BASI, LORI YAGONGANA DARAJA LA WAMI

0
702

 

 

Na MWANDISHI WETU


Basi la Kampuni ya Kidio One, limegongana uso kwa uso na lori la mizigo katikati ya daraja la Mto Wami, mkoani Pwani jana asubuhi.

Ajali hiyo imethibitishwa kutokea na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa aliyeeleza kuwa ilitokea jana asubuhi baada ya breki za basi hilo kufeli.

Alisema katika ajali hiyo, basi la Kidio One lililokuwa likitokea Dar es Salaam, lilipitiliza na kukutana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Tanga ambalo tayari lilishafika katikati ya daraja hilo.

“Ni kweli ajali hiyo imetokea na RCO wangu yuko huko, tunashukuru kwamba haina madhara kwa binadamu baada ya abiria wote kutoka wakiwa salama, wametafutiwa utaratibu wa kupandishwa kwenye mabasi mengine na kuendelea na safari,” alisema Kamanda Wankyo.

Alisema wapo abiria wachache waliopata mshtuko kutokana na kishindo cha ajali hiyo, lakini hakuna aliyejeruhiwa.

Ajali hiyo ilisababisha taharuki na usumbufu kwa watumiaji wa barabara hiyo baada ya kuzuia kwa muda magari yatokayo mikoa ya Kaskazini na yanayotoka Dar es Salaam ambayo yalilazimika kusubiri kwa muda hadi magari yaliyogongana yalipoondolewa kwenye daraja.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here