30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Benki ya NMB, Wizara ya Mifugo kushirikiana

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia mifugo, Profesa Elisante ole Gabriel, ameitaka Benki ya NMB kushirikiana na wizara hiyo katika kukuza sekta ya maziwa nchini kwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa wananchi kunywa maziwa kutokana na taarifa iliyotolewa na Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Prof. Gabriel aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dodoma, akiwa kwenye kikao na maofisa kutoka idara ya kilimo ya Benki ya NMB, waliofika ofisini kwake kumwelezea mikakati ya Benki ya NMB ambayo imekuwa ikifanya tafiti na wadau wa sekta ya maziwa, lengo likiwa ni kutaka kuwekeza katika sekta hiyo.

“Kwa takwimu ambazo zimetolewa na Shirika la Chakula Duniani ni kwamba, kwa wastani angalau mtu anatakiwa walau atumie lita mia mbili kwa mwaka za maziwa, lakini kwa bahati mbaya kwa Watanzania wastani ni lita arobaini na saba tu, bado tuna kazi kubwa sana,” alisema Prof. Gabriel.

Alisema Benki ya NMB inapaswa kuwa na ushirikiano na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Dawati la Sekta Binafsi ambalo limekuwa likiwaunganisha wadau wa sekta ya mifugo na uvuvi ili kuhakikisha mazao yatokanayo na ng’ombe yakiwemo maziwa yanatumika ipasavyo.

Katika kikao hicho ambacho kimehudhuriwa pia na watendaji wakuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Katibu mkuu huyo pia alisema ni wakati mwafaka kwa Benki ya NMB kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kuhakikisha inawaletea maendeleo wafugaji, hususan wafugaji wadogo ambao wamefanikiwa pamoja na wafugaji ambao watakuwa tayari kubadilika na kuingia katika ufugaji wa kisasa na kuachana na ufugaji wa kuhamahama.

 “Ningependa sekta hii ya mifugo iwe pia na tafiti nyingi zinafanyika, sasa tukifanya hizo tafiti tutaweza kuleta mabadiliko chanya na yenye uhakika katika maendeleo ya wafugaji kwa sababu lengo si tu kufanya jambo, lakini liwe jambo ambalo linaweza kugusa maisha ya wafugaji,” alisema Prof. Gabriel.

Kwa upande wake Meneja Mwandamizi wa Benki ya NMB kutoka Idara ya Kilimo, Carol Nyagaro, alisema kutokana na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli pamoja na utendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imewalazimu benki hiyo kubadili mtazamo wa namna ya kutafuta wateja wapya kupitia sekta mbalimbali.

“Kutokana na kasi ya Rais Dk. John Magufuli na uongozi mzima wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwetu inajenga mazingira mazuri ya kufanya biashara, pia kuchangia maendeleo ya jamii na kuweza kutengeneza wateja wa siku zijazo,” alisema Ngayaro.

Alisema Benki ya NMB kupitia idara ya kilimo inafikiria pia kuwekeza katika sekta ya samaki ambayo imekuwa ikifanya vizuri kiuchumi katika siku za hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles