23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BENKI KUU YAJIBU HOJA  ZITO

 


Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk. Yamungu Kayandabila, amevunja ukimya na kupinga hoja ya kuongezeka kwa deni la Taifa iliyoibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

Jana jioni Zitto alitoa taarifa akinukuu taarifa ya mapitio ya uchumi ya kila mwezi ya Juni mwaka huu, ambapo alisema Serikali imeongeza deni la ndani kwa Sh trilioni 1.5 katikati ya Mei na Juni mwaka huu.

Akizungumza jana na MTANZANIA Dk. Kayandabila, alisema suala la kuongezeka kwa deni la Taifa linalofikia Sh trilioni 1.5 si la kweli kama lilivyodaiwa na mbunge huyo.

Alisema nchi yoyote inayoweze kuendelea inahitaji kuwa na mifumo mizuri ya ndani ikiwamo kudhibiti madeni yake ya ndani na nje jambo ambalo linafanywa kikamilifu na Benki Kuu ya Tanzania (BoT)  kwa kushirikiana na serikali chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.

Dk. Kayandabila, ambaye alipata kuwa Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tatu, alisema kuwa hata ripoti ya hali ya uchumi inayotolewa na Benki Kuu iko sawa.

“Mimi ni mwalimu na sasa nitashika chaki ili kutoa somo la deni la Taifa. Ninachotaka kukwambia kwamba nchi yetu tuna instrument karibu nne.

“Kwa mfano kuna kitu kinaitwa DSA, tulifanya mwaka jana Desemba tukiwa pamoja na IMF, Benki ya Duania pamoja na taasisi zingine ambazo sisi ni wanachama ndani ya SADC ambapo huangalia hali ya nchi na madeni na IMF walitoa mapendekezo yao.

“Na kuna Mediam Term ambapo huwa tunafanya mapitio na tathimini ya kina ya madeni yetu hata kwa kuanzia miaka mitatu hadi 10 ijayo, na hapo ndipo unakuta kuna miradi mikubwa kama SGR, Stiegler’s, barabara itakuwaje yaani hapa ni ile miradi mikubwa ambapo pia tunaangalia hadi mikopo inakuaje.

“… na tatu tuna mfumo wa CTIA ambayo kwa nchi yetu tupo strong (imara) na tunaangalia sera, hizi ndizo tools (zana). Ambapo pamoja na udogo uchanga wa nchi yetu tunatumia njia hizi za kimataifa hivyo tuko vizuri tofauti na baadhi ya wanasiasa wanavyodai,” alisema Dk. Yamungu ambaye ni Naibu Gavana anayeshughulikia Uchumi na Fedha.

Dk. Kayandabila, ambaye pia alipata kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema katika awamu zote za uongozi imekuwa tofauti na Rais Dk. John Magufuli, ambaye amekuwa akifuatilia kwa kina kuhusu deni la taifa namna ya upandaji wake kila wakati.

“Katika wazee ambao wamepata kuongoza nchi yetu huyu bwana ni tofauti kwani amekuwa akifuatilia kila hatua ikiwamo deni la taifa. Ndio maana hata mikopo tunayochukua ni ile ya miradi mikubwa ambayo hataweza kuiumiza nchi,” alisema Dk. Kayandabila.

Hata hivyo alikanusha taarifa za zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii kwamba hivi sasa Benki Kuu kuwapo kwenye mpango wa kuchapisha noti mpya  huku akishangazwa na hoja hizo alizoziita hazina mashiko.

HOJA YA ZITTO

Jana jioni Zitto, alitoa taarifa akinukuu taarifa ya Mapitio ya Uchumi ya kila mwezi ya Juni mwaka huu, ambapo alisema serikali imeongeza deni la ndani kwa Sh trilioni 1.5 katika ya Mei na Juni mwaka huu.

Alisema Benki Kuu ya Tanzania imeonyesha kuwa Serikali ilitumia Sh trilioni 3 na bilioni Sitini  kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.

“Hii ilikuwa ni nyongeza ya asilimia 31 ya matumizi ya serikali ukilinganisha na matumizi ya mwezi Juni mwaka 2017. Hata hivyo, taarifa hiyo hiyo ya Benki Kuu inaonyesha kuwa mapato yote ya serikali kwa mwezi Juni 2018 yalikuwa ni Shilingi trilioni 1 na bilioni 800  kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo kodi na mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM).

“Hivyo kulikuwa na nakisi ya Shilingi Trilioni 1 na Bilioni 400 katika Mwezi huo. Ili kuziba nakisi hiyo Serikali iliuza dhamana na hati fungani zenye thamani ya shilingi bilioni 260 na hivyo kuendelea kubakia na nakisi ya Shilingi 1.14 Trilioni. Katika mwezi huu wa Juni Serikali ilitumia jumla ya Shilingi 1.7 Trilioni kulipia miradi mbalimbali ya Maendeleo kwa mujibu wa Taarifa hii ya Benki Kuu,” alisema Zitto

Alisema katika taarifa hiyo ya Benki Kuu inaonyesha pia kuwa Juni 2018 Serikali Kuu ilikopa kutoka ndani jumla ya Sh trilioni 1 na Bilioni 500 na hivyo kuongeza Deni la Taifa kutoka Sh trilioni 13.2 mpaka Sh trilioni 14.7 kati ya Mei, 2018 na Juni, 2018.

“Hapa ndipo panazua maswali ambayo Benki Kuu inapaswa kuueleza Umma ni nini kinaendelea kwenye maamuzi ya uendeshaji wa Uchumi wetu,” alisema

Alisema anatambua kwamba serikali hukopa kutoka Benki Kuu ili kuendesha baadhi ya shughuli zake kwa kupewa ‘overdraft’ au wakati mwengine kutoka kwenye mabenki nchini.

“Uzoefu unaonyesha kuwa ‘overdraft’ hii huwa na kikomo maalumu na hutolewa kusubiri makusanyo ya kodi ya Mwezi husika. Kwa mfano Taarifa za Benki Kuu za miezi na Machi na Mei zinaonyesha mikopo ya namna hii iliyochukuliwa na kurejeshwa. Hata kwa mwezi wa mwisho wa mwaka wa fedha na mkopo mkubwa namna hiyo inaleta mashaka makubwa,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Huyu mkuu wa benki hajachanganua hoja za mheshimiwa Zito alivyozianisha, je aseme hilo jambo halipo, Zito ni mzushi. Huwezi kusema tu kwamba si kweli. Mbona Zito ametoa takwimu zinaoeleweka?
    Mambo ya kuilinda serikali katika makosa mara nyingine sio sawa kabisa. Heri kukaa kimya, ni kujibu kuzuri zadi kuliko kutoa hoja zisizo na majibu kamili. Naamini Zito kwa moyo wa uzalendo anaangalia athari za baadaye za mikopo na uendeshaji wa serikali. Sisi mbumbumbu wa uchumi tunasikiliza kwenu.
    Swali liko hewani Zito amesema uongo?

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles