33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bendera yapandishwa kileleni Mlima Kilamanjaro kuzindua sherehe za Uhuru

Na Upendo Mosha, Moshi

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira, ametumia ufunguzi wa kupandisha bendera kwenye mlima Kilimanjaro, kumuagiza  Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) Angela Nyaki, kusimamia usalama wa wananchi wanaoishi vijiji vya jirani na mlima huo ikiwa ni pamoja na kudumisha mahusiano mazuri.

Mgwira alitoa agizo hilo wakati akizindua zoezi la kupandisha bendera ya Tanzania katika kilele cha mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 58 ya uhuru wa Tanzania.

Alisema ni wajibu wa mhifadhi huyo kusimamia usalama wa wananchi na mali zao pasipo ubaguzi wala uonevu ambao husabaisha tafrani na kwamba tukio la mwananchi kukutwa amefariki katika hifadhi hiyo katika mazingira tatanishi, inaleta shida juu ya usimamizi wa ulinzi wa mlima na jamii.

“Serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro itaendelea kutoa ushirikiano katika hifadhi zote zilizopo kwenye mkoa wetu, lakini na KINAPA mtoe ushirikiano kwa wananchi wanaozunguka hifadhii na mhakikishe usalama wao, suala hili litasaidia kuondoa migogoro baina yenu na wao”alisema

Alisema kila wakati kumekuwepo na malalamiko ya wananchi juu ya usalama wao pindi wanapokutana na askari wanaolinda mlima Kilimanjaro.

“Usalama wa mlima ni pamoja na usalama wa wananchi wanaoendesha maisha yao katika eneo la mlima, wananchi ndio asili ya usalama wa mlima la sivyo wangeharibu mazingira tusingeukuta mlima.

“Watu wengine wanapenda kuidharau Tanzania kwasababu ya unyenyekevu wetu, lakini pia tunaheshimu wengine na mipaka yao na tamaduni zao, hatupendi kuwaingilia na sisi wasituingilie”alisema.

Aidha alisema Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kuongezewa hifadhi nyingine sita za kuzisimamia kunaongeza wigo wa utalii na kuongeza mapato.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Tanapa, Kamishna Mwandamizi wa Hifadhi Kanda ya Kaskazini, Herman Batiho, alisema watu waliopandisha bendera kwenye mlima huo ni 40 ambapo imejumuisha wadau wa utalii, Kinapa, Tanapa, Jeshi la Kujenga Wananchi (JWTZ) na wanahabari.

Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Angela Nyaki, amewahakikishia wapanda mlima hao kuwa usalama wao utaimarishwa katika kipindi chote wawapo mlimani.

Naye kiongozi wa msafara wa wapanda mlima hao kutoka Jeshi la wananchi wa Tanzania JWTZ, Kanali Machela Mwise, aliahidi atashirikiana vyema na wapanda mlima wenzie ili kufikisha bendera katika Kilele cha mlima kilimanjaro kama ishara ya uzalendo wa kweli.

Wadau hao wanatarajiwa kushuka Desemba 11 mwaka huu na wanaongozwa na kaulimbiu “hifadhi mpya sita burudani mpya fursa mpya”.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles