historia kubwa.

“Tunaipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwekeza miundombinu iliyofanikisha matibabu ya mapacha hawa,” alisema.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alisema tangu mapacha hao walipopokewa, kulazwa na kufanyiwa upasuaji, hospitali hiyo imetumia takriban Sh milioni 34.

“Tuliwapokea kutoka Kisarawe, upasuaji ulikuwa wa mafanikio lakini hatukuweza kuwaruhusu kwenda nyumbani kwa sababu  makazi yao hayakuwa rafiki kwa ukuaji wao,” alisema.

Profesa Museru alisema hospitali hiyo itaendelea kufuatilia ukuaji wa mapacha hao hata baada ya kuwaruhusu na kwamba matibabu yao ndani ya hospitali hiyo yatagharamiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo alisema kwa hatua kubwa ambayo Muhimbili imefikia kuweza kuwatenganisha pacha hao, inastahili kupewa pongezi.

“Nawaomba UBA waje Kisarawe wafungue tawi karibu na wananchi waendelee kunufaika na haya mazuri waliyonayo.

“Tunaendelea kupokea chochote wananchi walichonacho, wakichangia itakuwa ni historia nzuri tunaijenga kwa pamoja kupitia namba hiyo ya akaunti, kutoa ni moyo si utajiri, tuendelee kushikamana,” alisema.

Akizungumza, Esther alishukuru uongozi wa benki hiyo kwa kumpatia ufadhili huo kwa sababu  hakutegemea na aliwashukuru pia madaktari waliofanikisha upasuaji huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles