24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

BASHIRU: HAKUNA CHAMA CHA KUSHINDANA NA CCM

Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema chama hicho kinaendelea kuimarika  na hakuna chama chochote nchini kinachoweza kushindana nacho kwenye ulingo wa siasa za ushindani wa sera za maendeleo kwa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa   wilayani Chakechake Kisiwani Pemba jana, katika mwendelezo wa ziara yake ya kujitambulisha kwa wanachama.

Alisema kutokana na uimara huo hakuna chama kingine mbadala wa CCM.

Alisema ni CCM pekee ambayo ina uwezo wa kushuka kwa wananchi, nyumba kwa nyumba na kuratibu kero zao kisha kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Dk. Bashiru aliwahakikishia wanachama na viongozi wa CCM  kutambua kuwa chama hicho tawala kitapata ushindi wa historia mwaka 2020   nchi nzima kuliko ushindi unaopatikana kwa sasa katika uchaguzi mdogo unaoendelea katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema sababu za kushinda na kusambaratisha upinzani zipo kwa vile  vyama vya upinzani nchini vimekosa mwelekeo na ndiyo maana wanachama wake wanahamia CCM kwa wingi.

Alisema Tanzania inahitaji vyama vya siasa imara vitakavyolinda na kuhubiri misingi ya utaifa na umoja na msikamano, bila ya kujali tofauti za siasa.

Katibu Mkuu huyo wa CCM aliwataka wanachama wa vyama vya upinzani Kisiwani Pemba wajitafakari kwa kujitawala kwa fikra kwa kujiunga na CCM.

Alisema hiyo ni kwa vile  Chama cha CUF hakina tena mvuto kwa jamii kutokana na tabia ya unafiki na uongo inayofanywa na viongozi wakuu wa chama hicho.

“Wanachama wa vyama vya upinzani njoo CCM, huku tupo shwari na tumekamilika kila idara wala msihofu chochote hakuna mtu yeyote wa kuwagusa.

“… na wale wote waliojiunga na chama chetu leo nahakikishieni kuwa mtafaidika na siasa safi na demokrasia iliyotukuka.

“Pia wana CCM wenzangu, hawa wenzetu wanaojiunga na CCM wapokeeni na kuwathamini kwa sababu  wamefanya uamuzi sahihi ambao hawataweza kuujutia,” alisema Dk. Bashiru.

Dk.Bashiru alitangaza rasmi kuwa CCM kitaendelea kuvunja ngome zote za upinzani kabla ya mwaka 2020 kutokana na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya mwaka 2015/2020.

Alisema dhamira ya taasisi hiyo kwa sasa ni kuendeleza kwa vitendo mambo mema yaliyoasisiwa na vyama vya ukombozi vya ASP na TANU vilivyoungana na kuzaliwa kwa CCM.

Aliwataka wanachama wa CCM kutambua kila mmoja anatakiwa kulinda Muungano, Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa sababu  tunu hizo ndiyo chimbuko la mafanikio yaliyopo hivi sasa.

Katika mkutano huo, Dk.Bashiru aliwapokea wanachama wapya 62 waliotoka chama cha CUF na kujiunga na CCM Kisiwani Pemba.

Aliwapongeza wanachama wajumbe wote wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa kumuamini kisha kupendekeza ateuliwe kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM.

Aliahidi kuwa atatumia nafasi yake kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo ndani na nje ya CCM.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk.Abdulla Juma Saadalla, alisema kazi kubwa ya CCM kwa zama za sasa ni kutekeleza kwa vitendo dhana ya CCM mpya na Tanzania mpya kwa maendeleo ya jamii.

Alisema miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwa ufanisi kisiwani Pemba ukiwamo mfuko wa maendeleo wa TASAF na kuongeza bei ya zao la karafuu, ni kutokana na utekelezaji mzuri wa sera za CCM.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma, alisema ndani ya mkoa huo inaendelezwa mikakati ya kuhakikisha CCM inashinda kwa ngazi zote katika uchaguzi mkuu ujao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles