27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bastian Schweinsteiger: Miaka 12 imetosha kuitumikia timu ya taifa

Bastian SchweinsteigerNA BADI MCHOMOLO

SOKA la nchini Ujerumani limekuwa tofauti na mataifa mengine kwa kuwa taifa hilo lina aina ya soka la kipekee ikidaiwa kwamba, wachezaji wa nchi hiyo wanatumia nguvu nyingi tofauti na sehemu nyingine.

Kwa hali hiyo ni wazi kwamba wachezaji wake hawawezi kulitumikia soka kwa miaka mingi sana kabla ya kuchoka na kupunguza kasi uwanjani.

Soka la kisasa linatumia akili nyingi kuliko nguvu, japokuwa kuna wakati nguvu zinahitajika kwa ajili ya kulazimisha matokeo, lakini akili zinahitajika zaidi.

Tofauti na walinda milango, wachezaji wa kawaida nchini humo soka lao linaweza kumalizika wakifikisha miaka 30, lakini kwa walinda milango wanaweza kufikisha miaka hiyo na bado wakafanya vizuri, lakini kwa wachezaji wa ndani uwezo wao unapotea.

Nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani, ambaye alikuwa anacheza nafasi ya kiungo katika timu hiyo ya taifa, Bastian Schweinsteiger, tayari ametangaza kustaafu kuitumikia timu ya taifa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 31, alitamani kuendelea kuitumikia timu hiyo lakini umri wake umefikia wakati wa kushindwa mikiki mikiki ya wachezaji chipukizi ambao wanaonekana kuwa na nguvu pamoja na kasi.

Ametangaza kustaafu kuitumikia timu hiyo mara baada ya kuichezea michezo 120 na kufunga mabao 24 tangu apate nafasi ya kuwa mchezaji wa timu hiyo mwaka 2004.

Ni miaka 12 tangu alipopata nafasi ndani ya timu hiyo, lakini sasa ni wakati sahihi wa kuwaaga mashabiki wake na kuwashukuru kwa kile ambacho wamemfanyia na alichowafanyia.

Uwezo wa mchezaji huyo kuwa chini ulizidi kuonekana tangu kuanza kwa michuano ya Euro 2016 nchini Ufaransa, ambapo mchango wa mchezaji huyo ulionekana kuwa mdogo, lakini alilazimisha huku akiwa na lengo la kutaka kuwa mfalme wa kuchukua taji hilo ila hakuweza kutokana na ushindi kuwa mkubwa kutoka kwa mataifa mengine.

Hata yeye mwenyewe anaamini kuwa kocha wa timu hiyo, Joachim Low, alimpa nafasi kwa mara ya mwisho ili aweze kutangaza ufalme wake, lakini hawakufanikiwa.

“Nimetoa shukrani zangu kwa mashabiki, Shirikisho la Soka Ujerumani na Kocha Mkuu wa timu ya taifa Joachim Low.

“Michezo 120 niliyocheza nikiwa katika timu ya taifa ilinifanya niwe katika mafanikio makubwa ya soka ndani ya taifa langu.

“Low alifahamu umuhimu wa michuano ya Euro 2016 iliyofanyika nchini Ufaransa kwa sababu nilitaka kuwa bingwa wa michuano hiyo ambayo Ujerumani haijafanikiwa kuchukua tangu mwaka 1996,” alisama Schweinsteiger.

Hata hivyo, mchezaji huyo kwa sasa ana wakati mgumu katika kikosi chake cha klabu ya Manchester United chini ya kocha mpya, Jose Mourinho.

Kocha huyo amedai kuwa mchezaji huyo hana nafasi ndani ya kikosi hicho, hivyo afanye mipango ya kutafuta timu ya kuitumikia katika kipindi hiki cha usajili.

Hii yote ni kutokana na umri wake kuwa mkubwa na kutumia nguvu nyingi katika Ligi ya Ujerumani huku akiwa katika klabu ya Bayern Munich tangu mwaka 2002 hadi 2015.

Kwa soka la ushindani wa sasa ni vema akatafuta sehemu sahihi ya kumalizia soka lake, kama ilivyo kwa Steven Gerrard ambaye yupo nchini Marekani pamoja na Andres Pirlo, Xavi Hernandes ambao wote wana umri zaidi ya miaka 30 na wameamua kwenda kumaliza soka lao sehemu ambayo haina mikiki mikiki mingine kama ilivyo kwenye ligi walizotoka.

Kwa sasa, Schweinsteiger hawezi kucheza tena soka la ushindani kama ilivyo zamani na amefanya maamuzi sahihi ya kuachana na timu ya taifa kwa kuwa hawezi tena kutoa mchango mkubwa kama ilivyo mwaka 2014 ambapo aliipa ubingwa wa Kombe la Dunia timu hiyo.

Sasa ni wakati sahihi wa kuwapisha vijana ambao wana ndoto ya kulisaidia taifa katika michuano mbalimbali ya kimataifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles