23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Basi, Hiace zaua tena

wer

Na JUDITH NYANGE-MWANZA

WATU 13 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha basi la Super Shem lenye namba za usajili T 874 CWE lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Mwanza na Hiace yenye namba T 368 CWQ iliyokuwa ikitoka Jijini Mwanza kuelekea Wilaya ya Kwimba.

Katika ajali hiyo mfanyabaishara ndogo ndogo maarufu machinga, Peter Tobari, aliokoa maisha ya abiria zaidi ya 30 kwa kumsaidia dereva wa basi la Super Shem ambaye alikuwa amekandamizwa miguu na basi hilo baada ya kugongana na Hiace.

Ajali hiyo imetokea siku mbili baada ya ile ya basi la Kampuni ya New force iliyotokea mkoani Njombe  ikihusisha basi lenye namba T 429 DEU lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma, ambapo watu 12 walifariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa vibaya.

Katika ajali ya Mwanza, gari dogo aina ya Hiace liligongana uso kwa uso na basi la Super Shem na kusababisha vifo hivyo na wengine 10 kujeruhi.

Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kidogo cha mabasi cha Hungumalwa njia panda ya Shelui na Mwamashimba katika Kijiji cha Mwamaya wilayani Kwimba mkoani Mwanza.

Ilielezwa katika tukio hilo, dereva wa Hiace aliingia barabara kuu ya Mwanza-Shinyanga bila kuchukua hadhari na hivyo kukutana na basi hilo.

Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema baada ya ajali hiyo watu 10 walikufa papo hapo na wengine 11 kujeruhiwa, ambapo mmoja alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba na wawili walifariki dunia wakati wakipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi kwa matibabu zaidi.

SIMULIZI

Akisimulia ajali hiyo, mfanyabiashara Tobari alisema baada ya magari hayo kugongana dereva wa basi lao alijaribu kuliepusha kupinduka, lakini alishindwa kutokana na kubanwa miguu.

Macginga huyo alishika usukani na kuliongoza gari hilo hadi kuliegesha pembeni na kufanikiwa kunusuru maisha ya abiria waliokuwemo ndani ya basi hilo.

“Baada ya kugongana, upande wa dereva wa gari la basi letu (Super Shem) uliharibika vibaya na wakati  dereva akijaribu kusogeza gari hilo pembezoni mwa barabara ili lisipinduke alishindwa kutokana na bodi la mbele na usukani wa gari kumkandamiza miguu.

“Nilipoona usukani umeshuka  na dereva hawezi kufanya lolote niliushika na kumsaidia kulisogeza pembeni mpaka nilipofanikiwa kuegesha na kulinusuru lisipinduke na kuhatarisha zaidi maisha ya abiria wenzangu.

“Baada ya hapo  nilimtoa dereva ambaye alikuwa amekandamizwa sana sehemu ya miguu na kutafuta usafiri kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Misungwi ambako anatibiwa,” alisema.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, Dk. Bethod Nchemba, akizungumzia ajali hiyo alisema walipokea  majeruhi 10  wakiwemo wanaume na wanawake watano ambapo mmmoja alikuwa na hali mbaya  na alifariki akiwa mapokezi wakati akiendelea kupewa huduma.

Aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Monica Shija, Christina Costantine, Theresia Majenga wote wakiwa wakazi wa Kijiji cha Gulumwa wilayani Kwimba, Lwinzi Kope mkazi wa Kijiji cha Chaselwe, Mabula Magi wa Rukwa, Isaya Deogratius mkazi wa Mbande, Moses Kamel wa Kijiji cha Bupamwadomu, George Ndila mkazi wa Sangu, Kondakta wa hiace aliyefahamika kwa jina moja la Poni pamoja na mtu mmoja mwanaume, mama mmoja na mtoto ambao hawajafahamika wote wakiwa ni abira wa Hiace.

Alisema  majeruhi watatu wanaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo na miili tisa kati ya 11 imeshatambuliwa isipokuwa mwili wa mama mmoja na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 5 na majeruhi sita wamelazimika kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa matibabu zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles