25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Benki  CRDB  kufanya maboresho huduma, kusambaa wilayani

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji Mpya wa Benki ya CRDB Ndugu Abdulmajid Mussa Nsekela amewahakikishia Wateja, Wanahisa  na Wadau wote wa Benki ya CRDB kuwa Benki hiyo ipo kwenye mikono salama na itaendelea kukua pamoja na kuzalisha faida kama ilivyotarajiwa.

Nsekela aliyasema hayo katika Mkutano na Waandishi wa habari wa kujitambulisha rasmi uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Nsekela alisema amedhamiria kufanya maboresho makubwa katika utoaji huduma kwa wateja kwa kutilia mkazo katika maeneo matano muhimu, ambayo ni uboreshaji wa mifumo na taratibu za  utoaji huduma, ili ziendane na mahitaji halisi ya wateja na soko, kuongeza weledi na umahiri wa wafanyakazi, kuwekeza kwenye teknolojia ya kisasa, kukuza biashara katika nyanja zote ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.

Atahakikisha Benki inafanya vizuri kwenye soko na kupata faida zaidi ili kutoa gawio nono kwa wanahisa.   “Tutakuwa tukiboresha mara kwa mara taratibu za jinsi ya kupata na kutumia huduma zetu. Tunataka upatikanaji na utumiaji wa huduma za Benki CRDB uwe rahisi, huku tukiendelea kuzisogeza huduma hizo karibu zaidi na wateja wetu” alisema Nsekela.

Akifafanua zaidi juu ya uboreshwaji wa huduma na mikakati ya Benki ya CRDB  katika eneo hilo muhimu, Nsekela alisema kwa kipindi kifupi kijacho Benki ya CRDB  itajikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidigitali (innovative products and services)  itakayowezesha kuwafikia wateja wengi zaidi, kwa urahisi zaidi, mahali popote walipo na hivyo kuwaondolea wateja wao ulazima wa kutembelea matawi ya Benki ya CRDB pindi wanapohitaji huduma.

“Tutatumia fursa ya kuwa zaidi ya watanzania milioni 19.3 wanatumia simu za mikononi  kufanya miamala yao na kuwashawishi kutumia bidhaa zetu za SimBanking na SimAccount ambazo nazo hutoa huduma kama hizo” alisema.

Akiongelea kuhusu mikakati ya kusogeza huduma kwa wateja, Nsekela alisema Benki ya CRDB imejiwekea malengo ya kufikisha huduma katika wilaya zote nchini ifikapo mwaka 2022.

Vilevile wamejiwekea lengo la kuongeza Mawakala wake wa FahariHuduma katika kila kona ya nchi. Alisema pia Benki hiyo ina mpango wa kuendelea kupanua wigo wa huduma zake nje ya nchi.

Akielezea kuhusu mahusiano baina ya Benki hiyo na Serikali na wadau wengine,  Nsekela alisema  kuwa Benki ya CRDB inaitambua Serikali kama Mwanahisa wake na mdau mkubwa wa biashara.

“Benki ya CRDB itaendela kuthamini mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na Serikali na taasisi zake na tutaendelea  kubuni huduma na bidhaa mbalimbali mahususi kwa ajili ya kufikia mahitaji ya Serikali pamoja na wafanyakazi wake mmoja mmoja. Tunajivunia kuwa mmoja wa wadau wakubwa wa Serikali ili kwa pamoja tuweze kujenga uchumi wa nchi hususani katika kipindi hiki ambacho tunaelekea katika kujenga uchumi wa kati wa Viwanda,” alisisitiza Nsekela.

Alisema ya uchumi nchini inatoa fursa kubwa ya ukuaji kwa mabenki nchini huku akibainisha kuwa Benki ya CRDB itaendelea kutia mkazo katika kuhudumia wateja  Wakubwa, Wadogo na wa Kati pamoja na Biashara ya kilimo na kuwawezesha wawekezaji kwenye sekta ya viwanda ili kujenga Tanzania ya viwanda.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CRDB Ally Laay alisema Bodi hiyo ina amini kuwa Nsekela ni mtu sahihi kabisa wa kuongoza Benki ya CRDB na kuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha.

Laay pia alitumia nafasi hiyo kumshukuru Dkt. Kimei kwa mchango wake kwa Benki ya CRDB kwa kipindi cha miaka 20 aliyoiongoza. “Ni kazi ngumu sana, lakini Dk Kimei ameifanya kwa kujitoa na weledi wa hali ya juu sana,” alisema Laay.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles